Jitihada za kuwatafuta wachimbaji wadogo 14 wa mgodi wa dhahabu wa RZ
uliopo Nyarugusu mkoani Geita waliofukiwa na kifusi baada ya udongo
kuporomoka mpaka usiku zilikuwa zikiendelea.
Wachimbaji hao wamefukiwa kwenye shimo lenye urefu wa mita 38 walimokuwa wanachimba dhahabu .
Tukio la kuporomoka kwa shimo hilo lilitokea saa tisa usiku wa kuamkia
jana na wachimbaji 13 raia wa Tanzania na mmoja mwenye asili ya China
walikuwa ndani.
Akielezea tukio hilo, msemaji wa kampuni ya RZ, Francis Kiganga alisema
shimo lililofukiwa na udongo licha ya kuwa na urefu wa mita 38 kwenda
chini, pembeni lina njia yenye urefu wa mita nyingine 38.
Alisema sababu za udongo kuporomoka na kuziba njia ni eneo hilo kuwa na
mashimo mengine yaliyochimbwa na wakoloni miaka ya 60 iliyopita na
kusababisha udongo kutitia.
Mmoja wa wachimbaji aliyeshuhudia tukio hilo, Lucas Misalaba alisema
saa nane usiku waliona shimo likititia ndipo walitoa taarifa kwa wenzao
walioko chini kusogea na kukaa pembeni na baada ya muda kidogo shimo
lote lilifukiwa na udongo.
Akizungumza baada ya kutembelea eneo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Geita,
Ezekiel Kyunga alisema yapo matumaini kwamba wachimbaji hao watakuwa hai
na kuitaka idara ya madini mkoa kuongeza nguvu za uokoaji ili
kuwanusuru wachimbaji hao.
Post a Comment