Wazazi na Walezi wa wanafunzi wa shule ya Msingi Nalopa
wakimsikiliza Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna Charles
Mkumbo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe ya Mahafali ya kuhitimu
darasa la Saba
Mgeni rasmi wa sherehe ya Mahafali ya darasa la Saba katika shule
ya Msingi Nalopa Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP)
Charles Mkumbo akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles
Mkumbo akiwahutubia wageni waalikwa katika sherehe za Mahafali ya
wanafunzi wa darasa la Saba wa shule ya Msingi Nalopa
Wito umetolewa kwa wazazi, na kuelezwa kwamba mbali na
kujitahidi kuwasomesha watoto wao katika
shule mbalimbali kwa lengo la kuwapatia elimu bora wametakiwa pia kuzingatia kuwapa
makuzi mema ili uhalisia wao kimuonekano uendane na elimu wanayoipata.
Hayo yameelezwa jana na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha
Naibu Kamishna (DCP) Charles Omari Mkumbo wakati wa sherehe ya mahafali ya
wahitimu wa darasa la saba katika shule ya Msingi Nalopa iliyopo jijini Arusha.
Kamanda Mkumbo ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika mahafali
hayo alisema kwamba, wanafunzi hao kwa sasa wanakwenda katika hatua nyingine ya
kimasomo lakini pia umri wao unaongezeka na kukumbana na changamoto mbalimbali,
hivyo wazazi wanatakiwa waendelee kuwakuza kimaadili ili elimu yao iwe na
manufaa kwao na kwa jamii.
Alisema elimu wanayoipata ikiendana na maadili itawasaidia
kuepuka kujiingiza katika vitendo vya uhalifu kama vile matumizi ya dawa za
kulevya na uhalifu mwingine wowote na hatimaye kuonekana kuwa wa thamani
machoni mwa watu.
Kamanda Mkumbo aliwataka wanafunzi hao kuongeza bidii katika
masomo yao hasa ya Sayansi ili idadi ya wataalamu wengi katika kada mbalimbali iongezeke
hasa katika huu ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia ambao ushindani wa soko la
ajira umekuwa mkubwa.
Akimkaribisha mgeni rasmi kuwatunuku vyetu wahitimu hao ambao
walifanya vizuri kimasomo, kinidhamu, uongozi, kimichezo na kujituma, Mlezi wa
shule hiyo Balozi Mstaafu Bw. Daniel Ole Njoolay alitumia nafasi hiyo
kumpongeza Kamanda huyo kwa kuzidi
kuimarisha hali ya usalama katika mkoa wa Arusha pamoja na changamoto
mbalimbali zilizopo.
Awali akizungumza
katika Mahafali hayo Meneja wa shule hiyo yenye wanafunzi 461 Bw. Edward
Njoolay alisema kwamba, awali akisoma wasifu wa shule hiyo alisema kwamba mwaka
1999 ilikuwa kama “Day Care” lakini ushawishi wa wazazi uliwawezesha kufanikiwa
kufikia hatua kubwa kimiundo mbinu na kitaaluma.
Shule hiyo imefanikiwa kutoa wahitimu wa darasa la saba mara
nane ukiondoa wahitimu wa jana na wote walifanikiwa kufaulu na kuendelea na
masomo ya Sekondari ambapo mwaka 2016 ilishika nafasi ya saba katika shule bora
za Halmashauri ya jiji la Arusha zilizofanya mtihani wa darasa la saba.
Post a Comment