Waziri wa Katiba na
Sheria wa Tanzania, Profesa Paramagamba Kabudi (kulia) na Waziri wa Nishati wa
Uganda, Bi. Irene Muloni (kushoto) wakionesha Mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa
Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania,
baada ya kuusaini, tukio lililofanyika leo katika Hoteli ya Serena, Kampala,
Uganda.
Na Benny
Mwaipaja, WFM
Serikali za
Tanzania na Uganda zimetiliana saini Mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa Bomba la
Mafuta Ghafi la kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania lenye
urefu wa Kilometa 1,443, uliokadiriwa kugharimu zaidi ya Dola bilioni 3 nukta 55,
mjini Kampala Uganda, leo.
Mkataba huo
umesainiwa na Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania, Profesa Paramagamba
Kabudi na Waziri wa Nishati wa Uganda, Mhandisi Irene Muloni.
Tukio hilo
limekuja siku chache baada ya Marais wa Nchi hizo mbili, Dkt. John Pombe
Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni, kutia saini tamko
la pamoja la kukamilika kwa majadiliano ya vipengele vya mkataba, Ikulu Jijini
Dar es salaam.
Hafla
ya kutia saini Mkataba huo iliyofanyika katika Hoteli ya Serena, Jijini Kampala,
Uganda imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nchi zote mbili wakiwemo
Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wanasheria Wakuu wa Serikali, Wakurugenzi na Viongozi
wa taasisi mbalimbali zinazohusika katika mradi huo.
Mradi
wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi Tanga Tanzania, unatarajia
kusisimua uchumi wa nchi hizo mbili na katika mchakato wa ujenzi wake zaidi ya
watu 10,000 wanatarajiwa kunufaika na ajira.
Hivi
Karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
aliuelezea mradi huo kuwa ni mkubwa kwakuwa Uganda imegundua shehena kubwa ya
mafuta katika eneo la Hoima kiasi cha mapipa bilioni 6 na laki 5 na kwamba
Tanzania inatarajia pia kupata mafuta kule ziwa Tanganyika na ziwa Eyasi, ambayo
yatapitishwa katika bomba hilo hilo. | | |
Post a Comment