Na mwandishi wetu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na
Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa mapambano ya
kukabiliana na tatizo la Dawa za Kulevya ni jukumu la kila mwananchi
na wala sio suala la kuiachia Serikali peke yake.
Ameyasema hayo
bungeni jana wakati akijibu hoja za wabunge waliochangia juu ya Taarifa ya
Kamati ya Kudumu ya UKIMWI na Dawa za Kulevya iliyoibua maswali kwa Serikali
kuendelea kupambana na wanaoshiriki katika biashara haramu ya dawa za kulevya
nchini.
Waziri Mhagama alieleza kuwa dhamira ya Serikali ni
kuhakikisha jamii yote kwa ujumla inakuwa mstari wa mbele katika
kutokomeza tatizo hili linalowaathiri vijana kwa kiasi kikubwa.
“Mapambano haya ni yetu sote, yasichague mtu na iwe
agenda ya Kitaifa inayowahusu Watanzania wote na ikumbukwe kuwa tatizo la dawa
za kulevya lina historia tangu mwaka 1990 na Serikali imekuwa ikipambana kwa
jitihada nyingi hivyo niombe watanzania wote tuunge mkono vita hii ili kumaliza
kabisa tatizo hili”. Alisema Waziri
Aliongezea kuwa, dhamira hii ya Serikali ilianza kuonekana
tangu kuwepo kwa sheria namba 9 ya mwaka 1995 hadi ilipofanyiwa marekebisho
mwaka 2014 na kubaini kuwa asilimia 56 ya nguvu kazi ya vijana ndiyo
imeathiriwa na tatizo la dawa za kulevya.
Aidha pamoja na
mapambano hayo, tayari sheria namba 5 ya mwaka 2015 na miundo ya mapambano
inaelekeza namna ya kupambana na vita dhidi ya dawa za kulevya.
Kwa upande wake
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe alieleza Bunge kuwa ziwepo
jitihada za makusudi za kuunga mkono mapambano haya yawe ya Watanzania wote kwa
kutoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam Mhe.Paul Makonda kwa namna alivyojidhatiti kupambana na wote
wanaoshiriki katika biashara hizi za dawa ya kulevya.
“Nieleza wazi kuwa jitihada za Serikali pekee hazitoshi ni lazima jamii iunge mkono kwa kuwafichua wanaojihusisha na mtandao huu wa Dawa za Kulevya na Mhe.Paul Makonda nampongeza kwa kuthubutu kuingia kikamilifu katika vita hii”.Alisema Mwakyembe
Alimalizia kwa kueleza kuwa, kinachohitajika ni dhamira ya dhati na si fedha, hivyo Serikali imedhamiria kukomesha kabisa tatizo hili nchini.
Post a Comment