RAIS
John Magufuli amesikitishwa na uzushi unaofanywa kwa lengo la kumchafua
Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na familia yake, na
amewataka waandishi wa habari na vyombo vya habari kuacha kuandika na
kuchapisha taarifa za uzushi na badala yake vizingatie weledi na kufuata
sheria.
Amesema taarifa
zinazomhusisha kwamba amezuia mizigo ya mke wa Rais mstaafu Kikwete,
Mama Salma Kikwete bandarini hadi hapo itakapolipiwa kodi, si kweli na
ni uzushi, kwani hajawahi kuzuia wala kuagiza kuzuiwa kwa mizigo ya Mama
Salma Kikwete.
Dk Magufuli aliyasema
hayo katika taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais, Ikulu, baada ya siku za karibuni, baadhi ya vyombo vya habari na
mitandao ya kijamii kuchapisha taarifa zinazomhusisha Mama Salma Kikwete
na Taasisi anayoiongoza ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) kwamba
imeshindwa kulipia kodi mizigo mikubwa iliyoiingiza nchini na hivyo kuwa
hatarini kupigwa mnada.
Aidha, taarifa hizo zimemhusisha Rais Magufuli kuwa anahusika kuzuia mizigo hiyo bandarini mpaka hapo itakapolipiwa kodi.
“Tunapenda kuutaarifu
umma kuwa taarifa hizo si kweli na ni uzushi, kwani Rais Magufuli
hajawahi kuzuia wala kuagiza kuzuiwa kwa mizigo ya Mama Salma Kikwete,”
ilieleza taarifa ya Ikulu.
“Rais Magufuli
amesikitishwa sana na uzushi huo unaofanywa kwa lengo la kumchafua Rais
mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete na familia yake na amewataka
waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini kuacha kuandika na
kuchapisha taarifa za uzushi na badala yake vizingatie weledi na kufuata
sheria,” ilibainisha taarifa ya Ikulu na kuongeza:
“Nimesikitishwa sana na
uzushi unaofanywa dhidi ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete na mke wake Mama
Salma Kikwete, tafadhali wale mnaotengeneza uzushi huu, acheni mara moja
na muacheni Rais mstaafu Kikwete apumzike.
“Rais mstaafu Kikwete
amefanya kazi kubwa ya kulitumikia Taifa hili, amestaafu anapumzika,
narudia muacheni apumzike, Serikali haitaendelea kuvumilia uzushi na
uchonganishi huu unaofanywa kwa makusudi ili kuwachafua viongozi
wastaafu,” ameonya Rais Magufuli.
Mwishoni mwa wiki, WAMA
ilikanusha taarifa zilizochapishwa na gazeti moja la kila wiki kwa lugha
ya Kiswahili kuwa Mwenyekiti wake, Mama Salma Kikwete ana mzigo mkubwa
bandarini ambao haujalipiwa ushuru na kodi.
Taarifa ya Wama
iliyosainiwa na Katibu Mtendaji wake, Daudi Nassib, ilisema taarifa hizo
ni za uongo na hazina ukweli wowote. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gazeti
hilo lilichapisha habari hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari, “Mali za
Salma Kikwete kuuzwa kwa mnada?” Katika toleo lake hilo la Novemba 30,
mwaka huu,
“Kumetolewa madai eti
kwamba taasisi ya Wama inayoongozwa na Salma Kikwete inao mzigo mkubwa
bandarini ambao haujalipiwa ushuru na kodi, hivyo Mamlaka ya Mapato
Tanzania imepanga kuuza mali hizo.
“Kwa niaba ya Taasisi ya Wama napenda kutoa masikitiko yetu kwamba habari hizo ni za uongo na hazina ukweli wowote.
“Kwa maoni yetu gazeti
hilo lina dhamira mbaya dhidi ya Taasisi ya Wama na Mwenyekiti wake
Salma Kikwete. Nia yao ni kupaka matope na kuchafua majina na sifa ya
taasisi yetu na kiongozi wake.”
Katibu Mtendaji huyo
alisema ukweli kuhusu jambo hilo ni kwamba, Wama ilitumiwa maboksi 11 ya
vitabu vikiwa ni zawadi kutoka Taasisi ya Nakayama ya Japan ambayo
ndiyo iliyofadhili ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wama-Nakayama iliyopo
Nyamisati, Kibiti na yalishatolewa bandarini tangu Agosti 10, mwaka huu
na tayari vitabu viko shuleni na vinatumika.
“Hakuna mzigo wowote wa
Taasisi ya Wama uliopo bandarini unaosubiri kutolewa wala kuuzwa na
TRA,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kulitaka gazeti hilo kuomba
radhi kwa Salma Kikwete na kwa Wama kutokana na taarifa hizo.
Post a Comment