Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
Sera, Uratibu na Bunge; Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Bibi
Jenista Mhagama (Mb) akieleza jambo
wakati alipokutana na wafanyakazi wa Shirika la Tija la Taifa (hawapo pichani)
alipolitembelea shirika hilo Januari 15, 2016.
Na. Mwandishi Maalum
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera,
Uratibu na Bunge; Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista
Mhagama (Mb) ameuagiza uongozi wa Shirika la Tija la Taifa kuwa wabunifu
katika utoaji wa elimu kwa umma ili jamii iweze kujua kazi na huduma
zinazotolewa na shirika hilo.
Mhe. Mhagama ametoa agizo hilo alipotembelea Shirika la Tija la
Taifa (NIP) Januari 15,2016 kwa lengo la kujionea kazi zinazotekelezwa pamoja
na changamoto zinazolikabili shirika hilo.
“Uongozi lazima uangalie changamoto zinazolikabili shirika hili
na kuangalia namna ya kugeuza changamoto hizo kuwa fursa muhimu na kutoa elimu
kwa umma wa Watanzania ili wajue umuhimu wa kutumia huduma yenu kwa lengo la
kujiletea maendeleo,”alisema Mhagama
Waziri alielekeza kuwa lazima viongozi wa NIP wawe wabunifu
katika kutumia vyombo mbalimbali vya habari vinavyoweza kuwafikia wananchi wa
aina zote huku akisisitiza kuangalia vipindi ambavyo havihitaji kulipiwa.
"Nendeni mkaongee na wadau wa vyombo vya habari maana
utakuta kuna fursa nyingi mngeweza kuzitumia bila gharama yoyote. kuna vipindi
kama vile Kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC 1, kipindi cha Kumekucha cha ITV,
kipindi cha 360 Clouds Tv na Tuongee asubuhi cha Star Tv na vingine vingi
amabavyo mnaweza kuvitumia kuwafikia wananchi wengi," alisisitiza Mhe. Mhagama.
Waziri alisema kuwa kwa kutumia ubunifu na fursa zilizoko
kwenye vyombo vya habari shirika litapata kujitangaza bila kutumia gharama na
kuweza kuyafikia malengo kama kuboresha ujuzi na uelewa wa usimamizi wa
rasilimaliwatu, kuchapisha na kusambaza fasihi na kuboresha utendaji wa Taasisi
za umma na zisizokuwa za umma.
Wakati akimkaribisha waziri, Mkurugenzi Mtendaji wa NIP
Bw.Novatus Massao alieleza kuwa miongoni mwa changamoto zinazokabili shirika
hilo ni suala la taswira hasi kwa jamii na uelewa mdogo wa jamii kuhusu
faida na umuhimu wa Shirika hilo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Bodi ya NIP, Prof.Samwel Wangwe
aliahidi kuwa shirika hilo litahakikisha linatekeleza maagizo yote ya Mhe. Mhagama
ili kuwezesha watanzania kuelewa na kutumia huduma za shirika hilo.
Aidha, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala Bw.Raphael Loishiye
alimshukuru Mhe. Waziri kwa kufanya ziara katika Shirika hilo na kujionea mazingira
na changamoto wanazokabiliana katika utekelezaji wa majukumu yao |
Post a Comment