KIKAO cha kwanza cha Bunge la 11 jana kilisimama kwa dakika 10 baada ya
wabunge bila kujali itikadi zao za kisiasa kusimama huku wakipiga meza
zao kumshangilia Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ambaye alikwenda bungeni
kushuhudia mkewe, Mama Salma akila kiapo cha ubunge.
“Tumekukumbuka, ingia ndani utusalimie, njoo huku ndani utusalimie.” Ni
baadhi ya kauli zilizotolewa na wabunge hao baada ya Spika Job Ndugai
kumtambulisha Rais mstaafu aliyekuwa ameketi kwenye ukumbi wa wageni wa
Spika, muda mfupi baada ya Salma Kikwete kula kiapo.
Wakati wabunge hao wakimshangilia, Rais Kikwete aliyeambatana na mmoja
wa watoto wake, Ally, alikuwa akitabasamu na kuwapungia mkono
wawakilishi hao wa wananchi, ambao baadhi yao waliwasha vipaza sauti na
kutoa hisia zao kwa Rais huyo wa Awamu ya Nne aliyemaliza muhula wa pili
wa utawala wake Novemba 2015.
Wabunge
Wabunge waliozungumza na gazeti hili baada ya kikao hicho kuahirishwa,
walitaja sababu za kumshangilia Kikwete ikiwamo wakati wa utawala wake
uchumi kuwa mzuri, kutokuwepo kwa demokrasia katika utawala wa Serikali
ya Awamu ya Tano na kuminywa kwa uhuru katika masuala mbalimbali.
“Haijawahi kutokea tangu niwe Mbunge. Hiki ni kipindi changu cha nne kwa
mgeni kushangiliwa namna hii,” alisema Ndugai wakati shangwe za wabunge
hao zikiendelea.
Wakati shangwe hizo zikiendelea, Ndugai aliwataka wabunge kusimama na
kumshangilia Rais huyo mstaafu kwa maelezo kuwa kufanya hivyo ni kumpa
heshima kubwa, ombi ambalo lilitekelezwa bila vikwazo na wabunge hao,
hata mawaziri.
‘’Kwa makofi hayo sasa naomba mumpe heshima mpigieni makofi mkiwa
mmesimama,’’ alisema Ndugai ambaye alichombeza: “Inawezekana waliommiss
(waliomkumbuka) nao wapo,” kuonekana kurejea tungo za wimbo uliozua
utata unaoitwa ‘Wapo’ ulioimbwa na msanii Emmanuel Elibariki ‘Nay wa
Mitego’.
Wimbo wa msanii huyo unaokosoa mambo mbalimbali ulipigwa marufuku na
Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), kabla ya Rais John Magufuli kutoa
kauli ya kutaka uendelee kupigwa sambamba na msanii huyo kuachwa huru,
ikiwa ni saa 24 tangu akamatwe na polisi kutokana na mashairi ya wimbo
huo.
Kauli ya JK
Wakati hayo yakiendelea, Kikwete alizungumzia ujio wake bungeni na
kubainisha kuwa sasa ni zamu yake kumuunga mkono mkewe kwa sababu wakati
akiwa Rais, Mama Salma alimuunga mkono.
“Leo asubuhi nimeshuhudia kiapo cha mke wangu, Mheshimiwa Salma Kikwete
kuwa mbunge wa kuteuliwa bungeni mjini Dodoma. Ni zamu yangu kumuunga
mkono,” alinukuliwa Kikwete katika akaunti yake ya Twitter.
Mama Salma ambaye ni Mwenyekiti wa WAMA, alipotakiwa kueleza sababu za
Rais Kikwete kushangiliwa, alisema: “Inaashiria kuwa Tanzania ni moja.
“Nashukuru wabunge kwa kunipokea vizuri, naamini tutafanya kazi nzuri
kwa kushirikiana, shangwe na vigelegele vya leo (jana) vinaonesha
Tanzania ni moja kwa kuwa zimetoka pande zote.”
Kauli za wabunge
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) alisema shangwe
hizo zinaashiria kuwa wabunge wamewakilisha wananchi wao kutoa hisia
zao kwa Serikali ya Awamu ya Tano, ijue kwamba watu wanakumbuka
walikotoka.
‘’Ile ilikuwa salamu kwa Magufuli, tunamkumbuka Kikwete, ambaye aliacha
uchumi mzuri, mishahara ilikuwa inalipwa kwa wakati, watumishi walikuwa
wanapanda vyeo, lakini sasa mambo yamekuwa ya hovyo kiwango chake
aliyemwachia amekishusha,” alisema Msigwa.
Alisema Magufuli amedidimiza demokrasia, hafuati taratibu za bajeti
ananunua ndege bila Bunge kuidhinisha, amehamia Dodoma bila Bunge
kuidhinisha, hivyo ni lazima Bunge linalobanwa lioneshe hisia.
