Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, akijibu maswali Bungeni, Jijini Dodoma |
Serikali
imeeleza kuwa Uchukuaji wa baadhi ya vyanzo vya mapato katika halmashauri ulifanyika
kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti iliyoridhiwa na Bunge ya mwaka 2015 kifungu
namba 58 ikiwa na lengo la kuongeza ufanisi wa ukusanyaji na matumizi ya mapato
hayo.
Hayo
yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Viti
Maalum Mhe. Suzana Mgonukulima, aliyependekeza itungwe sheria ya kuibana
serikali ikiwa haitarejesha fedha zilizotokana na vyanzo vya mapato vilivyopo
kwenye Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji zitakazokusanywa na kuwekwa kwenye
Mfuko Mkuu wa Serikali.
Akijibu
swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa kwa
mujibu wa kifungu cha 44 cha Sheria ya Bajeti, mgao wa fedha kutoka katika
Mfuko Mkuu wa Serikali utazingatia
bajeti iliyoidhinishwa, upatikanaji na mtiririko wa fedha, utekelezaji
mpango wa ununuzi na mpango wa kuajiri hivyo hakuna Fungu litakaloruhusiwa
kufanya matumizi ya aina yoyote mpaka kuwe na fedha za kulipa matumizi husika.
“Usimamizi
wa Mapato hayo kwa mujibu ya Sheria ya
Bajeti ya Mwaka 2015 Kifungu namba 58 unazingatia
mapato kuingizwa kwenye Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Fedha za Serikali, aliyepewa
mamlaka ya kukusanya mapato ya Serikali atawajibika katika ukusanyaji wenye
ufanisi, utunzaji wa hesabu, utoaji wa taarifa na kuzuia ufujaji wa mapato”, alisema
Dkt. Kijaji.
Alisema
Usimamizi wa mapato na matumizi umebainishwa vizuri na hivyo hakuna haja ya
kutunga sheria nyingine ya kuibana Serikali ikiwa haitapeleka fedha kwenye,
Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji.
Aidha
akijibu swali la nyongezai la Mhe. Mgonukulima kuhusu kutokuwa na usawa katika utoaji wa
fedha za maendeleo katika Wilaya, Dkt. Kijaji alisema kuwa tarehe 5 Mei, 2018
Serikali ilizindua Mkakati wa kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa
kutekeleza miradi yenye kuchochea upatikanaji wa Mapato ili ziweze
kujitegemea hivyo ni vema Halmashauri
zikabuni miradi ya maendeleo itakayoongeza mapato.
Akieleza
kuhusu utaratibu wa malipo ya Kodi ya Majengo kutoka katika Halmashauri nchini
Naibu Waziri Dkt. Kijaji, alisema kuwa Majengo yasiyofanyiwa tathimini yanatakiwa
kutozwa kiwango sawa cha Sh. 10,000 na majengo ya juu (ghorofa) yanatakiwa kutozwa
kiwango sawa cha Sh. 50,000.
Alisema
majengo yaliyofanyiwa tahimini ndiyo yanayoweza kulipiwa kodi zaidi ya kiasi
hicho, hivyo wakurugenzi wa Halmashauri wanapaswa kuzingatia utaratibu huo
uliowekwa katika ukusanyaji wa kodi hiyo, alieleza Dkt. Kijaji.
Imetolewa na;
Benny
Mwaipaja
Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara
ya Fedha na Mipango
Post a Comment