FARU akiwa anakula majani maalumu |
Wanyama wanaopewa ulinzi makini FARU ambao wapo hatarini kutoweka wakiwa wanachungwa katika kreta ya Ngorongoro |
Serikali imetakiwa kuongeza jitihada za kuwahifadhi wanyama pori walio hatarini kutoweka wakiwepo Faru na Tembo.
Akizungumza hivi karibuni jijini hapa Mhadhiri wa chuo kikuu cha Dar es
Salaam, Idara ya wanyama na uhifadhi wa viumbe pori, Dk Hamfrey Kiwia, alisema Tanzania ilikuwa ni miongoni ya nchi
zilikuwa na wanyama pori wengi miaka ya 1960 lakini sasa wamepungua.
Dk Kiwia ambaye ni mtafiti wa Faru, alisema miaka ya 1968
katika eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro pekee, kulikuwa na Faru 108
lakini kutokana na matukio ya ujangili
hadi kufikia mwaka 1977 walibaki
Faru 25 tu.
Hata hivyo, alisema jitihada ambazo zinafanywa sasa na
wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake, Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro(NCAA)
na Shirika la hifadhi za Taifa(TANAPA),kuwahifadhi na kuwarejesha wanyama
waliotoweka zinapaswa kuungwa mkono.
Dk
Kiwia alisema kwa sasa wanyama kama Faru wameongezeka Ngorongoro na
kufikia zaidi ya 50 tofauti na miaka 10 iliyopita na pia wanyama wengine
kama Tembo wameongezeka katika hifadhi za Taifa.
“Ni lazima tuwatunze wanyama hawa kwa gharama zozote kwani,
ni urithi wetu na kama tukiwaacha bila matunzo ya uhakika ipo siku watatoweka
wote”alisema
Kwa upande wake, Mwenyekiti
wa kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta Nditiye
alisema, uhifadhi wa wanyama waliohatarini kutoweka hauepukiki.
“dhana nzima ya uhifadhi ni lazima iende sambamba na
kuhifadhi misitu na wanyamapori ambao wapo hatarini kutoweka kama Faru, Tembo, Mbwamwitu na wengine”alisema
Akizungumzia uhifadhi wa Faru katika eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani alisema wizara hiyo, inaunga mkono
uhifadhi wa Faru bila kujali gharama zake.
Mhandisi Makani alisema, katika kuendeleza uhifadhi, suala
la gharama sio kipaumbele kwani wanyama ambao wapo hatarini kutoweka lazima
wahifadhiwe na kulindwa kwa gharama zote.
Post a Comment