Rais John Magufuli jana aliungana na
wananchi katika kufanya usafi ambapo akiwa katika eneo la Feri jijini
Dar es Salaam, ameweza kuzungumza moja kwa moja na wavuvi wadogo.
Baada ya kusikiliza kwa makini kero
zinazowakabili wavuvi hao wadogo akiwa amekaa ndani ya kifaa duni cha
kufanyia uvuvi maarufu kama ‘mtumbwi’ usio na mashine, rais Magufuli
aliwaahidi wavuvi hao kuzitatua kero hizo.
Kati ya mambo matatu aliyoahidi
kuyafanyia kazi kwa haraka ni pamoja na kuondoa masharti kuwa kuwa na
‘Fire Extinguisher’ ambapo alieleza kuwa sharti hilo halina mashiko kwa
wavuvi hao wadogo wasio na mashine.
“Kwanza maji yenyewe tu ni ‘fire extinguisher’, si moto ukianza unaingia ndani ya maji,” alisema Dk. Magufuli.
Kadhalika, rais aliahidi kuwasaidia
wavuvi hao kwa masharti ya kuunda umoja wao ambao utakuwa na viongozi
waadilifu wanaofanya kazi kwa maslahi ya wavuvi hao na sio maslahi ya
‘wakubwa’. Alieleza kuwa atalifanyia kazi suala la wavuvi hao
kukopesheka na kuwasaidia kuwa na vifaa bora.
Aliongeza kuwa atahakikisha anafuta ushuru kwa wavuvi hao wadogo ili kuwaondolea kero na mzigo wa gharama.
Pia, alisema atahakikisha anaanza kuwasaidia kadiri awezavyo wavuvi wa eneo la Feri kwa kuwa ni majirani zake.
“Katika kudhihirisha ujirani mwema, hayo matatizo nitayabeba.”
Hata hivyo, rais aliwataka wavuvi hao kuhakikisha hawajihusishi na uvuvi haramu wa kutumia sumu na mabomu.
Katika hali ambayo wengi hawakuitegemea,
rais Magufuli alimpa mmoja kati ya wawakilishi wa wavuvi hao namba yake
ya simu na yeye akachukua namba ya watu wawili kati yao.
Akiongea na waandishi wa habari baada ya
zoezi hilo, Dk. Magufuli aliwashukuru watanzania wote kwa ujumla kwa
kuitikia wito wake wa kufanya usafi huku akieleza kuwa hili linapaswa
kuwa zoezi endelevu kwani uchafu hauwezi kuisha kwa kufanya usafi mara
moja kwa mwaka.
Post a Comment