Na Ferdinand
Shayo,Hanang
Wagombea wa Nafasi za Ubunge na Udiwani katika Wilaya ya
Hanang iliyoko mkoa wa Manyara wamedai kutokua na imani na Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Hanang , Felix Mabula ambaye ni Msimamizi mkuu wa uchaguzi
katika jimbo hilo kwa madai kuwa Mkurugenzi huyo alikumbwa na tuhuma nyingi za
matumizi mabaya ya fedha kwenye miradi ya maji na kuboresha miundombinu ya
shule za msingi tuhuma ambazo ziliibuliwa na madiwani wa CHADEMA ambao ni wagombea kwa sasa jambo linalowapa
wasiwasi kuwa haki haitatendeka katika uchaguzi.
Mgombea Ubunge katika jimbo la Hanang Derick Magoma alisema
hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ,amesema kuwa tayari wameandikia
barua tume ya Uchaguzi yenye kumbukumbu namba CDM/HAN/UT/2/239 juu ya kutokua na imani na msimamizi wa
Uchaguzi wa jimbo hilo barua waliyoiwasilisha septemba 2 mwaka huu wakiitaka
tume iteue Msimamizi mwingine.
Magoma alisema kuwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha
zilijadiliwa katika Baraza la Madiwani zikiongozwa na madiwani wa CHADEMA ambao
ni Ndugu Peter Lori Diwani wa Kata ya Katesh,John Farayo Diwani kata ya
Endasiwold ,Masala Bajuta wa kata ya Gisambalang na wengine wengi.
“Madiwani hao waliomtuhumu Mabula ndio wagombea
na hao hao Mabula atasimamia uchaguzi wao ,tunaona
kabisa kuwa haki haiwezi kutendeka ,na hata kama ikitendeka hatutaamini kama
imetendeka” Alisema Magoma
Mgombea huyo alisema kuwa Mabula anakabiliwa na tuhuma za
kutumia vibaya shilingi bilioni 1 na milioni 100 ambazo zimepotea na
zingetumika kujenga vituo vya afya ,kuleta madawa na kusambaza huduma ya maji
safi ambayo ni changamoto kubwa kwa jimbo hilo.
Mgombea udiwani kata ya Endasiwold John Farayo alisema kuwa
wao kama wagombea hawana imani na Mkurugenzi huyo hivyo wameitaka tume ya
uchaguzi ichukue hatua za haraka kumteua msimamizi mwingine wa uchaguzi ili
uchaguzi uwe huru na wa haki.
Mwenyekiti wa Chadema Hanan`g Isack Joseph alisema kuwa chama hicho
kimesimamisha wagombea udiwani 31 kati
ya kata 33 na kufafanua kuwa kutokana na rekodi ya Mkurugenzi huyo wanahitaji
msimamizi mwingine wa uchaguzi ambaye watakua na imani naye.
Post a Comment