PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: Wakina Tundu Lissu na TLS yao Waonywa Kuhusu Mgomo, Wajiandae Kujibu Mashitaka
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma na Jeshi la Polisi nchini, wamelionya Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili ...


Wakina Tundu Lissu na TLS yao Waonywa Kuhusu Mgomo, Wajiandae Kujibu Mashitaka
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma na Jeshi la Polisi nchini, wamelionya Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), kutoingilia vyombo vya uchunguzi na upelelezi, vinavyochunguza tukio la mlipuko, uliotokea kwenye ofi si za Kampuni ya Mawakili ya IMMMA usiku wa kuamkia juzi jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Profesa Juma alisema TLS hawana haki ya kutoa agizo kwa mawakili, kutohudhuria mahakamani na kwenye mabaraza mengine, kwa kuwa kila wakili ana mkataba binafsi na mteja wake.

Profesa Juma alisema uhuru wa mahakama ni pamoja na kuheshimu mamlaka nyingine za nchi zinapokuwa zinafanya kazi zake. Alisema kwa kuwa tukio la kulipuliwa kwa ofisi za Mawakili wa Immma ni tukio la kihalifu, hivyo wanasheria waiache Polisi na vyombo vingine vya upelelezi kufanya kazi yao.

“Kama kutatokea wateja watakaolalamika kuwa mawakili wao hawakufika mahakamani siku ya Jumanne na Jumatano, hatua za kisheria dhidi ya mawakili hao zitachukuliwa ikiwemo kuwapeleka kwenye Kamati ya Maadili ya Mawakili,” alieleza Kaimu Jaji Mkuu.

Kauli ya Jeshi la Polisi Kwa upande wao, Jeshi la Polisi limesema liachwe liendelee na kazi ya uchunguzi, badala ya kulihusisha na tukio hilo. Msemaji wa Jeshi hilo Makao Makuu, Kamishina Msaidizi Barnabas Mwakalukwa alisema Jeshi la Polisi ndicho chombo chenye mamlaka ya kufanya uchunguzi na hivyo kama kuna mtu yeyote mwenye taarifa yoyote kuhusu tukio hilo, anatakiwa kuzitoa polisi badala ya kuzungumza na vyombo vya habari.

Kauli hizo za Polisi na ya Kaimu Jaji Mkuu, zimekuja baada ya Rais wa TLS, Tundu Lissu kuwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa Baraza lao la Uongozi lina taarifa kuwa kikundi cha watu wenye silaha za moto, wakiwa wamevalia sare za Jeshi la Polisi, kiliwateka nyara walinzi binafsi wa Kampuni ya IMMMA na kuingia ndani ya eneo la ofisi hizo.

Lissu alidai watu hao baada ya kuingia ndani, walitega milipuko na madumu manne ya mafuta ya petroli katika maeneo kadhaa ya jengo la ofisi hizo. Alidai muda mfupi baadaye, milipuko hiyo ililipuka na kusababisha uharibifu mkubwa wa jengo la ofisi za IMMMA Advocates zilizoko Upanga pamoja na majengo jirani.

“Kama Lissu ana hizo taarifa alitakiwa azilete polisi kwa kuwa ndicho chombo cha uchunguzi badala ya kuzungumza na vyombo vya habari. Kazi ya polisi ni kufanya uchunguzi wa kina na ndiyo maana Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu alisema atatoa taarifa uchunguzi ukikamilika, hivyo watu wanapaswa kusubiri taarifa kamili, nje ya hapo tunakuwa tunafanya kazi nje ya utawala wa sheria,” alieleza Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mwakalukwa.

Mwakalukwa alivitaka vyombo vya habari, kuwatafuta walinzi hao ambao Lissu alidai walitekwa na watu wanaodhaniwa kuwa polisi ili waeleze tukio lilivyokuwa na ikibidi walinzi hao kutoa taarifa za kutekwa kwao polisi.

Alisema jambo hilo siyo dogo, hivyo watu waviache vyombo vya uchunguzi, viendelee na kazi yake kwani uchunguzi pekee ndiyo utakaobaini chanzo na wahusika. Ili kuonesha mshikamano, Baraza la Uongozi la TLS limewataka mawakili wote ambao ni wanachama wao nchini, wasuse kuhudhuria mahakamani na kwenye mabaraza ya aina zote kwa siku mbili, kesho na keshokutwa.

Lissu alidai kuwa lengo la kususa huko ni kupeleka ujumbe kwa jamii kuwa tukio lililotokea kwenye ofisi za IMMMA siyo dogo na hivyo wananchi ambao ni wateja wao hawana budi kwa siku hizo mbili kuungana nao kupinga jambo hilo. Alisema watamwandikia Kaimu Jaji Mkuu barua ya kumfahamisha kusudio lao la kutohudhuria mahakamani na kwenye mabaraza yote kwa siku hizo mbili.

“Tunatambua kuwa wateja wetu wataathirika, na hiyo ndiyo maana ya kufikisha ujumbe wetu kwa jamii. Tunafahamu kuwa wajibu wa kwanza wa wakili ni kumwakilisha mteja wake mahakamani, lakini kama mawakili hawako salama, uwezo wa kuwawakilisha wateja wao mahakamani unakuwa haupo,” alieleza Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki kupitia tiketi ya Chadema.

Aidha, alililaani tukio hilo na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama, kuchunguza kwa kina ili wahusika wajulikane na kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi yao. Alisema mawakili wa IMMMA wanapaswa kupatiwa ulinzi dhidi ya vitisho au vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wao au kuwazuia kutekeleza wajibu wao wa kitaaluma.

Kwa mujibu wa Lissu, Baraza la Uongozi la TLS litakutana na uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Kaimu Jaji Mkuu, Waziri wa Katiba na Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuzungumzia vitendo vya kushambuliwa mawikili wakiwa wanatekeleza majukumu yao ya kisheria.

Naye Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Omar Shaaban alisema wanaungana na TLS kulaani shambulio hilo kwenye ofisi za IMMMA. Alisema IMMMA wana tawi lao Zanzibar na ndiyo maana aliamua kuungana na TLS kulaani tukio hilo.

Usiku wa kuamkia juzi kulitokea milipuko kwenye ofisi za IMMMA Advocates zilizopo Upanga katika Barabara ya Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam na kusababisha uharibifu. Imeelezwa kuwa vyombo vya uchunguzi vinaendelea na uchunguzi kubaini chanzo na wahusika wa tukio hilo.

Chanzo: Habari leo

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top