Katika ripoti ya pili ya Kamati ya kutathmini mchanga wa madini Mbunge
wa Bariadi, Andrew Chenge ametajwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo kuwa
alikuwa na mchango mkubwa wa kulisababishia Taifa hasara kubwa kutokana
na kuandaa au kusaini mkataba mbovu wa madini unaoyaruhusu makampuni ya
uchimbani kusafirisha mchanga huo kwenda nje ya nchi pamoja na kukubali
viwango vidogo vya mrabaha kwa Taifa katika sekta ya madini.
Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa kwa Rais na Mwenyekiti wa kamati
hiyo ni pamoja na kuwashughulikia viongozi na watendaji wote wa Serikali
walioshiriki kusababisha hasara hii kwa zaidi ya miaka 19.
Rais Dkt. Magufuli akiongelea pendekezo hili aliagiza vyombo vinavyohusika viwaite watu wote waliotajwa ili wahojiwe.
Baada ya kauli hiyo ya Rais, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania amesema kuwa Chenge ataendelea kuwa Mwenyekiti wa Bunge mpaka
atakapoitwa na kuhojiwa kuhusu mchanga wa madini (makinikia). Spika
Ndugai alisema hakuna kanuni inayomzuia Chenge kuendelea kuwa Mwenyekiti
wa Bunge kwa sasa.
“Kwa sasa hapana. Ataachia nafasi hiyo atakapoitwa kuhojiwa; akishathibitika ndio atatoka kwenye nafasi ya Uenyekiti,” alisema.
Utaratibu unaeleza kwamba Ofisi ya Spika ikishapata taarifa ya Mbunge au
kiongozi fulani wa Bunge kuhitajiwa na chombo cha dola na Spika akatoa
ruhusa hiyo, Mbunge huyo ataachia madaraka yake na kubaki na ubunge tu.
Mwenyekiti wa kamati ya pili ya kuchunguza hasara iliyoletwa na
kusafirisha mchanga wa madini, Profesa Nehemiah Osoro alisema kuwa
wakati Taifa linapitisha Sheria na mikataba ya hovyo, Mwanasheria Mkuu
wa Serikali alikuwa ni Andrew Chenge.
Post a Comment