MAWAZIRI wawili jana ‘walitumbua majipu’
baada ya kutangaza kusimamishwa kazi kwa Mtendaji Mkuu wa Mradi wa
Mabasi yaendayo Haraka (DART), Asteria Mlambo na Kaimu Mkurugenzi wa
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk Diwani Msemo, wote wakipisha
uchunguzi dhidi yao.
Mlambo amesimamishwa kazi kuanzia jana
ili kupisha uchunguzi baada ya serikali kubaini ukiukwaji wa wazi wa
Sheria ya Manunuzi ya Umma katika kumpata mtoa huduma ya mpito wa mradi
huo wenye nia ya kupunguza msongamano wa magari barabarani kwa madhumuni
ya kurahisisha usafiri na usafirishaji jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, George Simbachawene alisema kutokana na kukamilika
kwa sehemu ya ujenzi wa miundombinu ya Awamu ya Kwanza ya mradi,
Serikali iliamua kuwa na mtoa huduma wa mpito kabla ya kumpata wa
kudumu.
“Mtoa huduma wa mpito alipaswa
kupatikana kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma. Hata hivyo,
Serikali imebaini ukiukwaji wa wazi wa sheria hiyo wakati wa kumpata
mtoa huduma wa kipindi cha mpito.
“Kufuatia hali hiyo nimeamua
kumsimamisha kazi kuanzia leo tarehe 23 Desemba, 2015, Mtendaji Mkuu wa
DART, Bi. Asteria Mlambo ili kupisha uchunguzi,” alieleza Simbachawene.
Simbachawene alizitaja sababu za
kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu huyo wa DART kuwa ni kushindwa
kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma wakati wa kumpata mtoa huduma
katika kipindi cha mpito; kushindwa kuchukua hatua hata pale alipobaini
kuwa mtoa huduma wa mpito amekiuka masharti ya mkataba wa kutoa huduma
ya mpito; na kufanya maamuzi makubwa pasipo kuishirikisha Bodi ya
Ushauri ya DART.
Aidha, alisema Serikali inatambua kuwa
wapo watumishi wa DART ambao hawakumshauri vizuri Mtendaji Mkuu, hivyo
watumishi hao watachunguzwa na kuchukuliwa hatua na Kaimu Mtendaji Mkuu
atakayeteuliwa.
“Nimemwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi kuendelea na taratibu za kinidhamu dhidi ya Mtendaji Mkuu aliyesimamishwa kazi,”
alisema Simbachawene. Aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea
kuchukua hatua kwa haraka na uangalifu ili mradi huu uanze kutoa huduma
bora ya usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam bila kuchelewa zaidi, huku
akiwaomba kuitunza na kuithamini miundombinu ya DART kwa kuwa imegharimu
fedha nyingi kwa manufaa yao.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa alitembelea maeneo ya mradi huo wa DART na kuagiza kuwa uanze
kazi Januari 10, mwakani baada ya kupigwa kalenda kwa muda sasa tangu
mwaka jana.
Wakati Simbachawene akichukua hatua
hiyo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu amemsimamisha Dk Msemo kwa kile kilichoelezwa ni kupisha
uchunguzi unaolenga kubaini iwapo mgongano wa kimaslahi umeathiri
utendaji wa taasisi hiyo.
Aidha, watendaji wote wa serikali katika
sekta ya afya hususan wakuu wa vituo vya kutolea huduma za afya,
wafamasia, wauguzi na waganga wafawidhi, wameagizwa kukiri kwa maandishi
ndani ya siku 21 kuanzia sasa endapo wanamiliki hospitali, zahanati,
kliniki na maduka ya dawa.
Taarifa kwa vyombo vya habari
iliyosainiwa na Waziri Mwalimu, imefafanua uamuzi wa kumsimamisha Kaimu
Mkurugenzi huyo wa Ocean Road, unatokana na ziara walizofanya kukagua
utoaji wa huduma za afya katika maeneo mbalimbali ambako walibaini
upungufu wa dawa umeendelea kujitokeza kwa wingi.
“Baadhi ya wagonjwa walieleza kwa
uchungu jinsi wanavyopata tabu ya kupata dawa hata zile ambazo
wanatakiwa wazipate kwa bei ya ruzuku au zinazotakiwa kutolewa bure na
serikali,” ilisema taarifa hiyo.
“Kwa kuzingatia suala hili la
mgongano wa kimaslahi, manung’uniko mengi kutoka kwa wapokea huduma,
hususan katika Taasisi yetu ya Saratani ya Ocean Road, nimechukua hatua
ya kumsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi,” iliongeza taarifa ya waziri huyo.
Post a Comment