Dar/Dodoma.
Bunge la 10 likielekea ukingoni baada ya kupitisha Bajeti ya Serikali
leo, mambo matatu mazito yametajwa kama ‘madudu’ yaliyoleta mtikisiko na
kuonekana kama ishara ya kuisimamia Serikali na kusababisha baadhi ya
mawaziri kupoteza nafasi zao.
Mambo
hayo ni matokeo ya ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali
(CAG), Operesheni Tokomeza na ufisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo,
pamoja na kutaja kashfa hizo, baadhi ya wabunge waliozungumza na
Mwananchi wamelichambua Bunge hilo kwa mitazamo tofauti baadhi
wakimsifia Spika Anne Makinda kuwa alisimamia kanuni na wengine
wakimkosoa kwa kuilinda Serikali.
Bunge hilo
lililozinduliwa Novemba 18, 2010 kwa Rais Jakaya Kikwete kulihutubia,
anatarajia kulihutubia tena kwa hotuba ya mwisho, kati ya Julai 9 na 10,
mwaka huu na kulivunja kwa kwa mujibu wa sheria kupitia Tangazo la
Serikali (GN).
Ripoti ya CAG
Mwaka 2012,
Bunge hilo likiwa na miaka miwili tu, CAG alitoa ripoti iliyoonyesha
ufisadi mkubwa Serikalini na mawaziri kushindwa kuwajibika kisiasa
kusimamia mali za umma.
Ripoti hiyo ilizua mjadala mzito bungeni na wabunge wakashinikiza baadhi ya mawaziri wajiuzulu kutokana na kushindwa kuwajibika.
Baada ya
mvutano mkali Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri
baada ya kuwatema mawaziri sita na naibu mawaziri wawili.
Operesheni Tokomeza
Sakata
jingine lililoteka Bunge hilo ni ripoti ya Operesheni Tokomeza Ujangili
iliyoanzishwa na serikali kwa lengo la kukomesha ujangili nchini.
Operesheni hiyo ililalamikiwa na wabunge kuwa utekelezaji wake ulivunja sheria, kanuni na taratibu.
Katika
sakata hilo mawaziri wanne walitimuliwa na Januari 19, 2014 Rais Kikwete
akateua wawili wapya na naibu mawaziri wanane, huku akiwapandisha vyeo
manaibu mawaziri wanne kuwa mawaziri kamili.
2. Akaunti ya Escrow
Sakata la
uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow liliibuliwa na Mbunge
wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), David Kafulila baada ya kufichua
ufisadi uliohusisha uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Benki Kuu ya
Tanzania (BoT).
Katika
sakata hilo, mawaziri wawili walipoteza nyadhifa zao pamoja na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya Ripoti ya Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali kuwahusisha na sakata hilo.
Maofisa wengine kadhaa wa Serikali walisimamishwa au kufunguliwa mashtaka kutokana na kuhusika kwao kwenye ufisadi huo.
Kauli za wabunge
Mbali na
matukio hayo, baadhi ya wabunge wamesema katika Bunge hilo walijitahidi
kuwa wamoja katika masuala yanayoligusa Taifa, ingawa wakati mwingine
walitofautiana kwa sababu kadhaa zikiwamo za kiitikadi.
Moja ya
mambo waliyoainisha kama kasoro za Bunge hilo ni usimamiaji usioridhisha
wa Serikali katika utekelezaji wa bajeti unaosababisha fedha
zinazotengwa kutofika kwa wakati, kutofika kabisa au kufika pungufu
katika maeneo zilikopangwa.
Mbunge wa
Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF), alisema pamoja na kumpongeza
Spika Anne Makinda kwa kutekeleza mambo mengi yaliyopendekezwa, kuna
baadhi ya mambo ambayo yameachwa bila ya kujua iwapo ni kwa makusudi au
kwa bahati mbaya.
Alipoulizwa ni mambo gani alisema baadhi ya maazimio ya Bunge kuhusu sakata la Escrow hayajafika mwisho.
Mbunge wa
Makunduchi (CCM), Samia Suluhu Hassan alisema Bunge la 10 lilikuwa na
changamoto za vijana ambao walikuwa wakiwachemsha, lakini pamoja na yote
walishindana ndani ya ukumbi, lakini nje ya bunge wote walikuwa wamoja.
Alimsifu
Spika Makinda kwa kazi nzuri na kumwelezea kuwa hakuwa akibabaika
inapotokea presha za wapinzani hata ilipotokea wanasusia vikao.
Kwa upande
wake Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema) alisema Bunge la
10 linamaliza muda wake likiwa limeweka heshima kubwa kwa Watanzania
kwa kushughulikia kashfa kubwa za ufisadi.
Silinde
alitolea mfano wa masuala ya Escrow, Operesheni Tokomeza na mengine
ambayo yaliibuliwa katika bunge hilo alilosema lilikuwa limesheheni
vijana waliokuwa na mchango mkubwa katika kuibua mambo ya msingi.
Hata hivyo, alisema kuwa hawakufikia mwisho kutokana na maazimio mengi ya Bunge kuachwa bila ya kutekelezwa kama ilivyokusudiwa.
Akizungumzia
spika ajaye, Silinde alipendekeza awe walau na taaluma ya sheria ili
aweze kujua mambo ya kanuni na sheria kwa upana wake.
Mbunge
mwingine kijana, Moses Machali (Kasulu- NCCR-Mageuzi) alisema Bunge la
10 halikuwa la msisimko kwa kuwa Spika Makinda alikuwa akiibeba zaidi
Serikali na CCM na chombo hicho kushindwa kuibana Serikali pale
ilipokosea.
Alisema
Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta alikuwa akitoa nafasi sawa
ukilinganisha na Makinda, hali aliyosema ilisababisha Bunge kuyumba.
Kwa upande
wake, Prudencia Kikwembe (Viti Maalumu – CCM) alisema Bunge hilo
lilifanya kazi kwa nafasi yake lakini likakabiliwa na changamoto ya
ushabiki wa vyama badala ya maslahi ya Taifa.
Mbunge wa
Lindi Mjini (CUF), Salum Barwani yeye analia na mfumo wa kikatiba ambao
anasema kuwa ulisababisha Bunge kuwa sehemu ya Serikali.
Barwani pia alieleza kuwa hata Spika wa sasa alishindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo kutokana na mfumo wa kikatiba uliopo.
Akitoa maoni
yake kuhusu Spika ajaye, alisema awe ni kiongozi mwenye busara lakini
atambue kuwa chombo hicho ni mhimili unaojitegemea.
Alisema baadhi ya wabunge walikuwa makini kuwasilisha ujumbe kwa kuwa walikuwa wakionekana moja kwa moja kupitia runinga.
Mbunge wa
Mji Mkongwe (CUF), Ibrahim Saanya alisema Bunge limefanya kazi yake
lakini tatizo linakuja katika utekelezaji wa bajeti.
Mbunge wa
Kigoma Kusini, David Kafulila Kigoma (NCCR-Mageuzi) alisema sehemu kubwa
ya Bunge la 10 lilitawaliwa na vijana na wameweza hiyo kazi.
Alisema kuwa uchache wa wapinzani umewafanya wawe wanyonge katika kufikia uamuzi wa jumla.
Murtaza
Mangungu (Kilwa Kaskazini, CCM), alisema Bunge hilo lilikuwa la
mafanikio kwa kuwa mengi yalitimizwa na kwa kuwa walikuwa wanaonekana
kupitia TV, walifanya hadaa ili kuwaaminisha wananchi masuala ambayo
baadhi ni ya uongo na hayawezekani.
Post a Comment