Mama mzazi wa Andrew ,Janeth Chacha akimfanyia usafi wa mfuko ambao hutumika kutolea na kuhifadhi haja ndogo kwa mtoto wake |
Andrew Jacob akiwa na wazazi wake Jacob Rohole na mama yake Janeth Chacha nyumbani kwao mtaa wa Nyamatare,Musoma mjini |
Mtoto AndrewJacob akiwa na mfuko maalumu kwaajili ya kutolea haja ndogo |
'HERI KUFA KULIKO KUISHI'
*Ni kauli ya mtoto Andrew Jacob
*Anaiyeishi na mpira wa kutolea haja ndogo
*Ni baada ya kuangukiwa na ukuta
*Njia ya mkojo yapishana,aomba msaada wa matibabu
"HERI kufa kuliko kuishi,napata maumivu makali sana,muwasho usiokoma sehemu za siri jambo ambalo linanifanya nikose raha"
" Maisha yangu yamekuwa tia maji tia maji leo mzima
kesho mgonjwa...hospitali imekuwa nyumbani kwangu hali hii siipendi
basi tu sina namna ninaomba wasamaria wema wanisaidie kuokoa maisha
yangu bado safari ni ndefu ya kuweza kutimiza ndoto zangu kimaisha"
Haya ni maneno yaliyojaa kigugumizi na maumivu makali
kutoka kwenye kinywa cha mtoto Andrew Jacob(7) mwanafunzi wa darasa la
kwanza katika shule ya Msingi Nyamatare iliyopo Musoma Mjini mkoani
Mara wakati wa mahojiano na mwandishi wa Makala haya.
Akielezea masahibu yaliyompata hadi kufikia hatua ya kuomba
msaada kwa wasamaria wema,Mtoto Andrew anasema Ana kumbuka ilikuwa
jioni ya Desemba 13,2016 ambapo alikuwa akicheza mchezo maarufu kwa jina
la kombolela na wenzake aliangukiwa na ukuta wa nyumbani kwao
ulimsababishia kuvunjika kiuno,mguu wa kushoto na njia ya mkojo
kupishana.
Mtoto Andrew anasema kuwa wakati ajali hiyo ya kuangukiwa
na ukuta ikitokea wazazi wake ambao ni wajasiriamali wa kuuza matunda
hawa kuwepo nyumbani hivyo msaada wa kwanza aliupata kutoka kwa majirani
ambao walimtoa kwenye ukuta uliomwangukia na kisha kuwapigia simu
wazazi ambao ni Jacob Rohole na Janeth Chacha.
Andrew anasema wakati huo wote alikuwa hajitambui kutokana
na kupoteza fahamu na wazazi wake walipofika nyumbani walimchukua na
kumkimbiza katika hospitali ya mkoa ambako alipatiwa matibabu ya awali
na siku iliyofuatia alihamishiwa Hospitali ya Bugando iliyopo mkoa
Mwanza.
Baada ya kuwasili Bugando alipolewa vizuri na kuanza
matibabu ambapo siku chache baadaye alifanyiwa upasuaji wa njia ya
mkojo...hapa Andrew anashindwa kuendelea kuzungumza kutokana na
kigugumizi na maumivu makali hivyo kunikazimu kuendelea na mazungumzo na
baba mzazi Rohole.
Baba huyo wa mtoto Andrew anaeleza kuwa baada ya upasuaji
wa njia ya mkojo bado hali haikuwa ya kuridhisha sana kwani mtoto wake
hakuweza kujisaidia kama awali badala yake alilazimika kutumia mpira
maalumu ambao ulikuwa ukimsababishia maumivu makali.
Anasema hali hiyo ilidumu kwa miezi mitatu waliyolazwa
hoapitalini hapo na ndipo Daktari aliyekuwa akimuhudumia ( jina
linahifadhiwa) alipowapa rufaa ya kwenda hospitali ya KCMC iliyopo
Moshi mkoani Kilimanjaro kwa matibabu zaidi Machi 2017.
Hata hivyo baba huyo wa mtoto anaeleza kuwa kutokana na
ukata uliokuwa ukimkabili ilimlazimu kurejea nyumbani Musoma kwaajili
ya kujipanga kutafuta fedha kwaajili ya safari ya matibabu ya kuelekea
KCMC Moshi.
Baada ya miezi kadhaa ndipo alipo kwenda KCMC na kuandikiwa
kipimo cha X- ray ambacho kwa wakati huo kilikuwa na hitilafu hivyo
kulazimika kwenda Arusha ambako nako alikutana na tatizo hilo hilo
katika hospitali alizokwenda ikiwemo Mount Meru ambayo ni ya mkoa.
Rohole anabainisha kuwa alizunguka sana na mtoto Andrew
hadi walipofanikiwa kufanyiwa kipimo hicho katika kituo cha X- ray
Center jijini Arusha na kurudi KCMC huku wakiwa hoi kwa uchovu.
