WAMECHARUKA! Baada ya wanaume kusifika kuwa ndio wateja wakubwa wa
minofu ya samaki aina ya pweza na supu yake, hali sasa imebadilika baada
ya kinadada kuonekana pia wakichangamkia kwa wingi bidhaa hiyo.
Uchunguzi wa Nipashe katika maeneo maarufu ya uuzwaji wa pweza na supu
yake jijini Dar es Salaam, unaonyesha kuwa kwa sasa, tofauti na vile
ilivyozoeleka, kinadada na kinamama wamekuwa wakijumuika na wanaume
katika kumla pweza na pia kunywa supu yake.
Maeneo yaliyohusishwa zaidi katika uchunguzi huo ni pamoja na stendi ya
Makumbusho, Mwenge, Tegeta, Ubungo, Mbezi Luis, Buguruni, Tandika na
Mbagala.
Nipashe imebaini kuwapo kwa wateja wanawake wanaofika kwa idadi kubwa
katika maeneo wanayouza pweza na kujumuika na wateja wengine katika
kuchangamkia bidhaa hiyo, tofauti na ilivyokuwa awali.
Kwa wastani, kupitia wauzaji waliozungumza na Nipashe, imebainika kuwa
kuna ongezeko la takribani asilimia 40 ya wateja wanawake, hiyo
ikitokana na wastani wa kuwa na wanunuaji walau wanne katika kila wateja
10.
Awali, ilielezwa na wauzaji wengi kuwa haikuwa ajabu kutopata mteja wa kike walau mmoja wa supu ya pweza kwa siku.
Katika uchunguzi huo, Nipashe imebaini kuwa wako kinamama walioonekana
kujiandaa zaidi kwa kufika na vifaa vya kubebea supu, zikiwamo chupa za
maji zilizotumika huku baadhi yao wakifika kwa wauzaji na vifaa vya
kubebea supu, zikiwamo chupa za maji zilizotumika huku baadhi yao
wakifika kwa wauzaji wakiwa na bakuli maalumu za vyakula maarufu kama
‘hotpot’, chupa ya chai na kuwekewa supu na finyango za samaki huyo.
Wanaume ndiyo waliokuwa wakisifika kwa ulaji wa supu ya pweza uliopamba
moto zaidi jijini Dar es Saalam katika miaka ya hivi karibuni kutokana
na taarifa kwamba pweza husaidia mambo mengi mwilini, hasa katika
kuimarisha urijali.
Baadhi ya wauzaji wameiambia Nipashe kuwa hali sasa iko tofauti sana kwa
sababu wanawake ni miongoni mwa wateja wao wazuri kwa sasa.
“Tena wapo kinadada hawakosi kunywa supu ya pweza walau mara tatu kwa
wiki. Wapo pia ambao kila wanapokuja hunywa hadi vibakuli vitatu vya
supu na pia kutafuna minofu yake,” mmoja wa wauzaji katika eneo la
Makumbusho aliiambia Nipashe.
Muuzaji mwingine katika eneo la Ubungo alisema kabla, alizoea kupata
wateja wachache wanawake na kwamba, wengi wao walikuwa wakiomba
kufungiwa tu vipande vikubwa vya mikia ya pweza na kuondoka navyo; hali
ambayo hivi sasa imebadilika kwa kiasi kikubwa kwa sababu idadi yao wale
wanaofika kununua hivi sasa imeongezeka.
“Kama unavyoona mwenyewe… biashara hii tunaifanya sana kuanzia mida ya
saa moja usiku na kila ukija utawaona kinadada na kinamama wakiwa sehemu
ya wateja wetu. Tunashukuru sana kwa elimu inayoendelea kutolewa kuhusu
faida za pweza mwilini na hilo limechangia kutuongezea wateja na kukuza
mitaji yetu,” alisema muuzaji mwingine katika eneo la Mbagala,
aliyejitambulisha kwa jina moja la Salum.
Muuzaji mwingine katika eneo la Mwenge, alisema kwa eneo analouza yeye,
anakadiria kuwa wateja wanaume na wanawake hufika kwa uwiano sawa.
“Hapa kwangu, wateja wanawake na wanaume hawapishani kwa idadi… kwa
wastani, katika kila wateja 10, watano huwa ni wanawake,” alisema
muuzaji huyo, akiongeza kuwa umaarufu wa pweza na faida zake kwa walaji
unaweza kuwa chanzo cha kuongezeka kwa walaji kinadada katika siku za
hivi karibuni.
SABABU KUONGEZEKA WATEJA WANAWAKE
Wakizungumza na Nipashe, wauzaji wengi walidai kuwa kuenea kwa taarifa
za wataalamu zinazothibitisha ubora wa virutubisho vya samaki pweza
ndiyo sababu ya kuvutika kwa wanawake wengi zaidi katika utumiaji wa
samaki huyo.
“Pweza huliwa kwa idadi sawa majumbani. Lakini haikuwa kawaida kuwaona
kinadada katika maeneo haya ya wazi tunayouza vipande vya samaki huyo
vilivyokaangwa au kuchemshwa pamoja na supu yake.
Haya ni mabadiliko makubwa yenye faida kwetu kwa sababu wateja wanazidi
kuongezeka,” alisema muuzaji mmojawapo katika eneo la Tegeta, aliyedai
kwamba kwa siku huingiza faida ya hadi Sh. 25,000 kutokana na biashara
yake hiyo.
