WAMILIKI wa shule binafsi sasa wameomba kuingia ubia na Serikali ili
wapewe ruzuku kuwezesha shule zao kudahili wanafunzi wa kidato cha
kwanza, kwa maelezo kuwa shule hizo zitasaidia kuondokana na kero ya
baadhi ya wanafunzi wanaofaulu kukosa nafasi katika shule za serikali.
Hata hivyo, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi
imekataa ombi hilo kwa maelezo kuwa serikali ina shule za kutosheleza
mahitaji yaliyopo na haihitaji msaada wa shule binafsi katika
kukabiliana na changamoto zilizopo katika suala la vyumba vya madarasa.
“Serikali hatuna mpango wa kuingia ubia na shule binafsi katika kudahili
wanafunzi wa kidato cha kwanza, sisi tumeamua kutoa elimu bure na
tumeboresha mazingira ya shule zetu, wao wanaendesha shule zao kwa
kulipisha na waendeshe peke yao,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo, Profesa Simon Msanjila.
Ombi la Tamongsco Kupitia Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa shule na
Vyuo visivyo vya Serikali (Tamongsco), wamiliki hao wameiandikia Wizara
ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kuomba wizara
iwashirikishe katika udahili wa wanafunzi 12,000 ambao wamefaulu
mitihani ya darasa la saba mwaka jana, lakini kutokana na ukosefu wa
madarasa hawataweza kwenda kidato cha kwanza.
“Kila mwaka tunaiomba Serikali ituondolee kodi, badala yake shule
binafsi zipewe ruzuku ili watoto wanaokosa nafasi za kusoma katika shule
za Serikali kila mwaka wapate elimu hiyo katika shule binafsi kwa
mikataba maalumu ya ubia wa sekta ya umma na binafsi,” alisema Katibu
Mkuu wa Tamongsco, Benjamin Nkonya katika barua yao waliyoiwasilisha
wizarani.
Nkonya alisema baadhi ya madarasa katika shule zisizo za serikali hayana
wanafunzi wakati madarasa katika shule za serikali yamefurika wanafunzi
hadi 200 kwa darasa moja, jambo ambalo shule hizo binafsi zinaona
kwamba ni kuwaweka katika mazingira mabovu kabisa ya kujifunzia na
kufundishia wanafunzi hao.
Katibu Mtendaji huyo alisema kama Serikali inatoa ruzuku kwa hospitali
binafsi, ifanye hivyo pia kwa shule binafsi za sekondari ili watoto wote
wa kitanzania waweze kupata elimu kwa usawa. Majibu ya Serikali
Profesa Msanjila alisema kwamba Serikali imeamua kuboresha shule zake na
kutoa elimu bure, jambo ambalo limewavutia wananchi wengi na sasa
wanapeleka watoto wao katika shule za serikali tofauti na miaka ya
nyuma.
Alisema kutokana na hali hiyo serikali haina mpango wa kuingia ubia na
shule binafsi, badala yake itaendelea kutoa miongozo ya elimu
inayoelekeza sera za elimu zinazotakiwa kufuatwa na shule ambazo sio za
serikali na sio kuingia nazo ubia katika kudahili wanafunzi.
“Hawa tulitaka kuweka ada elekezi, lakini walitumia wanasiasa kupinga,
kwa madai kwamba tunaingilia elimu ambayo serikali haihusiki, jambo hilo
serikali imeamua kuachana na nalo ili soko liweze kuamua,” alisema
Profesa Msanjila.
Aliongeza kuwa serikali imekuwa inaingia ubia katika sekta ya afya
katika wilaya au mkoa ambako hakuna hospitali kubwa ya serikali na hivyo
kulazimika kuingia ubia na hospitali binafsi au za mashirika ya dini
zilizoko katika wilaya hizo.
“Sasa kwenye sekta ya elimu, serikali ina shule kila kata na kila
kijiji, sasa huo ubia wanaotaka tuingie kwa sababu zipi? Hakuna sehemu
ambako serikali haina shule,” alisisitiza Naibu Katibu Mkuu huyo.
Alisema baada ya kukataa ada elekezi, serikali iliona kuwa shule hizo
zisizo za serikali zinafanya biashara na hazitoi huduma kama zinavyodai
ndio maana zinalipa kodi zote zinatakiwa kulipwa na kampuni nyingine
inayofanya biashara.
“Baada ya kukataa ada sisi tuliona kwamba hawa wanafanya biashara, hivyo
lazima waendelee kulipa kodi maana hawatoi huduma,” alisema Profesa
Msanjila.
Mtazamo wa Tamongsco Alisema Tamongsco inaona kwamba kuwasubirisha
wanafunzi wengi hivyo kwa muda uliotajwa na serikali wa kujenga madarasa
ndipo wajiunge na kidato cha kwanza kutasababisha malengo ya Matokeo
Makubwa Sasa (BRN) kutofikiwa.
Katika andiko hilo ambalo limesainiwa na Katibu Mtendaji wa Tamongsco,
wanadai kwamba ubia wa sekta ya umma na binafsi katika sekta ya elimu
umeleta mafanikio makubwa nchini Uganda ambako serikali inatoa ruzuku
kwa shule binafsi ambazo ni asilimia 80.
“Tuna ushahidi kwamba nchi nyingine nyingi duniani hutumia mifumo hii ya
PPP na hufanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa elimu yenye ubora wa hali ya
juu kwa gharama nafuu kuliko gharama ambayo serikali ingetoa bila
kutumia mfumo wa PPP,” linasema andiko hilo la Tamongosco.
Wamiliki hao walisema kutokana na tofauti za wamiliki wa shule zetu,
wamependekeza njia za ushirikiano kati ya sekta ya umma na isiyo ya umma
zitumike katika kuondoa changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa kwa
ajili ya wanafunzi 12,422 waliokosa nafasi katika shule za serikali na
wale watakaokosa kwa miaka ijayo.
Miongoni mwa njia hizo ni Mfumo wa Udahili Uliowianishwa ambao lengo
lake ni kuondoa uwezekano wa mwanafunzi mmoja kudahili zaidi ya mara
moja.
Kama ilivyo katika vyuo vikuu. Pia Serikali itenge kiasi cha fedha kwa
mwanafunzi mmoja. Shule husika itatoza ada ya ziada kwa makubaliano na
serikali.
Njia nyingine ni udhamini katika utaratibu huu, ikokotolewe gharama
halisi ya kumsomesha mwanafunzi mmoja kwa mwaka katika shule ya serikali
kwa kila kanda kwa kuzingatia nguvu ya fedha ya mahali husika na
serikali itoe fedha hizo.
Post a Comment