Mwenyekiti wa zamani wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema Rais wa
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ndiye mtu pekee mwenye uwezo wa kumaliza
mgogoro wa Zanzibar.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Profesa Lipumba alisema mgogoro wa
Zanzibar utamalizwa kwa Dk Shein kuiruhusu Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar
(ZEC) kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25.
Alisema pamoja na mazungumzo yanayoendelea kati ya CUF na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk Shein ndiye mwenye uwezo kuumaliza mgogoro
huo.
“Mazungumzo yanaendelea na hatujui yatafika mwisho lini, lakini Dk
Shein ndiye anayeweza kuifanya Zanzibar iwe na amani au vurugu,
ninashauri aruhusu kutangazwa kwa matokeo,” alisema.
Alisema amani na utulivu uliopo Zanzibar wakati wananchi wakisubiri
hatima ya mgogoro huo, haiwezi kuwa ya kudumu kwani ikiamuliwa uchaguzi
urudiwe wapo ambao hawatakubali.
Profesa Lipumba alisema uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa huru na haki na
hata watazamaji wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali walishangaa matokeo
yake kufutwa.
Alisema wananchi wa Zanzibar walishapiga kura na kwamba wanachosubiri ni
matokeo vinginevyo haki yao ya kidemokrasia itakuwa imechezewa.
Oktoba 28 mwaka huu, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha alifuta
uchaguzi huo kwa kile alichosema kulikuwa na kasoro ndani ya tume
yenyewe na kwenye vituo vya kupigia kura.
Profesa Lipumba alisema mgogoro huo ukiendelea, utakwamisha msaada wa
Dola za Marekani 472.8 milioni uliokuwa utolewe na Shirika la Maendeleo
ya Milenia (MCC) la Marekani.
Alisema Bodi ya MCC ilikutana Desemba 16 na kushindwa kupitisha msaada
huo kwa Tanzania huku hoja kubwa ikiwa kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi
Mkuu Zanzibar.
Alisema miongoni mwa matumizi ya msaada huo ilikuwa kuunganisha wateja wapya 300,000 kupata umeme.
“Hapa tunategemea busara za Dk Shein kuumaliza mgogoro ili tupate
msaada huo wenye masilahi ya Taifa au kuendelea na mgogoro na kuukosa
msaada huo,” alisema.
Akizungumzia suala hilo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena
Sakaya alisema huu ni muda mwafaka kwa Dk Shein kuweka masilahi ya
Wazanzibari mbele.
Alisema atawekwa kwenye vitabu vya historia kama atafanya uamuzi wa
kuruhusu kutangazwa kwa matokeo hata kama viongozi wenzake wa CCM
hawatapenda uamuzi huo.
Post a Comment