Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akizungumza na Viongozi na watumishi
wengine wa Wakala wa Ununuzi na Ugavi Serikalini (GPSA) Mkoa wa Kagera
(hawapo pichani) alipotembelea ofisi hizo kuhusu kuhakikisha Taasisi
zote za Serikali zinapata huduma kutoka Wakala huo, alipofanya ziara
katika Mkoa huo.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akitoa maagizo kwa Kaimu Meneja wa Wakala
Ununuzi na Ugavi Serikalini (GPSA) Mkoa wa Kagera, Bi. Dorothea Bugenyi,
kuhusu kuwahudumia Taasisi zote za Serikali kwa kuwa ndio wajibu wa
Wakala huo, alipofanya Ziara katika Ofisi hizo za Mkoani Kagera.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera
ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Bw. Deodatus Kinawiro akielezea
namna atakavyoshirikiana na Wakala wa Ununuzi na Ugavi Serikalini katika
Mkoa huo ili kuhakikisha kunakuwa na matumizi adili ya fedha za
Serikali, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji
alipotembelea Ofisi za Wakala huo Mkoani Kagera.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Ununuzi
na Ugavi Serikalini (GPSA) Mkoa wa Kagera, Bi. Dorothea Bugenyi (kulia)
akimuonesha Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji
(kushoto) namna tetemeko la ardhi lilivyo haribu miundombinu ya Ofisi
hizo, alipotembelewa na Naibu Waziri huyo katika Ofisi za GPSA Mkoani
humo.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera
ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Bw. Deodatus Kinawiro (kulia)
akizungumza jambo wakati Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji (kushoto) alipotembelea Ghala la Wakala wa Ununuzi na
Ugavi Serikalini (GPSA) Mkoani Kagera.
Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (wa pili kulia) akitembelea maeneo ya
Ofisi za Wakala wa Ununuzi na Ugavi Serikalini (GPSA) ambapo aliweza
kupata maelezo namna Wakala huo unavyofanya kazi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa nne kushoto), Kaimu Mkuu wa Mkoa wa
Kagera ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Bw. Deodatus Kinawiro (wa
tano kulia), Kaimu Meneja wa Wakala wa Ununuzi na Ugavi Serikalini
(GPSA) Mkoa wa Kagera, Bi. Dorothea Bugenyi (wa tatu kushoto) na
watumishi wengine wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa
ziara ya Naibu Waziri huyo katika Ofisi hizo Mkoani Kagera.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
…………………………………………………………………..
Benny Mwaipaja, Kagera
NAIBU waziri wa Fedha na Mipango,
Dkt. Ashatu Kijaji, ameziagiza Mamlaka na Taasisi zote za Umma kufanya
ununuzi wa vifaa na mafuta kupitia Wakala wa Serikali wa ununuzi na
ugavi (GPSA) kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge na kuwaonya
wahusika wote watakaoendelea kukaidi maagizo hayo kwamba watachukuliwa
hatua za kisheria.
Dkt. Kijaji ametoa maagizo hayo
mkoani Kagera baada ya kutembelea na kukagua shughuli zinazofanywa na
Wakala wa Ununuzi na Ugavi GPSA mkoani humo na kubaini kuwa taasii na
idara nyingi za umma zinafanya manunuzi nje ya mfumo wa GPSA jambo
ambalo amesema ni ukiukwaji mkubwa wa sheria.
Alisema kuwa lengo la Serikali la
kuanzishwa kwa wakala huo pamoja na mambo mengine ilikuwa kudhibiti
matumizi ya Serikali na kuonya kuwa Serikali haitakubali kuona sheria
zinakiukwa kwa makusudi na kwa malengo yanayoonesha kuna nia isiyo njema
katika matumizi ya fedha za umma.
“Hili si ombi ni maelekezo na ni
agizo, taasisi zote zipate huduma kutoka kwa wakala wetu (GPSA) kwani
Serikali ilikuwa na dhamira ya uwepo wa matumizi sahihi ya fedha za
matumizi wanazopelekewa na ndiyo maana ukaanzishwa Wakala huu” Alisema
Dkt. Kijaji
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba,
Deodatus Kinawiro, akizungumza kwaniaba ya Mkuu wa mkoa wa Kagera,
aliiagiza Wakala wa Ununuzi na Ugavi (GPSA) mkoani humo kumpelekea
orodha ya taasisi ambazo hazitumii huduma za wakala huo ili aweze
kuchukua hatua.
Alisema kuwa ni jambo lisilofaa
kwa Taasisi za Umma kukiuka sheria na kwamba watatekeleza maelezo
yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango haraka ili kuokoa fedha
za Serikali na kuweka uwajibikaji.
Awali, Kaimu Mkuu wa Wakala wa
Ununuzi na Ugavi GPSA mkoa wa Kagera Bi. Dorothea Bugenyi alieleza kuwa
katika kipindi cha miaka 3 iliyopita Wakala huo umeongeza makusanyo
yatokanayo na mauzo ya vifaa na mafuta kutoka Shilingi bilioni 1.9 hadi
kufikia Shilingi bilioni 2.34.
Alisema kuwa mapato hayo
yangekuwa makubwa zaidi endapo taasisi zote za umma zingetii sheria na
kufanya manunuzi yao ya vifaa na mafuta kutoka kwa Wakala huo na kuiomba
Serikali kuusaidia Wakala huo kuziagiza taasisi zake za umma kutekeleza
sheria hiyo kwa vitendo.
Post a Comment