Dar es Salaam. Mwenyekiti wa
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba juzi
alifanya mazungumzo ya saa mbili ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe kuhusu masuala ya uongozi na
uwajibikaji baada ya mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kumtembelea
nyumbani kwake, Masaki, Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Zitto pia alimweleza
Waziri Mkuu huyo mstaafu maazimio ya Bunge kuhusu uchotwaji wa Sh306
bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Katika ujumbe wake mfupi alioutuma katika mtandao
wa Facebook, Zitto alisema: “Nimekuwa na mkutano wa zaidi ya masaa
mawili (saa mbili) na Mzee Warioba kuhusu masuala mbalimbali ya nchi
yetu kama uongozi na uwajibikaji. Pia nimemweleza kwa ufupi kuhusu
maazimio ya Bunge kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow.”
Kukutana kwa viongozi hao kumekuja ikiwa zimepita
siku mbili tangu Jaji Warioba kuzungumza na gazeti hili kuhusu sakata la
escrow na maazimio manane ya Bunge.
Zitto alimtembelea Jaji Warioba siku habari hiyo
ilipochapishwa, kitendo ambacho kimetafsiriwa kama ni mbunge huyo
kutolea ufafanuzi maoni ya Jaji Warioba ambaye pia amewahi kuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali hasa kuhusu maeneo yaliyoachwa katika
ripoti hiyo licha ya kuwa yanaonekana kuhusika katika kashfa hiyo.
Bunge lilihitimisha mjadala wa kashfa hiyo, kwa
kupitisha maazimio manane, ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Frederick Werema, Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Katibu Mkuu wa Nishati na Madini,
Eliakim Maswi.
Bunge hilo pia liliazimia kuwajibishwa kwa wajumbe
wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco pamoja na wenyeviti watatu wa kamati
za kudumu za Bunge; Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), William
Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na William Ngeleja (Bajeti).
Katika maoni yake juu ya kashfa hiyo, Jaji Warioba
alisema Bunge limefanya makosa ya kutozijumuisha Wizara ya Fedha na ile
ya Viwanda na Biashara katika uchunguzi huo kwa kuwa nazo zinahusika.
Alisema katika Ripoti ya CAG na PAC, wametaja
ukiukwaji wa malipo ya kodi ya ongezeko la mtaji (capital gain) na
ushuru wa stempu (stamp duty) na kuwa wanaohusika katika hilo ni Wizara
ya Fedha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na upande mwingine ni
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) ambao uko chini ya
Wizara ya Viwanda na Biashara.
Alisema hata kampuni iliyotajwa kuwa imesajiliwa
Brela inaonyesha katika ripoti kuwa wahusika walioisajili hawakuweka
majina yao, bali saini tu.
Alifafanua kuwa uamuzi wa Bunge uliilenga Wizara
ya Nishati na Madini lakini hasara iliyotajwa kuonekana inazihusu zaidi
Wizara ya Fedha na ile ya Viwanda na kusisitiza kuwa uamuzi wa Bunge
ulitawaliwa na mchezo wa siasa, kwamba baadhi walindwe na wengine
waachwe.
Jaji Warioba alisema kasoro nyingine ni kitendo
cha watu wanaodaiwa kupewa fedha na James Rugemalira kutajwa majina yao
sambamba na akaunti ya aliyewapa, lakini wale waliodaiwa kuchota fedha
hizo katika magunia hawakutajwa.
Post a Comment