PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: MZEE MSEKWA AANIKA SIRI YA MUUNGANO
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
WIKI mbili kabla ya Tanzania kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Mse...

WIKI mbili kabla ya Tanzania kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa ametoboa siri ya Muungano huo akisema “mchakato wa kuundwa kwake ulifanywa kwa siri na haraka sana,” kutokana na upepo wa kisiasa na usalama wa kipindi hicho. Akizungumza katika moja ya mfululizo wa vipindi vya miaka 50 ya Muungano vinavyorushwa na Redio ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC Taifa), Msekwa alisema woga wa hayati Abeid Amani Karume kupinduliwa na maadui, ulikuwa ni miongoni mwa sababu za kuharakisha Muungano huo.


Msekwa aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati Muungano unaasisiwa, alisema pia yeye na wenzake walichelewa kujua kwamba Mwalimu Julius Nyerere (Rais wa Kwanza wa Tanganyika) na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Karume walikuwa na majadiliano ya kuunganisha nchi hizo.


“Kikubwa cha kusema ni kwamba mazungumzo ya Muungano huo yalifanywa kwa siri.... kwa siri sana baina ya waasisi wa nchi hizo. Kwa nini yalifanywa kwa siri? Siyo kwa sababu walikuwa wababe, la hasha, bali kwa mazingira ya wakati ule, kulikuwa na maadui ambao wasingependa nchi hizi kuungana,” alisema Msekwa na kuongeza:


“Kwa woga huohuo, ndipo Mwalimu alipokubaliana na mwenzake wafanye mazungumzo ya siri mpaka waliposaini yale makubaliano na kunijulisha.”


Msekwa ambaye pia amewahi kuwa Spika wa Bunge la Muungano, alisema baada ya makubaliano ya Muungano, Nyerere alimwita na kumjulisha kuwa walishakubaliana (na Karume) kuungana, hivyo walihitaji baraka za Bunge kuridhia Muungano huo.


“Mwalimu akaniambia, ‘wewe Katibu wa Bunge unaweza ukawaita wabunge wakaja kwa harakaharaka kuridhia makubaliano?’


“Nakumbuka siku hiyo ilikuwa Jumanne na Mwalimu alipendekeza wabunge wafike Ijumaa ya juma hilohilo, nao wabunge wakaja wakaridhia.”


Simulizi hii ya Msekwa kuhusu Muungano imekuja wakati kukiwa na vuguvugu la muundo wa Muungano katika Bunge Maalumu la Katiba, kutokana na mapendekezo yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba kupendekeza serikali tatu badala ya Serikali mbili za sasa.


Bunge kuridhia
Aliongeza kuwa, baada ya Bunge la Tanganyika kuridhia Mwalimu Nyerere aliutaka muswada huo “kwa haraka sana” ili aufanye kuwa sheria na alitaka kupelekewa kwa mkono.


“Baada ya wabunge kuridhia pale Karimjee, nikauchukua muswada na kuupeleka Ikulu, sio mbali pale.

chanzo: MWANANCHI

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top