SAM_0054
Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, akiongea na wanachama na wananchi kwa ujumla kwenye mkutano wa kuwatambulisha watia nia ya kugombea nafasi za ubunge na udiwani katika jimbo la Singida magharibi,mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Puma,tarafa ya Ihanja
SAM_0049
SAM_0030
Baadhi ya watia nia ya udiwani na ubunge katika jimbo la Singida magharibi wakisakata ngoma za asili baada ya kumpokea mgeni rasmi katika mkutano huo.

Na Jumbe Ismailly,Ikungi      
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Singida kimewaagiza wanaachama wa chama hicho kuwashughulikia watu wote watakaobainika kukusanya vitambulisho vya kupigia kura na kuandika namba za vitambulisho hivyo,kwa lengo la kuihujumu tume,kabla ya kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Tundu Lissu alitoa onyo hilo alipokuwa akiwatambulisha wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge wa jimbo la Singida magharibi,kupitia chama hicho kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Puma,tarafa aya Ihanja,wilayani Ikungi.

Alifafanua Lissu ambaye pia ni Mwanasheria wa kambi ya upinzani Bungeni kuwa watu au mawakala wao wanaotumia nafasi za vyeo vyao kukusanya vitambulisho,kuandika majina na namba za vitambulisho hivyo,wamekuwa wakivunja sheria ya uchaguzi kwani wao siyo tume,hivyo watakaobainika hawana budi kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Watu wanaoandikisha vitambulisho majina na namba hiyo ni kinyume cha sheria ya uchaguzi wao siyo tume,tunaelewana,wanaandikisha majina ili waje wavuruge”alisisitiza kiongozi huyo wa kitaifa.

Aidha Lissu ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Singida mashariki aliweka wazi kuwa sheria za nchi hata kama watamuuliza askari aliyekuwepo katika mkutano huo,sheria zinamruhusu raia kukamata mhalifu na endapo mhalifu huyo anakataa kukamatwa,sheria inaruhusu pia nguvu kiasi itumike.

“Sheria za nchi hii zinaruhusu raia kukamata mhalifu na kama mhalifu anakataa kukamatwa,sheria za nchi hii zinaruhusu utumie nguvu kiasi kumdhibiti,sasa nguvu kiasi na ukiona anataka kukuzidi nguvu ukimpa kichapo cha uhakika siyo vibaya kabla ya kumfikisha kwenye vyombo vya sheria”alisisitiza Lissu.

Hata hivyo mjumbe huyo kamati kuu alihoji sababu za kuandikwa kwa majina ya watu ili wakayafanyie kitu gani na kuongeza kwamba walijaribu katika jimbo la Singida mashariki tangu juzi,naye aliwaagiza wawashughulikiea hadi watakapoamua kuwafikisha polisi wawe wamewalegeza viungo vyao vya kutosha.

“Hatuwezi tukafanya mchezo,hatuwezi tukaruhusu uchuro,hatutaruhusu ujinga,hatutaruhusu uhalifu,sasa kwetu sisi tuna vijiji vyote isipokuwa vitatu tu,sijui kwenye jimbo la magharibi mna vijiji vingapi,kwani anayekamatwa mpaka atakapofikishwa polisi anakuwa amelowa vya kutosha”alibainisha kwa msisitizo.

Kwa upande wake mbunge wa viti maalumu aliyemaliza muda wake,Christowaja Mtinda akijitambulisha kwa wanachama alisisitiza kwamba akina mama wajawazito,watoto wenye umri chini ya miaka mitano,wazee na walemavu wanatakiwa kupatiwa huduma za afya bure.