Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, amekutana na kufanya Mazungumzo na Rais wa
Jamhuri ya Uganda Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, ambapo pamoja na
mambo mengine wamekubaliana kujengwa kwa bomba la kusafirisha mafuta
kutoka Bandari ya Tanga nchini Tanzania hadi nchini Uganda.
Rais Museveni alimtembelea
Rais Magufuli katika Ikulu ndogo ya Arusha jana jioni mara baada ya
kuwasili hapa nchini akitokea nchini Uganda, ambapo leo atahudhuria
Mkutano Mkuu wa 17 wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, utakaofanyika katika Hoteli ya Ngurudoto Jijini
Arusha.
Akizungumza baada ya
viongozi hao kufanya mazungumzo ya faragha, Rais Magufuli alisema
wamekubaliana kutekeleza mradi huo wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka
Tanga hadi Uganda, kwa manufaa ya nchi zote mbili na nchi nyingine za
Afrika Mashariki.
Alisema bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,120 na kwamba mradi huo utazalisha ajira za watu zaidi ya 15,000.
Rais Magufuli aliongeza
kuwa pamoja na kujengwa kwa bomba la mafuta, pia walizungumzia kuongeza
biashara ndani ya nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki, kujenga viwanda
na kuzalisha ajira zaidi kupitia sekta mbalimbali za uzalishaji mali.
Aidha, Rais Magufuli
alisema katika Mkutano huu nchi wanachama watajadili maombi ya nchi ya
Sudan Kusini kupata uanachama ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alibainisha kuwa, kwa Sudan
Kusini kuwa mwanachama Jumuiya ya Afrika Mashariki, itakuwa na uwezo wa
kufanya biashara katika eneo lenye takribani watu milioni 150 na hivyo
kupata manufaa makubwa zaidi.
Kwa upande wake Rais Yoweri
Kaguta Museven pamoja na kuunga mkono yaliyosemwa na Rais Magufuli
alimpongeza kwa kasi yake nzuri aliyoanza nayo katika uongozi, na
alisema ni matumaini yake kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, sasa zitakuwa katika nafasi nzuri ya kwenda kwa kasi ya Rais
Magufuli katika maendeleo.
Post a Comment