KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad,
amewafunda wafuasi wake na kuwataka kuepuka fitna ambazo zitasababisha
kukigawa chama chao.
Maalim Seif aliyaeleza hayo katika Kijiji cha Matele Jimbo la Chambani
Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba alipoweka jiwe la msingi la tawi
la chama hicho.
Alieleza kuwa wapo baadhi ya watu waliokuwa wabunge wa chama hicho,
lakini baada ya kukataliwa na wanachama majimboni kwa sasa wamenuna na
kuanzisha migogoro ndani ya chama hicho.
“Walidhani vile vyeo ni mali yao, sasa wamesahau kuwa wenye mamlaka ya
kuteua mgombea ni wanachama, wanaanza kutaka kuharibu, lakini waambieni
watajiharibu wenyewe na siyo chama hiki,” alieleza Maalim Seif.
Aliwaambia wanachama hao kuwa wakati huu ni vyema wakawa na umoja na
kufanya kazi kwa pamoja katika chama ili kufikia malengo waliojiwekea.
“Wako watu wanajiita Mungiki, ambao wana nia mbaya na chama hiki, lakini
tunawaambia nia zao zitawarejea wenyewe,” alieleza Maalim Seif ambaye
ni Makamu wa Kwanza wa rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
(SMZ).
Alieleza kuwa kila mnafiki katika chama hicho atadhihirika na atatoka na kukiacha chama kikiendelea.
“Kwa hiyo ili kuwadhibiti hawa, ni vyema tukazidisha umadhubuti wa umoja
wetu na kuwafagia wote ili chama kizidi kuwatia joto CCM na Seriklai
zake,” alisema.
Alisema kuna watu kwa tamaa zao wamekubali kupokea hongo na kuanza kukihujumu chama chao huku akisema kuwa wamechelewa.
Maalim Seif alieleza kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa siku nyingi
wamekuwa wakikiandama CUF kutokana na kuwa malengo ya kuwakomboa
Wazanzibar na Watanzania, lakini wameshindwa kutokana na uimara
walionao.
Aidha, alisema kuwa CCM wakiona chama cha upinzani kina dalili ya
kuwaondoa madarakani, wanakifanyia kila aina ya hujuma ili kukimaliza na
kudai kuwa hawana tena nguvu hiyo dhidi ya CUF.
“Wanatia migogoro katika vyama vya upinzani na kuwahujumu viongozi wake
baada ya kuona wakati wowote madaraka yatawatoka,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Salim Biman, alielza
kuwa wasaliti wote ambao wamekisaliti chama hicho ni wale aliodai
hawakuwa na machungu ya kuwakomboa Watanzania ambao tayari wameshachagua
mabadiliko.
Aliwataka wanachama hao kutowapa nafasi wale aliodai mamluki kwani hawana nia nzuri kwa chama chao.
“Huu msukosuko unaopita kwenye chama chetu akipenda Mwenyezi Mungu
utakwisha, licha ya kupata baraka za SMZ na SMT,” alieleza Biman.
Wakati huo huo Maalim Seif alizindua magari maalum kwa ajili ya kutoa
huduma kwa Jimbo la Chambani ambayo yalitolewa na Mbunge wa jimbo hilo,
Yusouf Salim Husein.
Post a Comment