Mmoja wa kina dada waliokutwa wakipata huduma ya supu ya pweza eneo la
Makumbusho na kujitambulisha kwa jina moja la Joyce, aliiambia Nipashe
kuwa yeye alianza kuwa mlaji mzuri wa pweza miaka minne iliyopita baada
ya kujifungua na kubaini maziwa hayakuwa yakitoka vizuri, lakini
alipotekeleza ushauri wa kula pweza usiku na mchana, haikumchukua muda
mrefu kupata nafuu ya tatizo hilo.
“Na tangu hapo nikawa miongoni mwa walaji wakubwa wa pweza kwa sababu
nilikuja kuelezwa faida zake nyingine nyingi kiafya. Hata hivyo, kwa
sababu ya kazi, sipati nafasi ya kujiandalia mwenyewe na ndiyo maana
huwa nakula walau kidogo kwenye maeneo wanayouza mitaani,” alisema
Joyce.
DAKTARI ANENA
Akizungumza na Nipashe kuhusu faida za pweza na taarifa za kuwapo kwa
ongezeko la wateja kinamama, Dk. Damas Mahenda, Mhadhiri Msaidizi katika
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), alisema ni
kweli samaki jamii ya pweza wana faida nyingi mwilini, hivyo si ajabu
kusikia watu wakichangamkia matumizi yake, wakiwamo kinamama.
Dk. Mahenda alisema samaki jamii ya pweza wamejawa na virutubisho
vinavyosaidia mengi ikiwamo kuongeza ashki na kuboresha tendo la ndoa
huku pia minofu ya samaki huyo ikiwa na virutubisho vya kumuwezesha
mwanamke kuwa na sifa halisi za ‘ukike’ na pia mwanaume kuimarika afya
yake.
Alivitaja baadhi ya virutubisho vingi vinavyopatikana kwenye mlo wa supu
au minofu ya pweza kuwa ni pamoja na protini, mafuta (fats), vitamini
B12, selenium, madini chuma (iron), shaba na pia vitamini B6.
“Virutubisho vyote hivi vinapatikana kwa kiasi kikubwa kwenye minofu ya
pweza na karibu vyote ni muhimu katika mwili wa binadamu,” alisema Dk.
Mahenda.
“Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa pweza ana faida nyingi. Na kwa
ufupi, unaweza kumuelezea pweza kwa kumlinganisha na kifurushi cha
virutubisho muhimu vya mwili wa binadamu. Mnofu wa pweza una protini
nyingi kuliko wa kuku. Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa takribani
asilimia 10 ya virutubisho protini nyingi kuliko wa kuku. Baadhi ya
tafiti zinaonyesha kuwa takribani asilimia 10 ya virutubisho vyote
vinavyohitajika mwilini kwa siku hupatikana kwa pweza aliyeivishwa
vizuri,” Dk. Mwindah Abdallah wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) aliwahi
pia kuiambia Nipashe kuhusu faida za pweza, jambo linalochangia
kuongezeka kwa walaji wake wakiwamo wanawake kadri taarifa zinavyozidi
kuwafikia wengi.
Aidha, kupitia mahojiano na Dk. Mahenda, Nipashe ilibaini kuwa faida
nyingine za pweza zinazovutia walaji wengi kila uchao ni pamoja na kuwa
na virutubisho vya selenium vinavyosaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa nguvu
ya tendo la ndoa wanaume na wanawake na pia vipo vinavyosaidia
kuwaongezea wanaume idadi ya mbegu (sperm count).
“Kwa sababu hiyo, supu ya pweza iliyoandaliwa vizuri inaweza kuwasaidia
wanandoa katika kukamilisha jukumu lao la unyumba kwa namna bora zaidi,”
alisema Dk. Mahenda.
Faida nyingine ni ya virutubisho vya pweza ni kusaidia mwili kuukinga
dhidi ya maradhi mbalimbali ya saratani zikiwamo za midomo, tumbo,
utumbo mkubwa, matiti, shingo ya kizazi, na pia saratani ya mapafu;
kuukinga mwili dhidi ya kupungukiwa kwa uwezo wa ubongo hasa kwa watu
wenye umri mkubwa (Alzheimer); husaidia walaji kukabili athari za
maradhi ya pumu; kuongeza uzalishaji wa haemoglobin ambazo ni muhimu
katika damu na hiyo ni kwa sababu pweza ana madini mengi aina ya shaba
na pia kupunguza athari za baadhi ya maradhi ya moyo kwa sababu ya
kuwapo kwa kiwango cha mafuta aina ya ‘omega3 fatty acids’.
Hata hivyo, licha ya faida nyingi za supu ya pweza na minofu yake
mwilini, Dk. Mahenda alitahadharisha juu ya athari hasi zinazoweza
kujitokeza kwa baadhi ya walaji wa pweza kuwa ni pamoja na kushambuliwa
na mzio (aleji).
Nipashe imebaini vilevile kuwa ripoti za tafiti nyingine kuhusiana na
ulaji wa pweza zinaonya kuwa samaki huyo hapaswi kutumiwa sana na kina
mama wajawazito kwa sababu anaweza kusababisha athari zitokanazo na
madini ya zebaki ambayo hupatikana pia mwilini mwake, ijapokuwa huwa ni
kwa kiasi kidogo.
Chanzo: Nipashe
Home
»
HABARI ZA AFYA
»
KITAIFA
»
Matukio
» Sababu za Ongezeko la Wanawake Wanaokunywa Supu ya Pweza YABAINIKA PPITIA HAPA UJIONEE
About Author
Journalist , Enterpreneur, Lecturer and Blogger. Email :ngoboleaa@gmail.com.
Advertisement
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment