Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwaongoza Maafisa wa
Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania– TAWA,
Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la
Ngorongoro kupiga gwaride la ukakamavu muda mfupi baada ya kuwatunuku
vyeti vya kuhitimu mafunzo ya Jeshi Usu hivi karibuni katika kituo cha
Mlele mkoani Katavi.
Na Hamza Temba-WMU
........................................................
Wakati
huu tunapoadhimisha miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ni
takriban miaka miwili sasa na miezi kadhaa tangu Serikali ya awamu ya
tano, inayoongozwa na Mhe. Rais, Dk. John Pombe Joseph Magufuli iingie
madarakani.
Itakumbukwa
kuwa katika hotuba yake ya kwanza ya kulihutubia Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania akiwa mjini Dodoma, Mhe. Rais Magufuli alitoa
vipaombele kadhaa vya kutekelezwa na wizara zake huku Wizara ya
Maliasili na Utalii akiipa vipaombele vikuu vitatu ambavyo ni
kukabiliana na ujangili, kutatua migogoro ya mipaka kwenye maeneo ya
hifadhi na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Wizara
ya Maliasili imeendelea kutekeleza vipaombele hivyo pamoja na jukumu
lake la msingi la kuhifadhi na kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali
za maliasili na malikale, na kuendeleza Utalii kwa faida ya kizazi cha
sasa na kizazi kijacho.
Ujangili
Wizara
imefanikiwa kuanzisha mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ujangili na
biashara haramu ya wanyamapori ambayo imeanza kuzaa matunda.
Mikakati
hiyo ni pamoja na kuanzishwa kwa Kikosi Kazi Maalum cha Kudhibiti
Uhalifu wa Misitu na Wanyamapori nchini ambacho kilianzishwa mwezi
Julai, 2016 sambamba na kuimarishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambayo ilianza majukumu yake rasmi tarehe 1
Julai, 2016.
Mikakati
mingine ni mabadiliko ya mfumo wa utendaji kutoka ule wa kiraia kwenda
wa Jeshi Usu, matumizi ya teknolojia ya ndege zisizokuwa na rubani
(drones) kwa ajili ya doria, ushirikishwaji wa wananchi kwenye uhifadhi
na matumizi ya mbwa maalum wa kunusa ili kutambua nyara katika viwanja
vya ndege na bandari.
Kupitia
mikakati hiyo, mwaka 2016/2017 Wizara kupitia taasisi zake iliendesha
doria mbalimbali ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa na kufanikiwa
kukamata watuhumiwa 7,085 kwa makosa mbalimbali. Aidha, meno ya tembo
129 na vipande 95 vyenye uzito wa jumla ya kilo 810.03 vilikamatwa.
Vielelezo
kadhaa pia vilikamatwa ikiwemo silaha za kivita 48, silaha za kiraia
150, risasi 1,058, magobore 406, silaha za jadi 22,307 na roda 120,538.
Jumla
ya kesi 2,097 zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali na kesi 802
zilimalizika. Watuhumiwa 472 katika kesi 262 walifungwa jela jumla ya
miezi 42,153 na watuhumiwa 79 katika kesi 43 waliachiwa huru huku
watuhumiwa wengine 469 katika kesi 276 wakilipa faini ya jumla ya
shilingi milioni 452.1.
Katika
kuelekea kwenye Mfumo wa Jeshi Usu, Wizara imeendesha mafunzo kwa
watumishi 661 kuhusu ukakamavu, uongozi na ukusanyaji wa taarifa za
kiintelijensia kuhusu Ujangili. Watumishi walioshiriki mafunzo hayo ni
139 kutoka TAWA, 388 kutoka TANAPA, 117 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya
Eneo la Ngorongoro na 17 kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania.
Kutokana
na jitihada hizi hali ya ujangili imepungua kwa kiasi kikubwa. Kwa
mfano, katika Pori la Akiba Selous idadi ya Tembo waliouwawa imepungua
kutoka tembo 17 mwaka 2015/16 hadi tembo 7 mwaka 2016/17.
Hata
hivyo, katika siku za hivi karibuni, wanyamapori hasa tembo wameanza
kuonekana katika maeneo mbalimbali ambayo kwa kipindi kirefu hawakuwa
wakionekana, mfano hivi karibuni tembo kadhaa walionekana katika Chuo
Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Aprili
18 mwaka huu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla
akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke ofisini
kwake mjini Dodoma, alinukuliwa akisema kuwa ujangili hapa nchini
umepungua kwa zaidi ya asilimia 50.
Alisema
katika kipindi cha miezi sita iliyopita hadi kufikia mwezi huu wa
Aprili hakuna mauaji mapya ya wanyamapori yaliyoripotiwa kuhusiana na
ujangili na kwamba nyara zinazokamatwa hivi sasa ni masalia ya zamani
ambayo yanatafutiwa masoko.
Alisema
mafanikio hayo yametokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali
kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama sambamba na kuwashirikisha
wananchi kwa kuimarisha ulinzi na doria za mara kwa mara za
kiitelijensia katika maeneo ya hifadhi.
Utalii
Katika
kuongeza idadi ya watalii nchini, Wizara imeendelea kutekeleza shughuli
mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya
hifadhi, kuboresha miundo mbinu kwenye maeneo ya vivutio, kuanzisha
huduma mpya za utalii pamoja na utangazaji.
Juhudi
hizo zimewezesha ongezeko la watalii wa kimataifa kutoka 1,284,279
mwaka 2016 hadi kufikia 1,327,143 mwaka 2017 sawa na ongezeko la
asilimia 3.2.
Aidha,
mapato yanayotokana na utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani
bilioni 2.1 mwaka 2016 hadi Dola za Marekani bilioni 2.2 mwaka 2017.
Sekta
hii ya utalii imetoa ajira takriban 500,000 za moja kwa moja na ajira
nyingine milioni moja zisizo za moja kwa moja kwa mwaka.
Sekta hii pia inachangia takriban asilimia 17.5 ya Pato la Taifa na wastani wa asilimia 25 ya fedha zote za kigeni.
Aidha,
Wizara imedhamiria kupanua wigo wa vivutio vya utalii nchini kwa
kufungua utalii wa Kanda ya Kusini ili kuongeza idadi ya watalii na
mapato ya Serikali.
Kupitia
dhamira hiyo Serikali imesaini mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya
Dunia wa Dola za Marekani milioni 150, sawa na takriban shilingi bilioni
340 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Kusimamia Maliasili na Kuendeleza
Utalii wa Ukanda wa Kusini –REGROW.
Mradi
huu ambao maandalizi yake yalianza mwezi Novemba 2014 ulizinduliwa
rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia
Suluhu Hassan tarehe 12 Februari, 2018 katika viwanja vya Kihesa Kilolo
Mjini Iringa huku Kauli Mbiu yake ikiwa “Utalii kwa Maendeleo Endelevu-
Karibu Kusini”.
Mama
Samia alisema lengo la mradi huo ni kuongeza mchango wa sekta ya
maliasili na utalii katika uchumi wa taifa kwa kuboresha vivutio vya
utalii, miundombinu, usimamizi wa vivutio na kuongeza faida za kiuchumi
kwa jamii zinazoishi jirani na maeneo ya hifadhi katika ukanda huo wa
kusini.
Katika
kuongeza jitihada za kutangaza utalii ndani na nje ya nchi, Wizara
imeendelea kuongeza bajeti ya utangazaji ambapo Bodi ya Utalii Tanzania
kwa mwaka wa fedha 2017/18 imeongezewa bajeti kufikia shilingi bilioni
6.6 ikilinganishwa na shilingi bilioni 4.1 mwaka 2016/2017 na bilioni
4.3 mwaka 2015/16.
Aidha,
katika kufungua masoko mapya ya utalii nje ya nchi, Wizara inaangazia
masoko mapya katika nchi za China, Israel, Urusi, Australia na nchi
nyingine za Skandinavia.