Wangali wakiwa katika hali hiyo ya uchovu na maumivu makali
kwa mtoto Andrew walifanikiwa kuonana na daktari ambaye baada ya
kusoma picha za vipimo vya X- ray aliweka bayana kwamba tatizo la mtoto
huyo ni vigumu kutibika kwani hakukuwa na wataalamu hivyo warudi
Musoma hadi Agosti 2017 ambako KCMC ingekuwa na wataalamu kutoka nje
ya nchi ambao wangeweza kumtibu kijana wake.
" Sikuamini nilichokisikia,nilinyong'ea lakini sikuwa na
namna nyingine zaidi ya kurudi nyumbani na hilo ndilo linalonisukuma
kuomba msaada kwaajili ya mtoto wangu aweze kwenda kutibiwa nje ya nchi
"anasisitiza Rohole
Hata hivyo Rohole anaeleza kuwa mara baada ya kurudi Musoma
bado hali ya Andrew haikuwa ya kuridhisha na hata mahudhurio ya shule
hayakuwa mazuri kwani siku zingine huamka akiwa mgonjwa sana na
kulazimika kumkimbiza hospitali.
Ndipo kama familia wakafikia maamuzi ya kwenda kwa Mkuu wa
Wilaya ya Musoma mjini Dk Vincent Anney kumweleza juu ya tatizo la
mtoto wao na hali duni ya kimaisha waliyo nayo hivyo kupatiwa kibali
cha kuchangiasha fedha kwaajili ya matibabu ya mtoto Andrew.
" Pamoja na kwamba tuna kibali cha kuchangisha fedha
kwaajili ya mtoto Andrew lakini mwitikio ni mdogo sana na hali yake
kiafya nazidi kuzorota siku hadi siku " anaeleza Rohole kwa masikitiko
makubwa
Pamoja na mambo mengine Rohole anasisitiza kuwa kipato
chake ni duni kwani hukosa hata sh 50,000 kwa mwezi kwaajili ya kununua
vifaa vya kumsaidia Andrew kupata haja mdogo hivyo kumlazimu mama wa
mtoto huyo kufua vya zamani jambo ambalo si salama na ni hatari kiafya.
Naye mama mzazi wa mtoto Andrew, Janeth anasema tangu
mtoto wake apate ajali hiyo ya kuangukiwa na ukuta familia imeyumba
sana kimapato hivyo anaomba msaada kwa wasamaria wema wa kupatiwa fedha
na hospitali nchini India kwaajili ya matibabu ya haraka ya kijana
wake huku akimtaja rais John Magufuli na kumwomba aitazame familia hiyo
kwa jicho la tatu kwani siku za hivi karibuni amejitoa sana katika
kusaidia wagonjwa.
Kauli ya anyosoma Andrew
Kwa upande wake Mwalimu wa darasa wa mtoto Andrew,Dainess
Mwingi anakiri kwamba licha ya tatizo alilo nalo mtoto huyo lakini Ana
uwezo mkubwa sana kiakili ikilinganishwa na watoto wengine darasani.
Anasema wakati mwingine hata kama anaumwa hutoroka
nyumbani na kwenda shule hivyo hulazimika kumrudisha nyumbani ili apate
muda wa kupumzika na kutazama afya yake kwanza.
" Mtoto Andrew anahitaji msaada wa haraka kwaajili ya
matibabu ili aweze kurejea katika hali yake si jambo jema tena mwakani
akirudia darasa kama ilivyotokea mwaka jana ambapo alishindwa
kuhudhuria masomo mwaka mzima " anasisitiza Mwl wa mtoto Andrew
Andrew amezaliwa kwenye familia ya kawaida yenye watoto watano huku yeye akiwa ni mtoto wa nne kuzaliwa.
Ni familia inayoishi kwenye nyumba ambayo hata ujenzi wake haujakamilika kutokana na hali ngumu ya ukata .
Wazazi wa mtoto huyo ni wajasiriamali wadogo wa kuuza
matunda ambao hivi sasa ukata umeigubika familia hiyo kiasi cha
kushindwa kujikimu kimaisha tangu Andrew alipopata ajali
iliyomsababishia hali aliyo nayo hivi sasa.
Hivi sasa ni familia inayojiendesha kwa biashara ya mali
kauli katika matunda ambayo Wazazi hao wamejikita na hivi karibuni
walijikuta wakiingia katika madeni ya zaidi ya mil 2 baada ya kutapeliwa
na watu waliodai kutaka kuwasaidia ili waweke pesa kwenye akaunti ya
mtoto Andrew aweze kupata matibabu haraka.
Kifupi ni familia inayohitaji msaada wa haraka ili mtoto
Andrew aweze kutibiwa nchini India na kupona ili wazazi wake warejee
katika shughuli za uwajibikaji na kutunza familia ipasavyo.
Post a Comment