Rais wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli ameagiza muwekezaji wa kiwanda cha nyama cha Triple S
mjini Shinyanga aondolewe haraka, na atafutwe muwekezaji mwingine
anayeweza kufanya kazi hiyo kwa wakati.
Rais Magufuli akiwahutubia wakazi wa Shinyanga katika kilele cha maadhimisho ya sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika katika uwanja wa Kambarage mkoani humo
Rais Magufuli amefikia hatua hiyo
kutokana na muwekezaji huyo kuchelewa kuanza shughuli za usindikaji wa
nyama licha ya kupewa kibali kwa kipindi kirefu cha zaidi ya miaka 10,
huku wafugaji wakiwa hawana mahala pa kuuza mifugo yao.
Ametangaza uamuzi huo leo katika mkutano
wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kambarage mjini
Shinyanga, ambao licha ya kuwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani
Shinyanga, pia ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi
Matukufu ya Zanzibar ambayo kwa mwaka huu sherehe zake zimefanyika
katika pande zote mbili za muungano.
Amesema muwekezaji huyo amepewa kibali
cha kujenga na kuendesha kiwanda cha nyama kwa kipindi kirefu tangu yeye
akiwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, hadi akahamishiwa Wizara
ya Ujenzi na sasa ni Rais, lakini hakuna kilichofanyika.
Kutokana na hali hiyo ameutaka uongozi wa mkoa huo, Wizara ya Viwanda
pamoja na Wizara ya Kilimo,Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi kufuta mradi wa
kiwanda cha kusindika minofu ya nyama cha Triple S kutokana na
mwekezaji huyo kukaa muda mrefu bila kiwanda hicho kufanyakazi.
Rais Magufuli akipunga mkono kuwasalimia
wananchi wa Shinyanga waliofika katika uwanja wa mpira wa Kambarage
katika kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi ya
Zanzibar mkoani humo Januari 12,2017
"Viongozi wa mkoa, idara, taasisi husika
za serikali na wizara futeni huu mradi wa kiwanda cha nyama cha Triple
S, haiwezekeni tusubiri mtu miaka 10 huku wafugaji wanahangaika na
mifugo yao, ndiyo maana wengine wanahamahama, sasa wakihama mnawaambia
wauze ng'ombe, sasa watauza wapi kama kiwanda hakuna. Kuna wakati
tulitaka kumfuta huyu muwekezaji wa Triple S, wanasiasa wakamtetea,
nadhani sasa hawatamtetea tena". Amesema Rais Magufuli.
Mbali na agizo hilo, amewataka watendaji
katika mamlaka husika za serikali kutowakwamisha viongozi hao kuweka
muwekezaji mwingine, na kusema "Kama kuna mtu atawakwamisha, niambieni
mimi nitamkwamua"
Rais Magufuli pia ameuagiza uongozi wa mkoa wa Shinyanga kufuta
leseni ya Mwekezaji aliyetaka kuchukua machimbo ya wafanyabiashara
wadogowadogo zaidi ya 15,000 katika eneo la Mwakitoliyo Wilaya ya
Shinyanga vijijini.
Hayo ni maamuzi ya pili katika ziara
hiyo dhidi ya wawekezaji, ambapo jana akiwa mkoani Simiyu alimzuia
muwekezaji wa uchimbaji wa madini ya Nikel kuendelea na uchimbaji ili
eneo hilo pawekwe tanki ya maji kama ilivyokuwa imepangwa awali, na
kusema kuwa muwekezaji huyo siyo muhimu zaidi ya wananchi maelfu
wanaoteseka kwa kukosa huduma ya maji.
Post a Comment