Ikiwa ni takriban siku 40 baada ya kikao kizito kilichofanyika Ikulu ya
Chamwino mjini Dodoma, wabunge wa CCM watakuwa na mkutano mwingine
keshokutwa ulioitishwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli.
Hata hivyo, wabunge hawajaelezwa mahali wala muda utakaofanyika mkutano huo, kwa ahadi kuwa watataarifiwa baadaye.
Pia , wabunge hao hawajaelezwa ajenda za kikao hicho ambacho kwa kawaida
huwa cha siri na ambacho hutumika kuweka misimamo ya chama katika
masuala yanayojadiliwa au yanayotarajiwa kujadiliwa bungeni.
Katibu wa wabunge hao, Jasson Rweikiza ndiye aliyetuma ujumbe huo mfupi
wa simu kwa wabunge ambao baadhi yao wameithibitishia Mwananchi suala
hilo.
Ujumbe huo umemtaka kila mbunge awepo na hata wale waliosafiri, wajitahidi kurudi Dodoma kuhudhuria kikao hicho.
Alipohojiwa na gazeti hili jana, Rweikiza alisema Rais anaruhusiwa
kuzungumza na wabunge wake muda wowote kwa hiyo hilo lisiwe nongwa
linapotokea kwa CCM.
“Kwani (mwenyekiti wa Chadema, Freeman) Mbowe akiwataka wabunge wake
inakuwa nongwa? Yeye ni mwenyekiti. Wabunge ni watu anaofanya nao kazi
pamoja, hivyo kuwaita ili kuteta nao kujadili kazi isiwe nongwa,”
alisema Rweikiza.
Rweikiza alisema Magufuli kama mwenyekiti wa CCM anaruhusiwa kuwaita
wabunge na kukaa nao, kuongea au kuteta jambo lolote linalohusu
mustakabali wa chama hicho.
“Mkumbuke yeye ni mwenyekiti wa chama tawala,” alisema.
Viongozi wa juu wa CCM na Serikali wanatarajiwa kuwepo katika kikao
hicho, hasa kutokana na ukweli kuwa siku inayofuata itakuwa ni sherehe
za Muungano ambazo mwaka huu zinafanyika mjini hapa.
Kwa maana hiyo, Rais Magufuli, Dk Ali Mohamed Shein (Rais wa Zanzibar),
Samia Suluhu Hassan (Makamu wa Rais) na Phillip Mangula (makamu
mwenyekiti CCM) na Abdulrahman Kinana (katibu mkuu wa CCM) wanatarajiwa
kuhudhuria kikao hicho.
Vigogo hao wataungana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye yupo mjini hapa kuongoza shughuli za Serikali bungeni.
Vikao hivyo huwa vinaongozwa na Waziri Mkuu katika siku za kawaida za
mikutano ya Bunge kwa kuwa mtendaji huyo mkuu wa Serikali huwa Dodoma
kwa ajili ya mikutano ya Bunge.
Mara ya mwisho kikao baina ya Rais na wabunge hapo kilifanyika Machi 12,
mwaka huu na Rais alitumia muda mwingi wa hotuba yake kuwaelekeza
wabunge jinsi ya kuenenda, ikiwa ni pamoja na kuwaonya wasimpinge Waziri
Mkuu.
Maelekezo ya Rais
Katika kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na Kinana na Mangula,
kiongozi huyo wa nchi aliweka bayana kuwa iwapo wabunge watampigia kura
ya kutokuwa na imani naye (Waziri Mkuu Majaliwa), atamrudisha kwenye
chombo hicho na iwapo watamkataa tena, atalivunja Bunge.
Rais aliwaambia watunga sheria hao kutoka CCM kuwa amepata taarifa
kwamba wapo baadhi yao wanaotishia kuanzisha hoja ya kutaka Majaliwa
apigiwe kura ya kutokuwa na imani naye na kuwaambia wenye lengo hilo
hawatafanikiwa kwa kuwa wakithubutu kufanya hivyo, atapeleka tena jina
lake na wakirudia, atalivunja Bunge ili wote warudi katika uchaguzi.
Mbali ya kumkingia kifua Majaliwa, mwenyekiti huyo wa CCM pia aliwaonya
wabunge dhidi ya vitendo vya kushirikiana na wapinzani kuishambulia
Serikali, akitoa mfano wa mbunge wa chama tawala aliyemgawia muda wake
wa kuchangia hoja mbunge wa upinzani.
Kwa kauli hiyo, alikuwa akirejea kitendo cha mbunge wa CCM, Boniface
Getere kumpa dakika tano mbunge wa Serengeti (Chadema), Marwa Ryoba
wakati wa kuchangia taarifa ya Kamati za Bunge za Ardhi, Maliasili,
Kilimo na Utalii.
Pia alieleza kukerwa na wabunge wa CCM wanaofifisha vita dhidi ya dawa
za kulevya na mmoja akimtuhumu kutoa siri za chama kwa upinzani.
Rais Magufuli pia alieleza kuwa yeye ndiye aliyeamua kusitisha matangazo
ya moja kwa moja ya televisheni kwa baadhi ya shughuli za Bunge.
Pia, mwenyekiti huyo wa CCM alionya kitendo cha baadhi ya wabunge wa
chama hicho waliotaka kumtembelea gerezani Arusha, mbunge wa Chadema,
Godlbess Lema kwa madai kuwa kitendo hicho ilikuwa ni sawa na usaliti
kwa chama.
Katika kikao hicho, wabunge pia walimweleza Rais kuhusu uhusiano wao na
baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya, wakisema si mzuri na bado suala hilo
limeendelea kujitokeza katika mijadala ya Bunge la Bajeti.
Baada ya kuwasikiliza, Rais Magufuli alianza kuwapa taarifa za mafanikio
ya Serikali yake pamoja na mipango kabambe katika kutekeleza ilani ya
uchaguzi ya CCM, akiwataka waiunge mkono Serikali katika maeneo yao huku
suala la ujenzi wa reli pana, ambao tayari umezinduliwa, likipewa
kipaumbele zaidi.
Kikao moto cha Bunge
Kikao cha keshokutwa kinakuja wakati Bunge likiwa limetawaliwa na
mijadala inayoonyesha Serikali haijafanya kazi yake vizuri baada ya
hotuba tatu za bajeti kusomwa.
Bajeti hizo ni ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo ilitawaliwa na
majadiliano kuhusu vitendo vya utekaji, uvamizi na kuihusisha Idara ya
Usalama wa Taifa na matukio hayo.
Suala la kutekwa kwa msanii Roma Mkatoliki, kitendo cha mteule wa Rais
kuvamia studio za televisheni za Clouds Media, kutishiwa bastola kwa
mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na kutoweka kwa kada wa Chadema, Ben
Saanane yalitawala mijadala ya hotuba hiyo.
Bajeti nyingine ni za Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, zilizojadiliwa kwa pamoja na kutawaliwa pia na hoja za
utekaji na pia vitendo vya unyanyasaji unaofanywa na wakuu wa wilaya na
mikoa.
Mawaziri pekee watetea
Tofauti na inavyokuwa wakati wa bajeti hizo, ni wabunge wachache wa CCM
waliosimama au kuomba mwongozo wakati wapinzani walipokuwa
wakiishambulia Serikali.
Badala yake, mawaziri watatu; George Simbachawene (Tamisemi), Angela
Kairuki (Utawala Bora) na Jenista Mhagama (Bunge) ndio waliosimama mara
kwa mara kutoa taarifa au kuomba mwongozo.
Hoja dhidi ya Serikali zinazotolewa na wabunge wa upinzani pamoja na wa
CCM zinaweza kuchukua nafasi kubwa katika kikao cha keshokutwa, hasa
ikizingatiwa kuwa shughuli nyingi za maendeleo hazikupata fedha za
kutosha kama ilivyopangwa katika bajeti iliyopita.
Hadi wiki mbili zilizopita, miradi ya maendeleo ilikuwa imepewa asilimia
zisizozidi 40 ya fedha zilizotengwa. Bajeti ya mwaka 2016/17 ilitenga
asilimia 40 ya fedha zake kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Bajeti hiyo ya mwaka 2016/17 ilikuwa ya Sh29.5 trilioni na Sh11.8 trilioni zilitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Wabunge wamekuwa wakiilalamikia Serikali kuwa fedha zinazotolewa kwa
ajili ya shughuli mbalimbali haziendani na kiwango kilichoidhinishwa na
Bunge hilo na kusababisha nakisi ya zaidi ya asilimia 50 katika miradi
ya maendeleo.
Hali ya uchumi inaweza kuibua mijadala mikali katika hotuba za bajeti za
wizara zinazofuata, kutokana na malalamiko kuzidi kuongezeka, hasa
sekta binafsi ambayo wadau wanadai kuwa mazingira ya biashara hayajakuwa
rafiki.
Suala jingine ambalo limekuwa linazungumzwa na wabunge kutoka vyama
vyote ni uhakiki wa vyeti vya mteule mmoja wa rais anayedaiwa kufeli
kidato cha nne na kutumia vyeti vya mtu mwingine ambavyo vimeghushiwa
jina ili vilingane na jina lake la sasa.
Suala hilo pia lilihojiwa na wabunge wa CCM katika kikao chao cha kwanza
cha ndaniokabla ya mkutano wa bajeti kilichoongozwa na Waziri Mkuu.
Vilevile, zimekuwapo taarifa za wabunge kutaka masilahi yao yaongezwe,
lakini hoja zao zimekuwa zikigonga mwamba na taarifa za ndani zinasema
safari hii huenda kilio chao kikaongezeka.
Bunge, ambalo mwaka jana lilirejesha salio la Sh6.5 bilioni, mwaka huu
limejikuta na nakisi ya Sh8.5 bilioni ambazo wabunge wameeleza hofu kama
zitaweza kukifikia chombo hicho kabla ya kumaliza shughuli zake za
bajeti.
Post a Comment