PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: BRAZIL YATUMIA BILLION 11 KUWAWEZESHA WAKULIMA WA PAMBA NCHINI TANZANIA
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
  Samweli Nsima Marandu, mkulima wa Pamba katika Kijiji cha Kapanga, Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi ambae amenufaika na mradi wa Cotton ...

 


Samweli Nsima Marandu, mkulima wa Pamba katika Kijiji cha Kapanga, Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi ambae amenufaika na mradi wa Cotton Victoria akielezea mafanikio aliyoyapata

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mkoani Katavi, Onesmo Buswelu, akisaidia kuvuna Pamba kwenye moja ya shamba la mkulima katika Wilaya hiyo.



Na Valentine Oforo, Kigoma


maipacarusha20@gmail.com


SEKTA ya zao la Pamba nchini Tanzania imeanza kupiga hatua kubwa ya mafaniko, ikiwa ni pamoja na ongezeko kubwa katika uzalishaji na tija kwa hekari miongoni mwa wakulima hapa nchini.

Hatua hiyo muhimu katika uzalishaji wa zao hilo la kimkakati la  kibiashara ambalo mpaka sasa limewaajiri wakulima  500,000 katika eneo la takribani ekari 1,000,000 imetokama na utekelezaji wa Mradi wa Cotton Victoria.

Mradi wa Cotton Victoria ulianza kutekelezwa katika baadhi ya mikoa inayozalisha Pamba hapa nchini katika msimu wa uzalishaji wa 2016/2017.

Mradi, unatekelezwa kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Brazil (ABC) kupitia Ubalozi wa Brazil nchini Tanzania kwa bajeti ya Dola za Marekani 5,802,019.08, ambapo nje ya Tanzania, mradi huo pia unatekelezwa katika nchi za Kenya na Burundi.

Mpaka sasa, mradi umefanikiwa kubadilisha maisha ya wakulima wengi katika mikoa ya Tabora, Shinyanga,  Katavi, Geita, Mwanza na mipango inaendelea kuwafikia wakulima katika mikoa mingine inayolima Pamba hapa nchini.

Wakitoa ushuhuda, baadhi ya wakulima walionufaika na mradi huo wameeleza kuwa maisha yao yamebadilika kwa kiasi kikubwa.

"Kabla ya mradi kutufikia, nilikuwa navuna kilo 300 za Pamba kwa ekari, lakini baada ya kufikiwa na mradi na kufundishwa njia bora za upandaji na utunzaji wa Pamba shambani kwa sasa navuna kilo 860 kwa ekari, na ninatarajia kuvuna kilo 1000 msimu ujao," Samweli Nsima Marandu, mkulima wa Pamba katika Kijiji cha Kapanga, Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi anaeleza.

Marandu, ambae kutokana na mafanikio hayo ameweza kujenga nyumba ya kisasa ambayo hakutarajia kuimiliki katika maisha yake anasema pamoja na mambo mengine, mafanikio hayo yamepatikana baada ya mradi kumfundisha njia ya kisasa ya upandaji wa Pamba kwa nafasi mpya ya sentimita 60 mstari hadi mstari na sentimita 30 shimo hadi shimo ambapo idadi ya mimea inakua 44,444 kwa ekari ukilinganisha na mimea 22,222 kwa ekari kwa upandaji wa awali wa sentimita 90 kwa 40 aliokuwa akiutumia.

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mkoani Katavi, Onesmo Buswelu, kwa upande wake anasema tangu kuanza kwa mradi wakulima katika Wilaya hiyo wamenufaika kwa kiasi kikubwa, hali ambayo pia imechangia kuongeza kwa pato la Wilaya kupitia biashara ya Pamba.

Kwa Tanzania, mradi unatekelezwa kupitia kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Ukiriguru kilichopo Jijini Mwanza, kituo ambacho kina jukumu la kuratibu kitaifa shughuli za utafiti wa pamba na mazao ya mizizi (mihogo na viazi vitamu).

Dkt Paul Saidia, ni Mkurugenzi wa Kituo hicho cha TARI Ukiriguru na anaeleza kuwa utekelezaji wa mradi umeleta mwanga mpya wa matumaini, siyo tu kwa wakulima, lakini pia kwa sekta nzima ya Pamba nchini Tanzania. 

"Tunaishukuru Serikali ya Brazil kugharamia mradi huu unaojikita katika kuendeleza zao la Pamba hapa nchini," 

Dkt. Saidia anaeleza kuwa mradi umenunua vifaa mbalimbali vya kisasa vya kulima Pamba, ikiwemo Matractor makubwa na madogo Power Tillers, majembe mbalimbali, vifaa vya maabara, vifaa vya kuchakata na kuongeza thamani ya Pamba, vifaa vya maandalizi na kupandia Pamba, vifaa vya kutunza mbegu, vifaa vya kupambana na visumbufu, vifaa vya karakana, pamoja na vitendea kazi ofisini. 