Wananchi wanavyonufaika na uhifadhi
Wizara
ya Maliasili inaendelea na juhudi za kuhakikisha wananchi wanaoishi
jirani na maeneo ya hifadhi wananufaika na rasilimali zilizopo. Kupitia
Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori, jamii zinanufaika kwa kupata ajira,
kitoweo, elimu, miradi ya kijamii na kuongeza kipato.
Hadi
hivi sasa jumla ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori 38 zimeanzishwa.
Aidha, wananchi wanaoishi jirani na misitu wananufaika kupitia miradi ya
ufugaji nyuki ambapo kupitia uwezeshaji wa Mfuko wa Misitu Tanzania
miradi 254 ya kuboresha kipato cha jamii zinazoishi pembezoni mwa misitu
imetekelezwa.
Miradi
hiyo ni ya ufugaji nyuki ambapo vikundi vya ufugaji nyuki 399 na watu
binafsi 27 wamewezeshwa kupata mizinga ipatayo 11,730.
Udhibiti wa migogoro baina ya wananchi na hifadhi
Katika
kudhibiti migogoro ya mipaka kati ya wananchi na maeneo jirani na
hifadhi, Wizara kwa kushirikiana na Taasisi za Serikali na Wadau
imeendelea kuhakiki mipaka yote ya maeneo ya hifadhi na kuweka alama za
kudumu na mabango ya tahadhari.
Hadi
kufikia mwezi Mei, 2017 vigingi 14,755 vimesimikwa sawa na asilimia
62.4 ya vigingi 23,638 vinavyohitajika katika Hifadhi za Misitu, Mapori
ya Akiba, Hifadhi za Taifa na Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro.
Aidha,
kupitia program ya Panda Miti Kibiashara, Wizara imewezesha vijiji 48
kuandaa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi katika Wilaya za Ludewa,
Madaba, Makete, Mufindi, Njombe Mjini, Njombe Vijijini, Kilolo na Nyasa.
Mikakati mipya chini ya Waziri wa Maliasili, Dk. Hamisi Kigwangalla
Aidha
chini ya Uongozi Mpya wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla ipo baadhi ya mikakati yake mipya inayolenga kutoa uelekeo
mpya wa kuimarisha sekta Maliasili na Utalii nchini.
Dk.
Kigwangalla anaeleza mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuanzisha kwa
mwezi maalum wa Urithi wa Mtanzania (Tanzania Heritage Month) ambao
utaadhimishwa mwezi Septemba kila mwaka, kuanzishwa kwa Makumbusho ya
Marais Wastaafu waliotawala Tanzania mjini Dodoma na Kuboresha na
kuendeleza utalii wa fukwe kwa kuanzisha Mamlaka ya Fukwe.
Mikakati mingine ni pamoja na kujenga makumbusho ya meno ya tembo katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha na Iringa pamoja na kutambua barabara iliyokuwa ikitumika katika biashara ya utumwa wakati wa ukoloni ili iweze kutumika kiutalii.
Akizungumzia
migogoro ya mipaka iliyopo baina ya wananchi na maeneo ya hifadhi, Dk.
Kigwangalla amesema Serikali itatatua migogoro hiyo kwa kushirikisha
wananchi sambamba na kuwasaidia kutatua changamoto za msingi ambazo ni
kuimarisha maeneo ya malisho ya mifugo, upatikanaji wa maji kwa ajili ya
wananchi na mifugo, mpango bora wa matumizi ya ardhi na uendelezaji wa
kilimo na ufugaji.
Kwa
upande wa vitalu vya uwindaji wa kitalii, Dk. Kigwangalla amesema
Serikali itafanya mabadiliko katika mfumo wa ugawaji vitalu vya uwindaji
wa kitalii kutoka mfumo unaotumika hivi sasa wa Kamati “Administrative
Allocation” na kutumia mfumo wa mnada “Auction”.
Lengo
ikiwa ni kuongeza uwazi na kuruhusu nguvu ya soko kuamua bei ambapo
mapato ya Serikali nayo yatatarajiwa kuongezeka maradufu. Ili kutekeleza
hilo, sheria na kanuni zinafanyiwa marekebisho.