Mwajuma Ally Ramadhan,dereva
ni mhudumu wa ofisi katika kampuni ya
TBL kiwanda cha Arusha na anasema
kuwa anaifurahia kazi yake na anatoa ushauri kwa wanawake wenzake kupambana na
maisha na kutokata tamaa.
“Maisha siku zote sio lelemama
kinachotakiwa ni kupambana , kutokata tamaa,kuwa na malengo,na kuchukia kuishi
maisha ya utegemezi wakati nguvu na akili za kufanya kazi unazo”.Anasema
Mwajuma.
Mwajuma anatoa ushauri kwa
wazazi kutowadekeza watoto hasa wa kike ili wakiwa watu wazima wawe na uwezo wa
kujimudu kufanya kazi mbalimbali zinazowawezesha kujipatia kipato na kuendesha
vizuri maisha yao.
Akielezea historia yake yake
ya kazi alisema kuwa tangu alipokuwa na umri mdogo alikuwa anapenda sana kuwa
mwanamichezo na alipokuwa anasoma shule ya msingi Wilayani Handeni mkoani Tanga
alishiriki kucheza mchezo wa netiboli katika timu ya shule na aliendelea
kucheza mchezo huo hata alipokuwa
anasoma sekondari.
“Mchezo wa netiboli ndio
umenifikisha hapa nilipo kwa kuwa nilijiunga na kampuni ya TBL mwaka 1988
nikiwa mchezaji wa netiboli kwenye timu ya kampuni ambapo baadaye ndipo
niliajiriwa kama mhudumu wa ofisi “.Anasema.
Mwajuma alisema baada ya
kufanya kazi ya uhudumu wa ofisi kwa muda mrefu aliamua kujifunza kozi ya
udereva katika chuo cha Kilimanjaro Driving School ambapo alifuzu na kuweza
kupata leseni ya kuendesha magari madogo.
Baada ya kupata leseni mwajiri
wake aliweza kumpandisha daraja kuwa dereva wakati huohuo akifanya kazi ya
uhudumu “Hivi sasa naendesha magari ya kampuni na naaminika kufanya kazi
mbalimbali ikiwemo kupokea wageni wa kampuni
na kuwazungusha kwenye ziara za kazi,naifurahia kazi yangu na kuipenda
na nina mabosi wanaotoa ushirikiano ambao mara zote hunitia moyo na
kuniongoza”.Anasema.
Kuhusu changamoto
anazokabiliana nazo katika kazi yake alisema zipo changamoto za kawaida kama zilizopo
kwenye kazi nyingine . “Wakati mwingine hujitokeza hitilafu kwenye gari au
kupata pancha inakuwa shida kurekebisha hali hiyo au wakati mwingine unapokuwa
kwenye mizunguko ya kikazi unajikuta unafanya kazi masaa mengi na kuwa na muda
mchache wa kukaa na familia.
Mwajuma ambaye ni mama mwenye
watoto anasema kuwa anafurahi kufanya
kazi katika kampuni kubwa ya TBL kwa kuwa ina mifumo mizuri ya ajira yenye
maslahi mazuri ikiwemo taratibu za kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara
wafanyakazi wake na anakiri kuwa ajira
yake imemwezesha kujua mambo mengi na kupata mafanikio kimaisha.
Kuhusu mipago yake ya baadaye
alisema kuwa anatamani kujifunza kuendesha magari makubwa na alimalizia kwa kuwataka akina mama
wajitokeze na kujiamini kufanya kazi zote bila kuchagua kwa kuwa hakuna kazi
kwa ajili ya wanaume peke yao au wanawake peke yao.
Post a Comment