Wito huo umetolewa na Mratibu wa afya ya mama na mtoto wa Halmashuri ya Ngorongoro Bi. Anna Masago katika warsha ya kupinga ukeketaji inayoendelea katika halmashauri hiyo ambayo imeandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Masago amesema kutokana na jamii hizo kuendelea kushikilia mila potofu hasa ya kuwakeketa watoto wakike, kumekuwa kunawasababishia kupata maumivu makali wakati wa kujifungua na hatimaye kusababisha vifo kwa wanawake hao.
“Ninyi mangariba acheni kuwakeketa wanawake, mnawasababishia maumivu makali na mnasababisha vifo kwa hawa wanawake,” alisema Masago.
Pia Masago ametaja madhara mengine wanayo kumbana nayo wanawake walio keketwa kuwa ni kufanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua, kuchanika na kutokwa damu nyingi na kupata ugonjwa wa fistula.
Awali akitoa takwimu za hali ya ukeketaji mbele ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngorongoro, Raphael Siumbu kwa mwaka 2016, 17 na 18, Masago amesema kwa mwaka 2016 wanawake2991 waliofika kujifungua katika vituo vya afya walibaini wanawake 1783 walikuwa wameketwa (66%), mwaka 2017 wanawake 2731 walio fika kujifungua katika vituo vya afya walibaini wanawake 2201 walio keketwa sawa na asilimia 81 na kuanzia January hadi Machi mwaka huu, kati ya wanawake 869 waliofika kujifungua 751 walikuwa wameketwa sawa na asilimia 86.
Akizungumzia takwimu hizo, Siumbu amesema kuwa kuna kila sababu ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii hizo ili ziweze kuachana na mila potofu ya ukeketaji ili kusaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto pindi wanapo jifungua.
“Takwimu zinasikitisha na inaonesha wazi jamii hazitaki kuachana na mila potofu. Hivyo niwaombe wananchi wa Ngorongoro tuachane na vitendo vya ukatili wa kijinsia,” alisema Siumbu .
Warsha hiyo iliyoandaliwa na UNESCO, inashirikisha Mtandao wa Radio za Kijamii Tanzania (TADIO) kwa lengo la kuendesha kampeni ya mwezi mmoja ya kupinga vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto wilayani Ngorongoro, ukiwepo ukeketaji.
Post a Comment