Arusha.Kikao cha Makatibu wakuu wa wizara ya Maliasili na Utalii wa Kenya na Tanzania na wizara ya Afrika ya Mashariki juzi kumevunjika bila kupatikana suluhu ya mgogoro wa serikali ya Kenya kuzuia magari ya Tanzania kuchukuwa watalii uwanja wa Jomo Kenyatta.
Kutokana na kuvunjika kikao hicho, jana Waziri wa Utalii wa Kenya, Phyllis Kandaye amesusa kuhudhuria kikao cha kutafuta suluhu na Waziri wa Tanzania, Lazaro Nyarandu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu,alisema alifika Arusha kuhudhuria kikao na Waziri mwenzake wa Kenya, kujadili mgogoro huo, lakini hakutokea baada kuvunjika kikao cha juzi.
Alisema kikao hicho, kilikuwa ni utekelezaji wa makubaliano ya kikao cha awali, walichokifanya Nairobi nchini Kenya, kujadili kutatua mgogoro huo na walikubaliana kitanguliwe kikao cha wataalam na makatibu wakuu.
Nyarandu alisema, walikubaliana kikao hicho, kiwe na ajenda moja tu ni kwa nini serikali ya Kenya, imezuia magari ya Tanzania kuingia uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, kuchukuwa watalii na kuingiza watalii.
Alisema serikali ya Kenya, kuzuia magari ya Tanzania, kuingia uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, ni kukiuka mkataba wa ushirikiano katika sekta ya Utalii,uliosainiwa mwaka 1985 ambao unatoa ruhusa magari ya kila nchi kuingia katika nchi nyingine kuleta watalii.
"tulikubaliana magari ya Kenya, yanaweza kuingia Tanzania, katika miji ya Arusha, Moshi, Tanga na Musoma kuleta watalii, hivyo hivyo magari ya Tanzania kuingia Kenya lakini tunashangaa wenzetu wameweka zuio la magari yetu na yao yanaingia nchini"alisema
.
.
Akizungumzia kuvunjika kikao chao, Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii,Adelhelm Meru alisema kilivunjika baada ya wajumbe wa Kenya,kutaka kufumuliwa mkataba wa ushirikiano wa utalii uliosainiwa mwaka 1985.
Alisema wajumbe wa Kenya wakiwakilishwa na Katibu Mkuu wa wizara ya Utalii, Dk Ibrahim Mohamed na Katibu Mkuu wa wizara ya Afrika ya Mashariki, John Konchellah,walisema suala la kuzuiwa magari ni dogo lakini wanataka kufumuliwa mkataba wote.
"sisi Watanzania tulipinga,kwa kuwa ajenda yetu ilikuwa ni moja tu, kwanini magari ya Tanzania wamezuiwa kuingia uwanja wa ndege ya jomo Kenyatta na kama kuna matatizo basi ielezwe"alisema.
Alisema kutokana na mvutano huo, walishindwa kuelewana na hivyo kikao kuvunjika bila kufikia maridhiano.
Msimamo wa Tanzania.
Waziri Nyarandu alisema baada ya kushindikana vikao hivyo, msimamo wa serikali ya Tanzania, ni kuwataka mawakala wa makampuni ya Utalii na watalii kuwa wavumilivu wakati mgogoro huo unafanyiwa kazi.
"napenda kuchukuwa fursa hii, kuwaomba watanzani na watalii, kuwa wavumilivu na kutafuta njia mbadala za kutumia ili wasiendelee kuathirika na mgogoro huu"alisema.
Alisema serikali itafanya kila linalowezekana kutatua mgogoro huo,lakini watanzania waelewe kuwa Utalii wa Tanzania utajengwa na watanzania wenyewe.
Mwenyekiti wa chama cha mawakala wa utalii nchini(TATO) wilbard Chambulo ameitaka Serikali ya Tanzania na Kenya, kuendelea kukaa kumaliza mgogoro huo kwani una athari kwa nchi zote mbili katika sekta ya utalii.
Kuanzia desemba 22 mwaka jana, Serikali ya Kenya ilizuia magari ya watalii kuingia kuchukuwa watalii na kuwapeleka watalii hadi ndani ya uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta nchini Kenya hali ambayo imeathiri sana sekta ya utalii hapa nchini.
Post a Comment