“Tumemkumbuka sana pamoja na kwamba hakuwa mzuri kihivyo, lakini
ukimlinganisha na Magufuli anamwacha mbali mno, tulikuwa tunamtumia
salamu kwamba Magufuli Watanzania waliingia ‘choo cha kike’, mambo ya
hovyo sasa,” alisema Msigwa.
Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) alisema Kikwete
alishangiliwa kutokana na namna ya uongozi wake, hivyo Watanzania wengi
wamemkumbuka, kwani alikuwa Rais mchangamfu kwa watu wake, alipenda
kupokea ushauri hata kama anatukanwa.
“Tuna kila sababu ya kumkumbuka Kikwete na kumshangilia, ndiyo maana
mliona pande zote zilishangilia, hivi ndivyo wananchi walivyo, kwani
sisi tunawakilisha wananchi na tulichoonesha ndizo hisia za Watanzania
wengi,” alisema Bulaya.
Alieleza kipindi cha Kikwete vyama vya siasa vilikuwa na uhuru wa
kufanya kazi zao kwa mujibu wa sharia, alikuwa anapambana na ufisadi kwa
kuruhusu watu kuainisha maeneo yenye ubadhirifu, lakini sasa kila kitu
kimeminywa
Alisema: “Kikwete tunamkumbuka kwa kweli, japokuwa hakuwa mkamilifu kwa
asilimia 100 lakini ukimlinganisha na Magufuli hata ukiwaweka hapo
Watanzania wengi watamchangua yeye, tunakumbuka uhuru wa kujieleza,
uhuru wa Bunge na vyombo vya habari, uchumi unayumba yaani hakuna
kuzuri.
“Napata shida mno mtu akisema Serikali inapambana na ufisadi wakati
haitaki wananchi waeleze maeneo yenye ubadhirifu, akitokea mtu kueleza
anaonekana adui wa Serikali, Kikwete alijitahidi kuacha watu wamwoneshe
mafisadi na aliwawajibisha kupitia Bunge.”
Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza (Chadema) alisema kitendo cha
kumshangilia Kikwete kina tafsiri nyingi, lakini Serikali inataka
kuendesha nchi kibabe, japokuwa wananchi wanapinga.
Kikwete hakuingilia Bunge, aliliacha lifanye kazi yake, hakuwa anasimama
kutetea viongozi wanapotakiwa kuwajibishwa kama inavyotokea sasa katika
Serikali.
“Viongozi awamu hii wakitaka kuwajibishwa Rais anasimama anatetea, Rais
amekuwa akidhalilisha Bunge, Kikwete hakuyafanya hayo, aliruhusu
demokrasia na uhuru utawale, sasa tunarudishwa nyuma miaka 50, hivyo
wabunge walimshangilia kuonesha hisia zao kwake, japo hakuwa mkamilifu
lakini alifanya mengi mazuri,” alisema Peneza.
Mbunge wa Urambo, Magreth Sitta (CCM) alisema wabunge wamemkumbuka
Kikwete kwa kazi nzuri aliyofanya wakati akiwa Rais lakini pia
walishangilia kwa kuwa wengi hawajamwona siku nyingi.
“Nimemkumbuka kwa kutujengea barabara inayounganisha Tabora na mikoa
mingine hali inayotusaidia kusafiri kirahisi lakini pia wabunge wengine
huenda hawajamwona kiongozi wao aliyeongoza kwa miaka 10 hivi karibuni,
ndiyo maana walimshangilia,” alisema Sitta
Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), alisema Kikwete anakumbukwa
kwa mambo mengi mazuri, ukiwamo uhuru kwa vyama vya siasa kufanya kazi
zao na kukaa kuzungumza nao.
Bunge lilikuwa huru kufanya kazi zake tofauti na sasa, ambapo linaminywa
kufanya kazi zake, kwani kamati nyingi zinapangiwa kazi za kufanya
haziko huru ndiyo maana baadhi ya wenyeviti wamejiuzulu.
“Kikwete alishangiliwa kwa mapenzi ya dhati na watu wamekumbuka uhuru
ambao alikuwa anautoa na sasa umeminywa, biashara haziendi, uchumi
unadidimia, wabunge hawafanyi kazi zao kama inavyotakiwa vitu vingi
havieleweki,” alisema Waitara na kuongeza:
“Serikali ya Kikwete ilikuwa haina ubaguzi, mtu yeyote hata kama ni
rafiki yake akiharibu anatolewa, lakini Serikali hii kuna mtu ameghushi
vyeti anatumia jina la mtu mwingine, lakini Magufuli anaambiwa na
anasimama kumtetea hadharani, ni lazima watu tumkumbuke Kikwete.”
Post a Comment