Aidha, kutokana na mafanikio makubwa yaliyotokana na mradi huo, Serikali Mkoani Tabora imeazimia kutekeleza mkakati maalumu wa kuhakikisha wakulima wengi zaidi wanajikita katika uzalishaji wa zao la Pamba. 

Nganga Luhemeja, miongoni mwa wakulima wa Pamba waliofanikiwa katika mkoa wa Tabora

Afisa Kilimo wa Mkoa wa Tabora, Saidi Babu, anasema Pamba inalimwa na kustawi kwa wingi katika Wilaya sita Mkoani humo, ikiwemo Wilaya za Igunga, Nzega, Uyui, Tabora Manispaa, Urambo na Wilaya ya Kaliuwa.

"Tangu mradi wa Cotton Victoria kuanza kutekezwa hapa, tumeshuhudia wakulima wa Pamba wakipata mavuno mengi, tofauti kabisa na zamani, na hata maisha yao yamebadilika sana kiuchumi, " anashuhudia.

Kutokana na mafanikio hayo, anasema wameona ipo haja ya kuwashawishi wakulima wengi zaidi kuanza kulima Pamba ili kuongeza vipato vyao, na kuongeza uchumi wa Mkoa kwa ujumla.

"Kwa mfano, Tabora inasifika sana kwa uzalishaji wa zao la Tumbaku, lakini kwa sasa uzalishaji wa Tumbaku unakabiliwa na changamoto nyingi za mabadiliko ya tabianchi,  hivyo tija imeshuka na tunaona ipo haja wakulima kuanza kuwekeza nguvu zao kwenye Pamba," Babu alifafanua.

Zao la Pamba likiwa shambani kabla ya kuvunwa

Nganga Luhemeja ni miongoni mwa wakulima wa Pamba waliofanikiwa sana katika mkoa wa Tabora. 

"Kupitia mradi huu nimeweza kuongeza uzalishaji kutoka kilo 200 kwa ekari  hadi kufikia kilo 510, na ninatazamia uzalishaji kuongezeka zaidi msimu ujao," anaeleza.

Balozi wa Brazil nchini Tanzania,  Gustavo Martins Nogueira, anasema Brazil wanafurahi kuona utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati wanaoufadili umeweza kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya Pamba nchini Tanzania. 

"Kutokana na utekelezaji mzuri wa mradi tutaendelea kuipatia Tanzania vifaa vya kisasa na fedha za kutosha ili kuhakikisha nchi inapata matokeo mazuri zaidi katika uzalishaji wa Pamba," alisisitiza. 

Dkt. Furaha Mrosso ni Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu kutoka TARI Makao Makuu.

Kwa upande wake anaeleza: " TARI tumejipanga vyema kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa kuakisi thamani halisi ya fedha zilizotolewa na wafadhili, lakini pia, wakulima lazima wanufaike kikamifu kwa kujifunza mbinu bora ili kuendea kuongeza uzishaji na tija," alieleza. 

Wadau wengine wanahusika katika utekelezaji wa mradi wa Cotton Victoria ni pamoja na Wizara ya Kilimo ya Tanzania,  Taasisi ya Pamba ya Brazil (IBA), pamoja na Chuo Kikuu cha Shirikisho cha Lavras (UFLA).

Pamba ni miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini Tanzania, zao la kibiashara ambalo linalimwa katika Mikoa 17, Wilaya 56 likiwajumuisha wakulima wapatao 500,000 katika eneo la takribani ekari 1,000,000.

Mnyororo wa thamani wa zao la Pamba unategemewa na zaidi ya asilimia arobaini (40%) ya Watanzania wote. 

Mpaka sasa, takribani asilimia 70 (70%) ya Pamba inauzwa nje ya nchi na kuingiza mapato ya wastani wa Dola milioni 120 za Kimarekeni kwa mwaka.

Hali ya uzalishaji wa zao la Pamba nchini ni kati ya tani 122,000 hadi 370,000 kutegemea na hali ya hewa. 

Uzalishaji wa zao la Pamba huathiriwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa, kupungua kwa rutuba ya udongo, visumbufu kama wadudu na magonjwa, kutozingatia kanuni za kilimo bora cha pamba.

Tafiti mbalimbali zimefanyika, na zinaendelea kufanyika ili kuchangia kuongeza tija katika zao la pamba ambazo ni pamoja na ugunduzi wa mbegu bora, kanuni za kilimo bora cha pamba, pamoja na udhibiti wa visumbufu.

Mafanikio haya ya utafiti yanatokana na ushirikiano kati ya TARI na Bodi ya Pamba Tanzania (TCB).

Baadhi ya wakulima wakiwa tayari kukuza Pamba zao katika maghala

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top