Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwonya na kumwambia Mbunge wa Kawe,
Halima Mdee (Chadema), kwamba kadi za onyo kwa ajili yake zimeisha
kutokana na kushindwa kuhudhuria mahakamani siku ya kesi.
Kauli hiyo ilitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi
baada ya kubaini kwamba ilitolewa hati ya kumkamata mbunge huyo kwa
kushindwa kufika mahakamani.
Halima Mdee alipotakiwa kujitetea aliinuka na kujieleza kuwa amefika
mahakamani hapo akiwa na nyaraka za safari ikiwamo tiketi na VISA na
kwamba taarifa za safari alimpa wakili.
Kwa upande wa wakili wao, Hekima Mwesiga aliieleza mahakama kuwa nyaraka
za kuiarifu mahakama juu ya safari ya Halima Mdee nje ya nchi kwa
bahati mbaya hakuziwasilisha, alikuwa nazo Peter Kibatala ambaye alikuwa
akiendesha kesi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
“Tutaonana wabaya katika hili ni lazima unapofanya kitu adabu yake
ifuatwe, Wakili hakufuata taratibu na Halima kabla ya kusafiri ulipaswa
kutoa taarifa mahakamani ili uweze kupata ruhusa ya mahakama lakini
haukufanya hivyo.
“Sasa nafikiri wote tufuate taratibu za kuhudhuria mahakamani, Halima
Mdee kadi zako za kukuonya zimeisha tafadhali,”alisema Hakimu.
Mdee na wabunge wengine wa Chadema, Mwita Waitara, Saed Kubenea na
makada wao wanatuhumiwa kumjeruhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Theresa Mmbando.
Kabla ya onyo hilo, mahakama ilisikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka
uliotolewa na Mrakibu wa Polisi, ambaye pia ni Msaidizi wa Operesheni
Ilala, Eugen Mwampondele.
Mwampondele alidai siku ya tukio alimwona Rafii Juma na Halima Mdee wakimkunja Theresa Mmbando ili awape nyaraka.
Shahidi huyo alidai waliompiga Mmbando hawapo mahakamani. Washtakiwa
katika kesi hiyo ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea, Diwani wa
Kata ya Kimanga, Manase Njema (56), Halima Mdee (37) na Mbunge wa
Ukonga, Mwita Waitara (40).
Wengine ni mfanyabiashara na kada wa chama hicho, Rafii Juma (21)pamoja na Diwani wa Kata ya Saranga, Ephreim Kinyafu (33).
Inadiwa kuwa Februari 27, 2016 katika Ukumbi wa Karimjee Wilaya ya Ilala
jijini Dar es Salaam watu hao walimjeruhi Theresia na kumsababishia
majeraha mwilini wakati wa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.
Post a Comment