Msanii wa mashairi na kughani
Mrisho Mpoto ametoa somo kwa vijana wa watanzania kwa kuwapa njia
mbalimbali ambazo zinaweza kuwafanya kujikwamua kiuchumi endapo
watazitumia kuanzisha biashara ya kutumia mtaji mdogo au bila ya kuwa na
mtaji kabisa.
Mrisho Mpoto
Mrisho
Mpoto ametumia ukurasa wake wa facebook kutoa fursa tano ambazo anaona
kama vijana watazitumia zinaweza kuwa na tija katika maisha yao.
Biashara hizo alizozitaja Mpoto ni kama ifuatavyo:_
"1. Toa huduma.
Kama huna mtaji wa fedha, basi nina
uhakika una mtaji wa muda. Sasa tumia muda wako kutoa huduma ambayo
wengine wanaihitaji. Toa huduma kulingana na utaalamu wako, uzoefu wako
au ujuzi ulionao. Angalia ni namna gani unaweza kutumia muda wako
kuongeza thamani zaidi kwenye maisha ya wengine.
Kwa mfano kama wewe ni mwalimu, basi
unaweza kutenga muda wako wa ziada kutoa huduma ya kufundisha watoto
shuleni au hata majumbani mwao. Kama wewe unaweza kufanya kitu fulani,
basi tafuta wenye uhitaji wa kitu hiko na wasaidie kwa muda ulionao.
Unaweza kuwasaidia watu kwa kazi zao za nguvu au hata kazi zao za
kitaalamu. Unaweza kuwasaidia watu wanaofanya tafiti mbalimbali kwa muda
wako na utaalamu wako kwenye tafiti.
2. Biashara ya mtandao (network marketing).
Najua wengi mkisikia hii huwa mnakunja
sura na kuona kama mnapotezwa. Bado naendelea kusisitiza kama unataka
kuingia kwenye biashara na hujui wapi uanzie, basi ingia kwenye biashara
ya mtandao. Hii ni biashara ambapo unatumia bidhaa au huduma fulani,
kisha unawashawishi wengine nao watumie na unalipwa kamisheni kwa
manunuzi wanayofanya.
3. Biashara ya taarifa na maarifa.
Unaweza kuingia kwenye biashara ya kutoa
taarifa na maarifa. Kwa dunia ya sasa ambapo watu wengi wanatumia
mtandao wa intaneti, unaweza kutumia mtandao huu kutoa taarifa na
maarifa na kuweza kutengeneza kipato.
4. Kilimo biashara.
Kuna fursa kubwa sana kwenye kilimo cha
kibiashara, hasa kwa kilimo cha muda mfupi cha mboga mboga na matunda.
Kilimo hiki unaweza kuingia kwa mtaji kidogo na kama una muda wa kutosha
kukifuatilia kwa makini basi unaweza kuanza kidogo na kukua kadiri muda
unavyokwenda. Angalia kilimo kipi unaweza kuanza nacho na ukaribu wako
ili uweze kupata matokeo mazuri.
5. Biashara yoyote unayotaka kuanza, ila anza kidogo.
Unaweza kuanza biashara yoyote
unayopenda kuanza, hata kama ina uhitaji wa mtaji mkubwa, wewe anza
kidogo. Anza kwa hatua ya chini kabisa, weka juhudi kubwa na endelea
kuikuza.
Ukishaanza kuona matokeo mazuri, yaani
faida kwa hatua hiyo ndogo unayopiga, ni rahisi kuwakaribisha watu
wengine na wakakuchangia mtaji. Au hata kwenda kwenye taasisi za kifedha
na kuchukua mkopo."
Hiyo ni kwa mujibu wa Mrisho Mpoto
Post a Comment