Kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzanite One imekubali kuilipa Serikali fidia pamoja na kodi watakayokubaliana kutokana na dosari zilizokuwepo hapo awali.
Makubaliano hayo yametiwa saini Jijini DSM na Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Rais Dkt. Magufuli Profesa Palamagamba Kabudi na Mkurugenzi wa Tanzanite One Faisal Juma.
Akizungumza mara baada ya kutia saini makubaliano hayo, Mwenyekiti wa kamati ya majadiliano kwa upande wa Serikali, Prof. Palamagamba Kabudi amesema
Tanzanite One imekubali kulipa fidia Serikali kutokana na mambo
iliyofanya ambayo yalikuwa kinyume na utaratibu ulioleta hasara kwa
Serikali.
Amesema fidia hiyo inatakiwa kulipwa kwa awamu ambapo awamu
ya kwanza italipwa ndani ya wiki mbili kuanzia leo na haitahusisha
Kodi. Pia Kampuni hiyo Tanzanite One italazimika kulipa kodi kama
kawaida inazodaiwa na Serikali na tozo nyingine zote zinazodaiwa na
Serikali.
Pia Serikali imekubaliana na Kampuni ya Tanzanite One kuwa
itafuata masharti yote ya sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo
inaeleza kuwa ni Watanzania tu ndio wanaoruhusiwa kuchimba madini ya
Vito na pale ambapo watanzania hawana uwezo huo ndipo wanapoweza kuingia
ubia na wageni.
Aidha Prof. Kabudi amesema kuhusu wachimbaji wadogo
wadogo wa Tanzanite katika eneo la Mirerani utaratibu mpya unawekwa
lengo kubwa ikiwa ni kutekeleza sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo
inalenga madini ya vito kuwa mikononi mwa Watanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzanite One Faisal Juma amemshukuru Rais Magufuli kwa
kuunda kamati hiyo ya kizalendo katika kufuatilia rasilimali za madini
nchini ambapo wameweza kujadiliana na kufikia muafaka wa kulipa fidia
ikiwa ni mbali na malipo yote yaliyotakiwa kulipwa serikali ikiwemo
kodi.
Amesema Tanzanite One itahakikisha inafuata taratibu zote
za Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kwa lengo la kuhakikisha rasilimali ya
madini inawanufaisha Watanzania na kwamba uvunjifu wa sheria uliofanywa
na kampuni hiyo hautajirudia tena.
“Sisi kama Tanzanite One tunaihakikishia Serikali
kuwa uaminifu uliotuonyesha na sisi pia kama Kampuni tutahakikisha
tunakuwa waaminifu na kuwa zao hili linanufaisha taifa kutokana na imani
aliyotuonyesha Rais kama wananchi wake kutupa nafasi na fursa ya
kusikilizwa ili kurekebisha makosa tuliyoyatenda” amesema Faisal.
Faisal amesema Tanzanite One itahakikisha haitafanya
makosa iliyofanya mara ya kwanza na hivyo kuwa mfano wa kampuni
nyingine za madini kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha
Watanzania.
Post a Comment