Uamuzi huo wa TRAB ulitolewa na Katibu wake,
Respecius Mwijage kutokana na maombi yaliyofunguliwa na Kampuni za Pan
Africa Power Solution Tanzania Limited (PAP) na IPTL dhidi ya Kamishna
Mkuu wa TRA na Msajili wa Kampuni ya Usajili wa Leseni (Brela).
PAP na IPTL zilifungua maombi hayo, baada Kamishna
Mkuu wa TRA kuziandikia barua ya kusudio la kuziondoa hati hizo kwa
madai ya kuwapo kwa mkataba bandia wa mauziano ya hisa hizo kati ya
Kampuni ya Mechmar na Piperlink Investment Limited sambamba na kati ya
Piperlink na PAP.
Katika maombi yake, PAP na IPTL ziliomba
walalamikiwa wazuiliwe aidha wao wenyewe, mawakala wao, waajiri wao au
mtu yeyote atakayefanya kazi kwa niaba yao kuondoa hati hizo
zinazothibitisha kulipwa kwa kodi ya ongezeko la mtaji kuhusiana na
uuzaji wa hisa.
Hati hizo namba 004965600 na 0049657 zilitolewa
kwa ajili ya uuzaji wa hisa kutoka Mechmar na Piperlink Investment
Limited na kati ya Piperlink na PAP.
Katika maombi hayo yaliyoambatanishwa na hati ya
kiapo cha wakurugenzi wa kampuni hizo, Manraj Bharya na Parthiban
Chandrasakaran, waliomba zuio la kuondolewa kwa hati hizo hadi rufani
yao waliyokata katika bodi hiyo kupinga uamuzi wa TRA itakaposikilizwa
na kutolewa uamuzi.
Katika uamuzi wake, TRAB ilikubaliana na maombi hayo na kutoa amri hiyo ya zuio la Mkuda kusubiri uamuzi wa rufaa hiyo.
“Nia ya kuondoa hati hizo ilitolewa na Kamishna
Mkuu wa TRA, kupitia barua yake ya Novemba 19, mwaka huu, ikielekezwa
kwa Msajili wa Brela isimamishwe hadi maombi yatakaposikilizwa Desemba
10, mwaka huu.” alisems Katibu Mwaijage
Kwa mujibu wa hati hizo za viapo
zilizoambatanishwa katika maombi yake, PAP na IPTL zimesajiliwa kihalali
nchini kwa mujibu wa sheria za kampuni na kazi zao ni kufanya shughuli
za kuzalisha umeme.
Zinaeleza kuwa kama TRA haitazuiliwa kutekeleza
azma yake ya kuziondoa hati hizo kusubiri uamuzi wa rufaa yake, basi
mlalamikaji ataingia hasara isiyolipika.
Mbali na rufaa hiyo waliyokata TRAB, pia
walalamikaji wanadai kuwa kwa sasa kuna kesi mbalimbali ambazo bado
zinaendelea Mahakama Kuu na nyingine Mahakama ya Biashara.
Post a Comment