Na.
MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Ajira na Watu
wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa kufufuliwa kwa kiwanda sambamba
na shamba la Miwa la Mbigiri itasaidia kuondoa uhaba wa sukari nchini kwa
kuzingatia uwepo wa kiwanda hicho na shamba la miwa Mbigiri.
Ameyasema hayo mapema
mwishoni mwa wiki hii walipokuwa katika ziara na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Katiba na Sheria kujionea namna uboreshaji wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na
Jeshi la Magereza unavyoendelea.
Alieleza kuwa, Tayari
hekari 300 zimeshapandwa miwa kati ya Hekari 1200 na hekari 700 zimeshalimwa
ambapo hii itasaidia sana kuongeza uzalishaji wa sukari nchini tofauti na ilivyo
sasa na kuwaomba Watanzania kuunga mkono jitihada za Mifuko ya Hifadhi ya PPF
na NSSF ambao wamechangia asilimia hamsini kwa hamsini katika kuhakikisha
kiwanda na shamba vinafikia malengo ya kuzalisha sukari kwa wingi nchini.
“Ninaipongeza Mifuko
ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF kwa kuona umuhimu wa kukiboresha kiwanda
hiki ili kukidhi hitaji la nchi katika kutatua changamoto ya sukari nchini ambapo
matarajio ni kuvuna miwa tani 500,000 na uzalishaji wa sukari utakuwa Tani
30,000”Alisisitiza Mhagama
Sambamba na
hilo, Waziri Mhagama alifafanua kuwa
uwepo wa viwanda hivi ni moja ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Miaka mitano
unaoelekeza kuwa na uchumi wa viwanda.
“Kiwanda hiki
kikianza kufanya kazi kitakuwa kimekidhi matakwa ya Mpango wa Maendeleo ya
Taifa ya miaka Mitano ambao unaeleza uchumi wetu wa viwanda uwe uchumi utakaotumia
malighafi zinazozalishwa hapa nchini na bidhaa zitakazo zalishwa ziwanufaishe
Watanzania”Alisema Mhagama
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa alieleza kuwa Kiwanda
hiki kikimalizika kitasaidia kuongeza uzalishaji wa sukari nchini na kupata
masoko mpaka nchi za nje.
“Jambo hili
likifanikiwa litaweza kutatua changamoto ya sukari hapa nchini basi sisi kama
Kamati na kwa niaba ya wajumbe wenzangu tunaipongeza sana Serikali kwa hatua
kubwa iliyofanya na hii itasaidia pia kujikwamua kiuchumi sisi kama Nchi ”
alisisitiza Mtengerwa
Aidha Mkurugenzi Mkuu
Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Prof. Godius Kahyarara alieleza
kuwa lengo jingine la kukifufua kiwanda hicho ni pamoja na kukuza uchumi wananchi
kwa kuuza sukari ndani na nje ya nchi.
“Tunatarajia kupata
soko la ndani na nje hususani kuuza ukanda wa Afrika ya Kati hivyo sukari
itakayozalishwa lazima iwe ya viwangi vya juu na mfano mzuri ni nchi ya Congo
ambao wanazalisha tani elfu 70 ingawa hitaji lao kwa mwaka ni tani laki moja
hii ni picha halisi la uwepo wa siko la sukari barani Afrika” Alieleza Prof.Kahyarara
Naye, Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro Mhe. Stephen Kebwe alipongeza juhudi za Serikali kufufua kiwanda hicho
cha Mbigiri na shamba la miwa ambapo vitaleta tija kwa jamii kwa ujumla na
kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge kuona umuhimu wa kutembelea Kiwanda hicho
na Shamba la Miwa.
Post a Comment