KATIBU Mkuu Kanisa la Anglikana Tanzania, Johnson Chinyong’ole amesema
aliyekuwa Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentine Mokiwa
anakabiliwa na mashitaka ya jinai kwa kuingia mikatiba mibovu na
matumizi mabaya ya fedha za kanisa makosa yanayoangukia kuvunja sheria
za nchi.
“Hatujakurupuka kuchukua hatua, ushahidi wote tumeshauwasilisha kwa
vyombo vinavyohusika serikalini, sisi tumetimiza wajibu wetu, hivyo
tunaviachia vyombo vinavyohusika kufanya kazi yake katika eneo hilo la
ubadhirifu wa fedha,” alisema Chinyong’ole.
Alifafanua kuwa wakati wanaenda kutangaza uamuzi wa kumvua uaskofu Dk
Mokiwa juzi kanisa la Ilala, walienda kutoa taarifa kwa msajili wa vyama
ambaye ndiye anayesajili makanisa, lakini pia wameshatoa taarifa katika
ofisi za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa ajili ya
kuchukua hatua za kisheria.
Alitaja sheria alizovunja Dk Mokiwa kuwa ni sheria ya miunganiko ya
wadhamini sura ya 318, sheria ya ardhi namba 4 ya 1999 na sheria ya
mipango miji sura ya 355 kwa kuruhusu mabadiliko ya matumizi ya ardhi
katika shamba la kanisa la Mtoni Buza na eneo la Kanisa la Mtakatifu
Mariam Kurasini.
“Sisi tunasubiri mrejesho kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Rita na kwa
Msajili wa vyama vya kiraia,” alisema katibu mkuu huyo wa kanisa la
Anglikana Tanzania.
Alifafanua kuwa katika mashitaka 10 anayokabiliwa nayo, shitaka la tatu
ndilo ambalo ni la ubadhirifu wa mali za kanisa ndilo ambalo linaifanya
serikali kuingilia kati.
Alisema makosa ya Dk Mokiwa yanahusisha pia kughushi na akatoa mfano wa
kuingia mikataba kwa kuwatumia watu ambao si wadhamini wa kanisa hilo
wakati sheria inamtaka atumie wadhamini wawili wanaosimamia mali za
kanisa, pamoja na kutumika kwa muhuri bandia wakati sheria inasisitiza
muhuri unaotumika ni ule wa moto.
Katibu Mkuu huyo alisema ripoti ya tume iliyoundwa kuchunguza tuhuma
dhidi ya askofu hiyo yenye kurasaa 173 imewasilishwa pia serikalini ili
vyombo vinavyohusika kufuatilia tuhuma hizo viweze kujiridhisha wakati
vinapoenda kuchukua hatua.
“Hakuna mtua aliyeonewa, wala kuchafuliwa, hizi ni tuhuma za ubadhirifu
wa mali ya kanisa, lazima vyombo vya dola vihusike hapa,” alisema katibu
mkuu huyo na kuongeza kuwa serikali ndio inayotakiwa kuchukua hatua kwa
sababu tume iliyoundwa na kanisa imeshaweka hadharani ushahidi kwa
lengo la kuokoa mali za kanisa.
Amevunja kiapo cha utii Kwa hali hiyo jambo hilo tayari wameliwasilisha
kwa msajili wa vyama ambaye ndiye msajili wa kanisa hilo na pia
wamewasilisha suala hilo kwa wakala wa vizazi na vifo (Rita) kwa kuwa
sheria ya nchi iliyovunjwa ni ya udhamini.
Akizungumza na gazeti hili jana, Chinyong’ole alisema kwa mujibu wa
katiba ya kanisa hiyo ya mwaka 1970 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004,
pamoja na Dk Mokiwa kugoma kung’oka madarakani baada ya kuvuliwa
madaraka yake na askofu mkuu Dk Jacob Chimeledya, kwa sasa katiba
haimtambui kama askofu wa kanisa hilo.
Alisema kabla ya marekebisho ya mwaka 2004, sinodi ya dayosisi ndio
ilikuwa inakuwa na tamko la mwisho dhidi ya askofu wa dayosisi, lakini
baada ya marekebisho kufanyika askofu mkuu ndiye msimamizi wa maaskofu
wote wa dayosisi na ana mamlaka ya kuwastaafisha pale wanapokiuka katiba
ya kanisa.
“Dk Mokiwa amenyang’anywa utawala wa dayosisi ya Dar es Salaam, katiba
inampa mamlaka askofu mkuu kuwastaafisha maaskofu ikibainika wameenda
kinyume cha sheria na katiba ya kanisa,” alisema Chinyong’ole.
Aliongeza kuwa baada ya kumvua utawala wa dayosisi, hatua inayofuata ni
taratibu zingine za kisheria ambazo zitashughulikiwa na kanisa ikiwa ni
pamoja na kumbana Dk Mokiwa kukiuka kiapo chake cha kumtii askofu mkuu
wa kanisa.
Alisisitiza kuwa Dk Mokiwa amevunja kifungu namba 7 cha katiba ya kanisa hilo kuhusu kiapo cha utii kwa askofu mkuu aliposema
“Nakubali na kuahidi kumheshimu na kumtii, kama inipasavyo, askofu mkuu
wa kanisa Anglikana Tanzania... watakaofuata baada yake...”
Katibu mkuu huyo alisema Dk Mokiwa kutokana na hatua yake kugoma
kujiuzulu baada ya kushauriwa na askofu mkuu Tanzania, amevunja kiapo
cha utii kwa katiba ya jimbo kinachosema,
“Ninaahidi pia kwamba nitakubali kujiuzulu au kujitoa kwa hukumu yoyote
itakaoniachisha madaraka na mapato yanayohusika na dayosisi hii
nitakayohukumiwa wakati wowote baada ya uchunguzi wa kutosha wa barza
lenye kbali cha sinodi ya kanisa.”
Pia amevunja kiapo cha utii kwa katiba ya dayosisi kinachosema
“Ninaahidi pia kwamba nijiuzulu wakati wowote kama ikiazimiwa na Askofu
Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania kwa mujibu wa katiba ya kanisa na ya
Dayosisi.”
Wachunguzi wa mambo wanabainisha kuwa kugoma kwa Dk Mokiwa kung’oka
madarakani kutaleta mtafaruku mkubwa ndani kanisa hilo kutokana na
baadhi ya makanisa katika Dayosisi ya Dar es Salaam kuunga mkono uamuzi
wa askofu mkuu na wengine wanamuunga mkono Dk Mokiwa.
Juzi, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Jacob Chimeledya
alimvua uaskofu mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Mokiwa baada ya
mashitaka 10 yaliyofunguliwa na walei 32 wa kanisa hilo katika dayosisi
hiyo kumtuhumu kwa ufisadi wa mali za kanisa hilo.
Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya Askofu Mokiwa kugoma kujiuzulu kama
ilivyoshauri nyumba ya maaskofu ambayo ilimkuta na hatia ya ufujaji wa
mali za kanisa hilo na kukiuka maadili ya kiuchungaji ambayo
yalibainishwa kwenye ripoti ya uchunguzi ya kanis ahilo nchini.
Hata hivyo, Dk Mokiwa amegomea uamuzi huo kwa maelezo kuwa, mwajiri wake
ni Sinodi ya Dar es Salaam ambayo ndio yenye uamuzi wa kumfuta kazi na
si askofu mkuu au askofu mwingine yeyote wa kanisa la Anglikana
Tanzania.
Post a Comment