Serikali kupitia Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Nape Nauye, imelifungia kwa muda wote gazeti la kila wiki
la MAWIO linalochapishwa na kampuni ya Victoria Media Services Ltd.
Katika tangazo lake lililotolewa kupitia gazeti la Serikali
notisi namba 55 ya Januari 15, 2016 Serikali imebainisha kuwa imechukua
uamuzi huo wa kulifungia gazeti la Mawio kwa muda wote kwa mujibu wa
mamlaka iliyonayo kupitia sheria ya magazeti ya mwaka 1976 sura ya 229
kifungu cha 25(1).
“Mawio linatakiwa kusimamisha uchapishaji wake kwa
kipindi chote ikiwemo pia katika vyombo vya mawasiliano vya
kielektroniki kuanzia Januari 15, 2016”, ilisema sehemu ya tangazo hilo ambalo limetolewa katika gazeti la serikali, likisainiwa na waziri Nape Nauye.
Tangazo hilo halikuweza kufafanua zaidi ni makosa gani hasa
yaliyosababisha gazeti kufungwa na kwanini adhabu iliyotolewa ni kubwa
sana ukizingatia kuwa Mawio halikuwahi kufungiwa wala kuonywa kwa kosa
lolote katika siku za wa awali.
Serikali ilianza kulikabili rasmi gazeti la Mawio 31
Desemba, 2015 kwa barua iliyoandikwa na msajili wa magazeti ikimtaka
mhariri wa gazeti hilo kutoa maelezo ya kwanini gazeti hilo lisifungiwe
kufuatia makala zake mbili zenye vichwa vya habari “Hosea kortini” na “Seif Rais Zanzibar” ambazo zilidaiwa kuzua taharuki.
“Nakujulisha kwamba ofisi ya msajili wa magazeti
haijaridhika na utetezi wako kwa kuwa hujatoa uthibitisho usio na shaka
juu ya madai ya makala ulizochapisha,”ilitamka sehemu ya barua iliyosainiwa na Raphael Hokororo, kwa niaba ya msajili.
Gazeti la Mawio ambalo huandika habari za kiuchunguzi
limefuata mkondo uleule ambao gazeti la MwanaHALISI liliufuata 30 Julai
2012 pale lilipofungiwa kwa muda usiojulikana kwa madai ya kuchapisha
taarifa za uchochezi.
MwanaHALISI lilikaa kifungoni kwa zaidi ya miaka mitatu
kabla ya kurejeshwa kwa amri ya Mahakama Kuu mwezi Agosti, 2015 kufuatia
Mkurugenzi wa kampuni ya Hali Halisi Publishers, Saed Kubeneakufungua kesi, akipinga kufungiwa kwa gazeti hilo.
Post a Comment