PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: Rais wa Uturuki Kutua Nchini Kesho Akiambatana na Ujumbe wa Watu 150...!!!
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
RAIS wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili Tanzania kuanzia kesho akiwa na ujum...

RAIS wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili Tanzania kuanzia kesho akiwa na ujumbe wa watu 150.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa, Rais huyo ambaye ataambatana na mke wake, atawasili nchini kwa mwaliko wa Rais John Magufuli.

Taarifa hiyo imesema kuwa wajumbe watakaokuwa kwenye ziara hiyo ni pamoja na mawaziri, wabunge, maofisa kutoka serikalini na wafanyabiashara.

Aidha, taarifa hiyo imesema Rais huyo atawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kesho jioni na atapokewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

“Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza uhusiano mzuri uliopo baina ya Uturuki na Tanzania ‎na kupanua fursa za uwekezaji hususan katika maeneo ya biashara na uwekezaji,” imesema taarifa.

Kadhalika, taarifa hiyo ilisema wakati wa ziara hiyo, Rais Erdogan atakutana na Rais Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande zote mbili na baadaye watashuhudia utiaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali. 

“Jumatatu (Januari 23) kutakuwa na Kongamano la Biashara kati ya Uturuki na Tanzania litakalowakutanisha wafanyabiashara kutoka nchi hizi mbili. Kongamano hilo litahutubiwa na viongozi wa Tanzania na Uturuki,” ilisema taarifa.

Pia taarifa hiyo imeeleza kuwa, Rais Erdogan na ujumbe wake watashiriki dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Ikulu kwa heshima ya Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Serikali ya Tanzania imefungua ubalozi wake nchini Uturuki na jana Rais Magufuli alimwapisha Prof. Elizabeth Kiondo kuwa balozi wake.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top