JENGO la Amani na Usalama lililopo Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU)
mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, limetangazwa rasmi kuwa litaitwa
Mwalimu Julius Nyerere.
Jengo hilo limepewa jina hilo rasmi katika hafla ya chakula cha mchana,
iliyofanyika jana na kuhudhuriwa na Rais John Magufuli pamoja na marais
mbalimbali wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, Antonio Guterres, mawaziri na mabalozi mbalimbali
wanaohudhuria Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa
Afrika unaoendelea mjini humo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, akizungumza katika hafla hiyo, Rais
Magufuli aliwashukuru viongozi wote wa AU kwa kuamua jengo hilo liitwe
jina la Mwalimu Julius Nyerere ikiwa ni kutambua mchango wake katika
kupigania amani na usalama na alibainisha kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa
Mwafrika halisi na kiongozi mahiri na shupavu.
“Na kwa hakika naweza kusema kuwa alikuwa mmoja wa viongozi bora kabisa
ambaye amewahi kutokea katika Bara letu, katika maisha yake yote Mwalimu
Nyerere alipambana ili kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Afrika,
alikuwa mmoja wa waanzilishi wa umoja huu, sisi Watanzania kwa hakika
tunajivunia sana Mwalimu Nyerere kuwa Baba wa Taifa,” alisema Dk
Magufuli.
Dk Magufuli aliongeza kuwa Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa katika
kupambana na ubaguzi na unyonyaji wa kila aina, alisaidia ukombozi wa
nchi nyingi za Afrika, na hata alipong’atuka katika hatamu za uongozi wa
Taifa la Tanzania aliendelea kutoa mchango wake kupigania amani katika
nchi za Afrika.
“Wito wangu kwenu, waheshimiwa viongozi ni kwamba, sambamba na kumuenzi
Mwalimu Nyerere kwa jengo hili, itakuwa ni jambo jema zaidi kama
tutajitahidi kufuata nyayo zake pamoja na kuishi maisha ya viongozi
wengine hodari wa Bara hili wakiwemo Kwame Nkrumah, Ahmed Ben Bella,
Sekou Toure, Gamal Abdel Nasser na bila kusahau shujaa wetu mwingine
Nelson Mandela,” alisisitiza Rais Magufuli.
Post a Comment