NA: MWANDISHI WETU, BABATI
Wakazi wawili wa kijiji cha Endagire wilayani Babati mkoani Manyara wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kukutwa na meno ya tembo bila ya uwa na kibali cha uwindaji.
Waliohukumiwa kifungo hicho na mahakama ya wilaya hiyo ni John Lulu (42) na Zebedayo Safari (34)
Akisoma hukumu hiyo mahakamani hapo jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi Victor Kimario alisema washtakiwa hao wametiwa hatiani kwa kosa la kumiliki kinyume cha sheria meno mawili ya tembo ambayo ni nyara ya serikali.
Hakimu Kimario alisema kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Octoba 23 mwaka 2022 wakiwa katika kijiji cha Burukeli wilaya ya Babati.
Katika hukumu hiyo alisema washtakiwa hao walikamatwa wakiwa wanasafirisha vipande viwili vya meno ya tembo yenye thamani ya shilingi million 35.1 ambayo ni sawa na tembo mzima.
“Baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka uliowasilisha vielelezo tisa ambavyo vilithibitisha mahakama hiyo kuwa washtakiwa walikutwa na nyara za serikali na kisha kusikiliza upande wa utetezi mahakama imejiridhisha pasipo na shaka kwamba walitenda kosa hilo.”
“Kutokana na kosa hilo mahakama hii inawatia hatiani kwa kukiuka kifungu cha 86 (1) (2) (b) cha sheria ya uhifadhi wa wanyamapori sura ya 283 ya sheria iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Kabla ya kusomwa hukumu hiyo wakili wa serikali Rusticus Mahundi akisaidiwa na wakili Abood Komanya alidai mahakamani humo kuwa washtakiwa hawana rekodi ya kufanya makosa ya uhalifu ila kwa kiwa Wanyamapori wana mchango mkubwa katika pato la Taifa ni vyema mahakama hiyo ikawapa adhabu wanayostahili iwe fundisho kwa watu wengine.
Mamlaka za serikali ikiwepo, Mamlaka ya usimamizi wanyamapori (TAWA) ,Hifadhi ya Taifa ya Tarangire , Mwekezaji sekta ya Utalii taasisi chem chem , Burunge WMA na halmashauri Babati wamekuwa wakiendesha ulinzi wa pamoja kupambana na matukio ya ujangili.
Hadi Sasa watuhumiwa kadhaa wa ujangili wa Tembo na Twiga wamekamatwa na kufikishwa mahakamani mkoani Manyara.
Post a Comment