NA: ANADREA NGOBOLE, ARUSHA
MAHAKAMA ya Afrika ya haki za binadamu leo imetolea maamuzi mashauri tisa yaliyofunguliwa katika mahakama hiyo ambapo katika mashauri hayo tisa mashauri nane yalikuwa dhidi ya serikali ya Tanzania.
Miongoni mwa mashauri yaliyotolewa maamuzi na mahakama hiyo ni shauri namba 11/2020 lililofunguliwa na kituo cha sheria na haki za binadamu kwa kushirikiana na Bob Chacha Wangwe kupinga sheria ya uchaguzi inayowaidhinisha wakurugenzi wa halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi.
Katika shauri hilo wafungua shauri waliwakilishwa na mawakili Furgence Masawe, Jebra Kambole, Paulo Kisabo na Amani Joachim na kwa upande wa serikali iliwakilishwa na wakili Mkama Musalamu na Christabella Madembwe kutoka ofisi ya mwanasheria mkuu wa Serikali.
Hoja ya msingi kupinga kifungu hicho kwa wafungua shauri ilikua ni kwamba wakurugenzi wa Halmashauri wanavinasaba vya kisiasa kwa kuwa wao ni wateule wa Rais lakini pia haijaanishwa sifa tofauti katika uteuzi wao zinazowawezesha kuwa na sifa za kuwa wasimamizi wa uchaguzi ambao utakua huru na haki.
Akisoma hukumu hiyo mahakamani hapo Jaji Dennis Dominic Adjei amesema kwa pamoja majaji hao wamekubaliana na hoja za wapeleka maombi kwa hoja walizoziwasilisha na maamuzi ya mahakama hiyo ikatoa miezi 12 kwa serikali ya Tanzania kubadili kifungu hicho kinachotumika kuteua wakurugenzi kuwa wasimamizi wa uchaguzi na kuiagiza serikali ya Tanzania ndani ya miezi sita kuwasilisha taarifa katika mahakama hiyo imefikia hatua gani katika kutekeleza maamuzi hayo ya mahakama.
Maamuzi hayo ya mahakama ya Afrika ya haki za binadamu yameendana na hukumu ya awali iliyotolewa na mahakama kuu kuhusiana na shauri hilo lilipofunguliwa katika mahakama kuu na baadae serikali kukata rufaa mahakama ya Rufaa ya Tanzania na mahakama hiyo kutengua uamuzi wa mahakama kuu hali iliyopelekea Wangwe na LHRC kuamua kupeleka shauri hilo mahakama ya Afrika ambayo leo imelitolea maamuzi.
Mahakama hiyo pia ilitolea uamuzi shauri namba 039/2020 lililofunguliwa na kituoa cha sheria na haki za binadamu kwa kushirikiana na Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania ambapo walifungua shauri dhidi ya serikali ya Tanzania kupinga kifungu cha sheria ya makossa ya jinai namba 145 kifungu kidogo cha 5 kinachonyima haki ya mtuhumiwa kupata dhamana.
Kifungu hicho kimeanisha makossa mbalimbali ambapo katika makossa hayo kuna makossa yametajwa kutokua na dhamana pindi mtu anapotuhumiwa kuyatenda.
Katika shauri hilo wapeleka maombi walitoa sababu za kupinga kifungu hicho kuwa kinakiuka haki za binadamu na pia kinaingilia uhuru wa mahakama katika kuendesha mashauri mahakamani kwa mtuhumiwa kuwekwa ndani hata kabla ya mahakama kumthibitisha kuwa ana hatia.
Mahakama katika kupitia shauri hilo majaji wa mahakama hiyo wamejiridhisha kuwa kifungu hicho kinakiuka misingi ya haki za binadamu na hivyo kuiagiza serikali ya Tanzania kukifanyia marekebisho kifungu hicho na kuhakikisha marekebisho hayo yanawekwa katika tovuti ya Mahakama, mbao za matangazo za mahakama ili wananchi wote kuelewa mabadiliko hayo.
Akizungumza mara baada ya maamuzi hayo ya mahakama kutolewa wakili Jebra Kambole alisema hiyo ni hatua kubwa kufikiwa kwa nchi hivi sasa wakati Rais akiwa ameunda tume ya haki jinai kwa dhamira ya kuhakikisha kunafanyika maboresho makubwa ya sheria za haki jinai.
Kambole alifafanua kuwa tume hiyo inapaswa sasa kutumia uamuzi huo wa mahakama kuishauri serikali kutekeleza kwa haraka ili dhamira njema ya Rais kwa nchi yake kuwezesha wananchi kupata haki wanazostahili itimie.
Post a Comment