Katibu Mtendaji wa TATO, Siriri Akko akichangia mada katika kikao kazi hicho juu ya maazimio ya kuondoa kero na changamoto wakutanazo watoa huduma za utalii nchini |
Add caption |
Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro(NCAA) na Chama cha
Mawakala wa Utalii(TATO), wamefikia makubaliano ya kuondoa vikwazo baina
yao na hivyo kushirikiana katika kukuza utalii hapa nchini.
Makubaliano hayo, yalifikiwa jana katika kikao kazi
kilichofanyika Arusha katika hotel ya New Arusha, baina viongozi NCAA,TATO na Kampuni za
Utalii ambazo hivi karibuni zilitajwa kuwa huenda zingezuiwa kuingiza
watalii katika hifadhi ya Ngorongoro.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu mhifadhi wa NCAA
anayeshughulikia Huduma za Shirika Asangye Bangu alisema,NCAA imejipanga
kuboresha huduma kwa watalii na kuondoa changamoto zinazowakabili wenye
makampuni ya Utalii.
"Kikao chetu kimekwenda vizuri, NCAA tutaendelea kuboresha
mifumo ya malipo, kuboresha mawasiliano baina yetu na mawakala wa utalii
lakini pia kutatua changamoto kadhaa, ikiwepo barabara ndani ya
hifadhi"alisema
Alisema katika kukabiliana na kero ya barabara, NCAA
inatarajiwa mwezi wa nane mwaka huu, kuanza ujenzi wa barabara ya kutoka
geti la kuingia Ngorongoro hadi geti la kuingia Serengeti yenye urefu
wa kilomita 83 kwa kuweka tabaka gumu juu.
"hii ni kero ya muda mrefu ya makampuni ya Utalii lakini
sasa Shirika la umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi na
Utamaduni(UNESCO)limetukubalia kuijenga barabara hii na ikikamilika
tunaimani barabara itadumu kwa zaidi ya miaka 40"alisema
Awali Katibu Mtendaji wa TATO, Siriri Akko alisema, katika
siku za karibuni kuliibuka taarifa za kuwachanganya baadhi ya wanachama
wao juu ya kuzuiwa kuingia ngorongoro kupeleka watalii.
Hata hivyo, alisema baada ya kupata maelezo kutoka NCAA
wamefikia makubaliano ambayo lengo lake ni kuboresha sekta ya utalii
nchini na pia kuondoa changamoto zinazowakabili.
"kikao chetu kimekwenda vizuri na ile hofu ya kampuni
kuzuiwa sasa haipo na tunaimani kampuni zote zitafuata sheria na
taratibu za kufanya biashara ya utalii hapa nchini"alisema
Akizungumza katika kikao hicho,Mkurugenzi wa kampuni ya
Utalii wa Shidolya, Lazaro Mafie alisema ni muhimu kuwepo na mawasiliano
ya mara kwa mara baina ya NCAA na makampuni ya utalii ili kutatua kero.
Mafie alisema wao kama wamiliki wa makampuni ya Utalii,
wateja wao ni watalii sawa na NCAA ambayo uwepo wao unategemea watalii
hivyo ni lazima kuwepo na mawasiliano mazuri baina yao.
"kuna changamoto kadhaa ambazo tunakabiliana nazo lakini
tunaimani sasa zitafanyiwa kazi ili kuboresha sekta ya utalii hapa
nchini"alisema.
Post a Comment