Na. Farida Ramadhani na Haika Mamuya, WFM, Dodoma
Serikali imezindua Awamu ya Sita ya Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP VI) ili kuongeza ufanisi katika kusimamia mapato ya ndani pamoja na kudhibiti matumizi ya fedha za umma.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Salum Mkuya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Dkt. Mkuya alisema utekelezaji wa programu hiyo unafanyika kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Wadau wa Maendeleo ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato na urasimishaji wa sekta zisizo rasmi lengo likiwa kupata mchango wao kwenye ukusanyaji wa mapato hayo.
“Serikali itazijengea uwezo taasisi zote zinazohusika na masuala ya usimamizi wa matumizi ya umma zikiwemo taasisi za ukaguzi na Bunge ili kuzuia mianya yote ya ufujaji wa fedha za umma na kuongeza uwazi na uwajibikaji”, alisema Dkt. Mkuya.
Dkt. Mkuya alisema programu hiyo pia imehusisha masuala ya jinsia na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yatasimamiwa kuanzia wakati wa uandaaji na utekelezaji wa bajeti.
Aidha aliwapongeza wadau wa maendeleo ambao wameendelea kushirikiana na Tanzania katika programu mbalimbali za maendeleo hususani programu za usimamizi wa fedha za umma.
Naye Mwakilishi wa Wadau wa Maendeleo, Bi. Milou Vanmulken, amesema Wadau wa Maendeleo wataendelea kushirikiana na Tanzania Bara na Visiwani katika kufanikisha ajenda ya maendeleo kupitia PFMRP.
Alisema wapo tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza programu hiyo muhimu ambayo wanaamini kwa kiasi kikubwa italeta maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Aidha aliipongeza Serikali kwa kuweza kutekeleza programu mbalimbali zilizopita ambazo changamoto zake zimewezesha kutengeneza programu mpya ambayo utekelezaji wake utaongeza ufanisi na uwajibikaji katika usimamizi wa matumizi ya fedha za umma.
Awali akitolea ufafanuzi wa programu hiyo, Mratibu wa Mradi, Bw. Denis Mihayo alisema Programu za Usimamizi wa Fedha za Umma zimeanza miaka ya 90 kwa awamu tofauti za miaka mitano.
Alisema kila baada ya awamu kumalizika hufanyika tathmini ambazo matokeo yake husaidia kuanzisha awamu nyingine ili kutatua changamoto zilizojitokeza katika awamu iliyotangulia.
Bw. Mihayo alisema mafanikio ya awamu zilizopita ni kuanzishwa kwa mifumo mbalimbali ya ukusanyaji mapato kama vile GePG kwa Tanzania Bara, Zan Malipo kwa Zanzibar na TAUSI unaotumiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI
Post a Comment