RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu, ameibuka na
kusema, “vijembe vinavyorushwa na Ummy Mwalimu,” Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, “vitajibiwa na mimi mwenyewe,”
Akihutubia mkutano wa nusu mwaka wa mawakili nchini (AGM), kaka mkubwa
wa Lissu, Alute Mughwai Lissu, ameeleza kuwa ameelekezwa na mdogo wake
huyo, kutomjibu Ummy Mwalimu, badala yake kazi hiyo itafanywa na yeye
mwenyewe.
Alute ambaye ni wakili wa kujitegemea anayefanya shughuli zake mkoani
Arusha ameuambia mkutano huo, “nimeongea na Lissu leo saa nne asubuhi.
Amenielekeza kuwa familia isijibu hoja za waziri Ummy Mwalimu.”
Amesema, “kazi hiyo itafanywa na yeye mwenyewe mara akataporejea nchini
kutoka kwenye matibabu yake nje ya nchi. Ameahidi kuendeleza mapambano
ya kudai haki bila kuchoka.”
Wakili Alute amesema, Lissu amemueleza kuwa “hatarudi nyuma katika
harakati zake za kutetea haki na demokrasia nchini. Ameapa kupambana
hadi tone lake la mwisho.”
Kwa mujibu wa Alute, afya ya Lissu inaendelea vizuri na anawashukuru
madaktari wanaomtibu kwenye hospitali ya Nairobi alikolazwa. Amewataka
wajumbe wa mkutano huo kuendelea kumuombea.
Alute alikuwa akitoa salamu kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa TLS uliofanyika jana mjini Arusha.
Hii ni mara ya kwanza kwa Lissu kuzungumza kwa simu tokea
aliposhambuliwa kwa risasi na wanaoitwa na serikali, “watu
wasiofahamika,” ambako alimiminiwa rundo la risasi zilizolenga kuondoa
maisha yake.
Wakati huohuo, akiongea na Azam TV, Alute Lissu amesema kwamba familia
yake imemwandikia barua Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiomba uchunguzi
wa tukio la kushambuliwa mdogo wake ufanywa na vyombo kutoka nje ya
nchi, kwani katika mazingira ya sasa jeshi la polisi haliko tayari na
haliko huru kufanya uchunguzi huo kwani hadi sasa hakuna mtu yeyote
aliyekamatwa.
Kuhusiana na serikali kuitaka familia iandike barua ya kuomba matibabu
kwa ajili ya Tundu Lissu, kaka yake huyo alisema mdogo wake huyo ambaye
anatibiwa Nairobi amemwambia suala hilo atakuja kulizungumzia yeye akiwa
ni mbunge mwenye haki zote za kupewa matibabu kama wabunge wengine.
About Author
Journalist , Enterpreneur, Lecturer and Blogger. Email :ngoboleaa@gmail.com.
Advertisement
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment