Na. Josephine Majura WFM, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamadi Hassan Chande, amewataka wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini hususani Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM), kufanya kazi kwa ubunifu, uaminifu na uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa, ufisadi, wizi na matumizi ya madawa ya kulevya.
Rai hiyo imetolewa, jijini Dar es Salaam wakati wa mahafali ya 48 ya Chuo Cha Usimamizi wa Fedha katika Kampasi Kuu ya Dar es Salaam, ambapo zaidi ya wahitimu 4,000 wametunukiwa tuzo mbalimbali
Alisema kuwa IFM imekuwa mstari wa mbele katika kuongeza idadi ya watanzania wenye taaluma na utaalamu katika Sekta ya Fedha, Uhasibu, Bima na Hifadhi za Jamii hivyo ni vema idadi hiyo iendane na kukidhi mahitaji ya soko ambayo yanahitaji wanataaluma wenye weledi na uadilifu.
Mhe. Chande ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuzalisha wataalamu katika fani mbalimbali na kuliwezesha Taifa kufikia malengo yake ya kujitosheleza katika fani za fedha kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi, kiteknolojia, kisiasa na kijamii.
Kwa upande wa Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Mhe. Chande, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuongeza kiwango cha wanafunzi wanaopata mikopo mwaka hadi mwaka ili wanafunzi wenye sifa waweze kunufaika.
Alisema jambo hilo litawezekana endapo wale wote waliopata mkopo wa Serikali kwa ajili ya kuwasaidia kuweza kutimiza ndoto zao watarejesha mikopo waliyopata kwa wakati hivyo kuiongezea Serikali uwezo wa kutoa fursa za mikopo kwa wanafunzi wengi zaidi.
Katika mahafali hayo Kaimu Mkuu wa Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dkt. Imanueli Mnzava, alisema Chuo kimeendelea kurahisisha upatikanaji wa mafunzo kwa wananchi kwa kusogeza huduma za mafunzo hayo karibu na wahitaji.
“Chuo kina kampasi Mwanza, Dodoma, Simiyu na sasa tunamalizia ujenzi Kampasi ya Geita kwa ufadhili wa Serikali, kama tunavyofahamu elimu ni chachu ya mabadiliko ya kitabia, kiutendaji na uwezo wa kubadilisha mazingira yanayotuzunguka”, Alisema Dkt. Mnzava.
Aliongeza kuwa licha ya mafanikio mbalimbali yaliyopatikana chuoni hapo, alieleza kuwepo kwa uhaba wa madarasa, ofisi na mabweni ya wanafunzi hivyo kuiomba Serikali isaidie kupata majengo yaliyo karibu na Chuo ili kurahisisha utoaji wa elimu bora kulingana na mahitaji ya soko.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo, Prof. Emanuel Mjema, alisema Baraza la Uongozi la Chuo litaendelea kusimamia utekelezaji wa malengo ya Chuo na kuainisha vipaumbele kwa kuzingatia misingi ya tija na upatikanaji rasilimali ili kuboresha viwango vya wahitimu w2atakaoweza kujiajiri wenyewe na kujitegemea na pia kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kilianzishwa mwaka 1972 kikiwa na uwezo wa kutoa kozi mbili, ambapo jumla ya wahitimu 59 walihitimu mwaka huo. Chuo hicho kinatoa zaidi ya kozi 33 katika fani mbalimbali ikiwemo Fedha, Bima, Uhasibu na nyinginezo ambapo hadi mwaka 2021 jumla ya wahitimu 39,723 walitihimu chuoni hapo katika kozi mbalimbali
Post a Comment