PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: Rais Magufuli Awapasukia ya Moyoni Viongozi wa Afrika,Ataka Wayafuate ..!!!
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
JENGO la Amani na Usalama lililopo Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, limetangazwa rasmi ...



JENGO la Amani na Usalama lililopo Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, limetangazwa rasmi kuwa litaitwa Mwalimu Julius Nyerere.

Jengo hilo limepewa jina hilo rasmi katika hafla ya chakula cha mchana, iliyofanyika jana na kuhudhuriwa na Rais John Magufuli pamoja na marais mbalimbali wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, mawaziri na mabalozi mbalimbali wanaohudhuria Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika unaoendelea mjini humo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli aliwashukuru viongozi wote wa AU kwa kuamua jengo hilo liitwe jina la Mwalimu Julius Nyerere ikiwa ni kutambua mchango wake katika kupigania amani na usalama na alibainisha kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa Mwafrika halisi na kiongozi mahiri na shupavu.

“Na kwa hakika naweza kusema kuwa alikuwa mmoja wa viongozi bora kabisa ambaye amewahi kutokea katika Bara letu, katika maisha yake yote Mwalimu Nyerere alipambana ili kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Afrika, alikuwa mmoja wa waanzilishi wa umoja huu, sisi Watanzania kwa hakika tunajivunia sana Mwalimu Nyerere kuwa Baba wa Taifa,” alisema Dk Magufuli.

Dk Magufuli aliongeza kuwa Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa katika kupambana na ubaguzi na unyonyaji wa kila aina, alisaidia ukombozi wa nchi nyingi za Afrika, na hata alipong’atuka katika hatamu za uongozi wa Taifa la Tanzania aliendelea kutoa mchango wake kupigania amani katika nchi za Afrika.

“Wito wangu kwenu, waheshimiwa viongozi ni kwamba, sambamba na kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa jengo hili, itakuwa ni jambo jema zaidi kama tutajitahidi kufuata nyayo zake pamoja na kuishi maisha ya viongozi wengine hodari wa Bara hili wakiwemo Kwame Nkrumah, Ahmed Ben Bella, Sekou Toure, Gamal Abdel Nasser na bila kusahau shujaa wetu mwingine Nelson Mandela,” alisisitiza Rais Magufuli.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top