Maafisa wa UNDP kupitia program ya miradi midogo wakiwa na maafisa wa TNRF na MAIPAC walipotembelea ofisi za Maipac jijini Arusha mapema leo. |
Faustine Ninga afisa program miradi midogo UNDP akizungumza na watendaji wa maipac mapema leo |
Mratibu wa miradi midogo UNDP Faustine Ninga akisisitiza jambo kwa mkurugenzi wa Maipac Mussa Juma alipomtembelea ofisini kwake mapema leo |
Diana Elisa & Beatrice Jonh FJS,Arusha.
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP) kupitia Programu ya miradi midogo(SGP) nchini, limeahidi kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari ya kusaidia jamii za Pembezoni(MAIPAC) katika kutekeleza miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, utunzaji wa mazingira, Misitu na Vyanzo vya maji.
Maafisa wa UNDP kupitia programu ya miradi midogo(SGP), pamoja na maafisa wa Taasisi ya Jumuiko la Maliasili Tanzania(TNRF) leo Julai 25,2023, wametembelea Ofisi ya MAIPAC jijini Arusha, kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi wa uhifadhi wa misitu,Maji na Mazingira kwa maarifa ya asili, uliokuwa unatekelezwa na MAIPAC katika wilaya za Longido, Monduli na Ngorongoro.
Akizungumza watendaji wa MAIPAC, Afisa Programu ya miradi midogo(SGP) wa UNDP Tanzania, Faustine Ninga, amesema wameridhishwa na MAIPAC jinsi ilivyotekeleza mradi huo, ambao ulikuwa unadhaminiwa na mfuko wa mazingira duniani(GEF) na wadau wengine wa maendeleo.
“Tumekuja hapa kuona jinsi ambavyo mmetekeleza mradi wenu, kwa ujumla tunawapongeza sana MAIPAC, mmefanyakazi nzuri kuzifikia jamii za pembezoni na kukusanya maarifa mengi ya asili na baadaye kutoa katika vyombo vya habari na kuandaa vitabu”amesema
Amesema MAIPAC imeweza kufikisha ujumbe maeneo mbalimbali juu ya umuhimu wa maarifa ya asili katika uhifadhi wa mazingira, vyanzo vya maji na misitu lakini pia kushirikiana na taasisi nyingine ikiwepo za serikali kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira.
“Tutaendelea kufanyakazi pamoja,kikubwa muendeleze kutoa elimu kwa maarifa ambayo mmekusanya lakini pia kubainisha fursa nyingine ambazo mnaona tunaweza kushirikiana ili kusaidia jamii”amesema
Mkurugenzi wa MAIPAC Mussa Juma akiagana na Mratibu wa miradi midogo UNDP Faustine Ninga alipotembelea ofisi za MAIPAC mapema leo |
Kaimu Mkurugenzi wa TNRF, Steve Ngowi ambao walikuwa waratibu wa miradi amesema MAIPAC imefanyakazi nzuri ikiwepo kushirikiana vizuri kutoa habari na machapisho za mashirika mengine, ambayo yalikuwa katika progamu ya miradi inayosaidiwa na UNDP.
“Kama walivyosema wenzangu, sisi tumeridhika na utekelezaji wa mradi wenu na tunaimani zikitokea fursa nyingine, mtashiriki vizuri na kuendelea pale ambapo mmeishia”amesema
Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma amesema wanashukuru UNDP kupitia programu ya miradi midogo(SGP) na TNRF kuamua kushirikiana na MAIPAC katika kutekeleza mradi wa uhifadhi wa mazingira,Vyanzo vya maji na Misitu kwa maarifa ya asili.
Juma amesema mradi huo, ambao umetekelezwa kwa mwaka mmoja, umekuwa na manufaa makubwa, kwani jamii imeshirikishwa, halmashauri za wilaya ya Longido, Monduli na Ngorongoro lakini pia serikali kuu.
“Mradi huu umekuwa na manufaa makubwa kwani tulimshirikisha hadi Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira Dk Suleiman Jaffo ambaye alizindua vitabu ambavyo tulichapa juu ya maarifa ya asili na kuahidi kuendelea kushirikiana na MAIPAC na wadau wengine katika uhifadhi wa mazingira”amesema
Juma pia amesema pia wanahabari wameshiriki vyema katika kutangaza, kuandaa vipindi na makala maalum juu ya mradi huo ambao ni mara ya kwanza kutekelezwa nchini.
Mkurugenzi wa MAIPAC Mussa Juma akimkabidhi Stella Zaarh Mratibu Msaidizi Miradi midogo UNDP kitabu cha maarifa ya asili na utunzaji wa Mazingira alipotembelea ofisi za MAIPAC mapema leo. |
Meneja Miradi na Utawala wa MAIPAC, Andrea Ngobole amesema wanaimani wataendelea kushirikiana zaidi na UNDP, TRNF, GEF na serikali ya Ujerumani na wadau wengine katika kutekeleza miradi ya kusaidia jamii, zikiwepo za pembezoni.
Watendaji wa UNDP na kushirikiana TNRF, wapo katika ziara ya kukagua na kufanya tathimini ya utekelezwaji miradi midogo kwa mashirika 13 ambayo yalipatiwa fedha na UNDP kutekeleza miradi midogo nchini.
Post a Comment