Baadhi ya wanyama waliouliwa na majangili kwa ajili ya kitoweo |
Watuhumiwa wa Ujangili 2617 wamekamatwa kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 katika maeneo ya mapori ya akiba ,mapori tengefu na hifadhi za jamii(WMA) ambayo kampuni sita zilizo chini ni mfuko wa kusaidia uhifadhi wa Friedkin(FCF) zimewekeza, huku zaidi ya sh 4.5 bilioni zikitumika katika vita dhidi ya ujangili.
Watuhumiwa hao wamekamatwa, kwa ushirikiano pia na maafisa
wa Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori(TAWA) ambao kisheria ndio
wanasimamia maeneo hayo .
Akizungumza na princemedia Meneja miradi wa FCF ,Nana Gross
Woodley alisema watuhumiwa hao wa ujangili walikamatwa katika maeneo
sita yenye zaidi ya ekari 2.8 milioni ambayo kampuni zilizo chini ya
mfuko huo,zinafanya kazi za uwindaji wa kitalii, utalii wa picha na
uhifadhi.
Kampuni hizo ni Tanzania Game Tracker Safari, Wenget Windrose Safari na Mwiba Holdings.
Maeneo ambayo kampuni hizo, zimewekeza ni Pori la akiba la
Maswa, maeneo ya Mbono na Kimali,eneo la Mwiba Ranchi na hifadhi ya
jamii ya Makao, wilayani Meatu, eneo la Uvinza,Pori la akiba ya Ugala
kusini na kaskazini, pori la akiba ya Moyowosi eneo la kusini na pori
tengefu la ziwa Natroni.
Woodley alisema, katika kipindi cha miaka mitatu, kila
mwaka FCF imekuwa ikitumia kati ya sh 1.4 bilioni hadi 1.7 bilioni,
katika vita dhidi ya ujangili, ikiwepo kununua magari,kuajiri askari
ulinzi,kununua vifaa vya ulinzi na kuendesha operesheni mbali mbali
dhidi ya ujangili.
Alisema kutokana na jitihada za FCF, kwa kushirikiana na
TAWA na vyombo mbali mbali vya ulinzi na usalama, matukio ya ujangili
yamepungua kutoka matukio 1226 mwaka 2013 hadi kufikia matukio 721
mwaka 2015.
Akitoa mchanganuo wa majangili waliokamatwa katika kipindi
cha miaka mitatu, alisema majangili wa nyama kwa ajili ya chakula
waliokamatwa ni 304, majangili wa tembo, 18,majangili wa mbao 283,
majangili wa urinaji asali 6 na majangili ya uvuvi haramu 142.
"katika kipindi hiki cha miaka mitatu 2013 hadi 2015,
tumekamata wafugaji walioingiza mifugo hifadhini,853,wajangili waliokuwa
wakichoma mikaa 82, waliokuwa wameingia hifadhini kinyume cha sheria
881,walioingia kuchoma moto hifadhini 49"alisema
Mkurugenzi wa Mamlaka ya usimamizi wanyamapori(TAWA),Dk
James Wakibara, ambaye mamlaka yake ndio inasimamia maeneo yote uhifadhi
nje ya hifadhi za Taifa, akizungumza na princemedia hivi karibuni
alisema, jitihada za serikali na wadau mbali mbali ikiwepo wawekezaji
wameweza kupunguza sana matukio ya ujangili.
Alisema kila mawaka matukio ya ujangili yamekuwa yakipungua
hasa ujangili wa Tembo ambao unatoweka kabisa kutokana na ulinzi katika
maeneo ya hifadhi na nje kuimarishwa.
Hata hivyo, alisema changamoto kubwa sasa katika uhifadhi ni tatizo la ongezeko la mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa.
"TAWA kwa kushirikiana na wadau wengine, tuna mikakati
mbali mbali ya kukabiliana na matukio yote ya ujangili na kiasi kikubwa
imefanikiwa lakini wito ni kwa wananchi wanaoishi jirani na hifadhi ni
kuwa mabalozi wa kupinga matukio ya ujangili"alisema.
Post a Comment